Habari za Punde

Mwakilishi akabidhi dawa Pemba

Na Haji Nassor, Pemba
VIFAA tiba na dawa za matumizi ya binadamu zenye thamani ya zaidi ya shilingi 15 milioni, zilizotolewa wiki iliopita na Mwakilishi wa Jimbo la Chake chake Mhe: Omra Ali Shehe, kwa hospitali kuu ya Chake chake, vimegundulika kupitiwa na muda na baadhi yao tokea mwaka 2011.
Vifaa hivyo vikiwemo kwa ajili ya mama wajawazito, wagonjwa waloziba mkojo, glavu, pamba za kusafishia meno, vifaa vya kupitishia hewa kabla na wakati wa operesheni, sindano na dawa baada ya kuungua moto, vimegunduliwa na madaktari wa hopsitali hiyo wakati walipokuwa wakizichambua kwa ajili ya kuanza matumizi.
Mfamasia mkuu wa hospitali hiyo dk Kassim Zahir, alisema baadhi ya dawa na vifaa hivyo tiba, vipo baadhi havijapitiwa na muda ingawa vyengine vilishapitiwa na matumizi ya binadamu miaka minne iliopita.
Akizungumza na waandishi wa habari hospitali hapo baada ya vifaa hivyo kutengwa kwa ajili kukabidhiwa Mwakilishi huyo, alisema kama hawakuwa waangalifu wangeteketeza afya za wagonjwa wao.
Alisema dawa kama za kusafishia sehe za siri, pamba za kusafishi meno vifaa vya kuweka mdomo vyenge sababisha kensa kwa wananchi watakaofika hopsitali hapo wakihitaji huduma za matibabu.

Mfamasia huyo alisema anashangaa kuona baadhi ya dawa hizo ambazo walikabidhiwa kama msaada na Mwakilishi huyo wa Jimbo la Chake chake, vipo ambavyo muda wake umeshamalizika tokea Disemba mwaka 2011, Machi 2013, pamoja na Machi mwaka 2014.
“Kwa kweli tulitarajia kwamba alau kuwe na dawa zilizopitwa na mda miezi sita nyuma, mitatu au miinne lakini miaka mine na mitatu ni jambo la hatari kwa wenzetu wanaotuletea misaada ya dawa’’,alilalamika Mfamasia huyo.
Kwa upande wake daktari dhamana wa hospitali hiyo Dk Yussf Hamad Idd, alisema baada ya kugungua dawa hizo mchanganyiko na vifaa tiba vyenye tahamani ya shilingi 15 milioni, sasa wanawasiliana na Mwakilishi huyo ili kumkabidhi.
Alisema hatua hiyo ya kumkabidhi ni kufanya taratibu za kisheria ili kuziangamiza kwa vile gharama ya zoezi hilo humuelekea mwenye kuleta mzigo ambao ambao umeshapitiliza muda wake (expire date).
Alisema anaamini nia ya Mwakilishi huyo sio kuwapatia dawa na vifaa hivyo ambavyo havitumiki, bali kulikua na ufahamu mdogo wakati wa ununuzi au uwagishiaji.
Hata hivyo dk dhamana huyo alisema haamini sana kwamba kabla ya kufanya taratibu hizo, kwamba Mwakilishi huyo aliwasiliana na uongozi wa wizara ya afya, kwani vipo baadhi ya vifaa vya wanawake hawavihitaji kwa mazingira ya Zanzibar.
“Ipo mirija maalumu kwa ajili uchunguzi wa wanawake, lakini mirija tuliokabadhiwa kwa kwetu hayafai hata kama hajapitiwa na muda wake wa matumizi maana ni mikubwa kuliko maumbile’’,alifafanua.
Baadhi ya wananchi waliwataka wafadhili wa majimbo na wengine wanapohitaji vifaa tiba na dawa kwa ajili ya matumizi ya mwanadamu kuwasiliana na uongozi wa hospitali husika ili kuepusha kupatiwa vifaa visivyostahili.
Mmoja wa wananchi hao Ali Kassim Hassan alisema inawezekana Mwakilishi huyo hakununua mwenyewe vifaa hivyo na pengine ametapeliwa bila ya yeye mwenyewe kufahamu.
Nae Asha Kombo Haji alisema kama sio uwelewa wa madaktari wa hospitali ya Chake chake wagonjwa watakaofika hospitali hapo wengeongezewa mradhi kwa kuwepo dawa mbovu.
Mwakilishi wa Jimbo la Chake Chake Mhe: Omar Ali Shehe alipotafutwa kwa njia ya simu kujibu kadhia hiyo, alisema yeye hafahamu kwamba dawa hizo zimeshapita muda wake kwa vile na yeye alipewa msaada.
Alisema dawa hizo na vifaa tiba alipewa msaada kutoka Uingereza na wala hafahamu jinsi zilivyokuwa zimefungwa (package) bali anachoamini alipewa dawa hizo kwa nia safi.
“Mimi sio mtaalamu wa dawa ukiniambia mirija na sindano zimetiwa pamoja wakati ni kosa sielewi, maana mimi sina utaalamu wa kupeki dawa’’,alifafanua kwa njia ya simu.
Hata hivyo alisema kama zimo dawa ambazo hazifai kwa matumizi ya mwanadamu ni vyema madaktari hao kuzitenga mbali kwa ajili kuangamiziwa, kwani lengo haiku Zanzibar kuifanya jaa kwa dawa mbovu.
Mwakilishi huyo wa Chake chake alisema msaada huo aliopokea kutoka kwa vijana wa kizanzibari walioko Uingereza ingawa kwa bahati mbaya bila ya yeye kufahamu ndio hilo lililojitokeza.
“Mimi siamini kwamba waone dawa  na vifaa tiba vimeshaharibika wavilete, bali ni kosa la kibinadamu lililojitokeza, na kwa hio zitengwe zisitumike’’,alifafanua.

Mei 3 mwaka huu, Mwakilishi nafasi za wanawake wilaya ya Chake chake Salma Mohamed Ali kwa niaba ya mwakilishi wa Jimbo la Chake  Chake Mhe: Omar Ali Shehe alikabidhi dawa na vifaa tiba mbali mbali kwa uongozi wa hospitali ya Chake chake ambapo baadhi ya hivyo havifai

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.