Habari za Punde

Umoja wa Mataifa Wawaenzi Walinda Amani Wake.

 Maura  Mwingira, Charge d' affaires a.i wa Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa,  akipokea kutoka kwa  Mkuu wa Idara ya Operesheni za Ulinzi wa Amani za  Umoja wa Mataifa ( DPKO ) Bw. Harves Ladsous,  Medali  Maalum ya  Dag Hammarskjold  ambazo wametunukiwa  Mashujaa wanne walinda Amani  kutoka JWTZ ambao walipoteza maisha mwaka  2014  wakati wakitekeleza majukumu yao. Umoja wa Mataifa umeitenga  Mei 29 kama siku ya  Kimataifa ya  kuwakumbuka na kuwaenzi walinda amani  ambao walipoteza maisha katika misheni mbalimbali za Umoja wa Mataifa. Jumla ya  walinda amani  126 walipoteza maisha mwaka jana . Medali hizo  zitawasilishwa kwa Familia za Mashujaa   hao.
  Maura Mwingira wa Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, akiandika katika kitabu maalum,  baada ya kupokea  kwa niaba ya  familia  za mashujaa  wanne wa JWTZ waliopoteza maisha wakati wakihudumu katika misheni za kulinda amani mwaka jana.  Medali hiyo  maalum  ya Dag  Hammarskjold  ilitokwa  siku ya  ijumaa kama  ishara ya kuwaenzi, kutambua na kuthamini mchango mkubwa wa mashujaa hao.

Mpiga Buluji akiimba wimbo maalum wa  maombolezo kama ishara ya kuwakumbuka mashujaa 126 walinda amani waliopoteza maisha  mwaka jana. shughuli za utoaji wa medali  maalum zilitanguliwa na uwekaji wa  shada maalum la maua katika eneo ambalo limetengwa katika viunga vya Umoja wa Mataifa .Pichani anaonekana Katibu Mkuu Ban Ki Moon akitoa salamu za heshima kwa wahanga hao anaonekana pia Naibu Katibu Mkuu  Jan Eliasson

Na  MwandishiMaalum,  New York
Mashujaa Private Ally Salum Jumanne, Private Mohamed John Mbizi,  Private Vasco Adrian Msigala na Sajent Hamis Juma Nyange kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ni miongoni mwa mashujaa 126 ambao siku ya Ijumaa,  Umoja wa Mataifa uliwatunuku medali ya  Dag Hammarskjold
Ijumaa ya Mei 29 ya kila mwaka Umoja wa Mataifa umeitenga kama siku
maalum ya kutambua na kuenzi mchango wa walinda Amani ambao wamepoteza maisha wakati wa kitekeleza majukumu ya ulinzi wa Amani kupitia operesheni za Umoja wa Mataifa.

Katika adhimisho
hilo na ambalo lilihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa,  Ban ki moon,   Naibu wake  Jan Eliasson,  na Wakuu wa Idara za Ulinzi za Umoja wa Mataifa,  jumla ya mashujaa 126  kutoka nchi 38 waliopoteza maisha mwaka jana (2014) walienziwa kwa kutunukiwa medali maalum ya Dag Hammarskjold.

Adhimisho hilo lilitanguliwa na uwekaji wa shada la maua kwa heshima ya mashujaa hao,  shada liliwekwa na Katibu Mkuu  Ban Ki Moon  katika sehemu maalum ambayo imeandaliwa kwa ajili ya kumbukumbu hiyo.
Akizungumza kwa masikitiko makubwa wakati wa hafla hiyo, Katibu Mkuu, Ban Ki Moon,  amesema, katika maadhimisho yote yanayofanyika katika Umoja wa Mataifa,   hakuna adhimisho lenye kutiasimanzi na ngumu kama hili la kuwakumbuka na kuwaenzi walinda amani ambao wamepoteza maisha yao wakati wa kitoa ulinzi kwa watu wengine.



“ Ninasikitika kusema kwamba,   hii ni mara ya saba mfululizo ambapo zaidi ya walinda amani 100 wamepoteza maisha katika kipindi cha mwaka mmoja. 
Hatari wanayokumbana nayo walinda amani wetu inazidi kuongezeka kwa kasi kubwa,  kutokana  kushambuliwa na makundi ya wahafidhina na makundi ya wanamgambo wenye silaha mpaka hatari ya magonjwa ambukizi kama  vile  Ebola” amesema KatibuMkuu.

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa akaendelea kusema.  
“ Tumekusanyika hapa kuwaenzi mashujaa wetu waume kwa wake ambao wamepoteza maisha yao wakati wakiwalinda wananchi katika maeneo hatari duniani. Kujitoa kwao muhanga na namna walivyo ishi maisha yao,  wanatufanya sisi tujisikie fahari na kututia shime ya kufanyakazi kwa bidii zaidi ili kudhihirisha kwamba maisha yao hayakupote abure.
Ban Ki Moon,  awaeleza wawakilishi kutoka nchi ambazo zimepoteza mashuja wake kwamba,  operesheni za ulinzi wa amani chini ya Umoja wa Mataifa zitaendelea kuwa zenye changamoto na hatari kubwa, na cha kusikitisha ni kwamba adhimisho lililofanyika ijumaa la kuwaenzi mashujaa hao halitakuwa la mwisho
“Walinda amani wetu wanabeba jukumu zito kwa ajili yetu sote.
Natoa heshima zangu kwa mashujaa na salamu zangu za pole kwa familia za mashujaa hawa” akasisitiza Katibu Mkuu.

Walinda amani hao 126 naraia 19 wamepoteza maisha wakati 
wakihudumia katika misheni zilizopo, Afghanistan,  Jamhuri ya Afrika ya  Kati, Ivory Coast, Cyprus, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Haiti, Mali,  Mashariki ya Kati, Liberia, Sudan na Sudan ya Kusini
Pamoja na Tanzania  nchi nyingine ambazo zimepoteza mashujaa wake katika misheni mbalimbali za kulinda Amani katika mwaka uliopita ni  Senegal,  Afrika ya Kusini, Uhispania, Togo, Rwanda, Benin, Burkina Faso,  Bangladesh,na  Burundi.

Nyingine ni  Cambodia,  Chad, El Salvador, Ethiopia, Fiji, France, Ghana,  India, Indonesia,  kenya , Malawi, Niger,  Pakistan,  Philippines, Tunisia na Zimbabwe.

Pamoja na mashujaa hao ambao ni wanajeshi, wapo pia raia 19 wakiwamo pia polisi, Madaktari, watumishi na watoa misaada ya kibinadamu ambao wamepoteza maisha wakati wa kitoa misaada kwa binadamu wenzao.

Wakati Umoja wa Mataifa ukiwaenzi mashujaa hao waliopoteza maisha mwaka jana. Tayari mwaka huu wa 2015 mashujaa wapatao 49 wamekwisha poteza maisha wakitekeleza majukumu yao ya kuleta Amani ,utulivu na ulinzi wa raia wasiona hatia katika nchi zenye migogoro. Kati ya mashujaa 49 hao wapo watanzania wawili.

Jumla ya walinzi wa Amani 3,300 wamekwisha kupoteza maisha tangu kuanzishwa kwa Operesheni za Ulinzi wa Amani  chini ya Umoja wa Mataifa mwaka 1948.



No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.