Habari za Punde

Balozi Seif Atembelea Kituo cha Michezo cha Filbert Bayi Mkuza Kibaha

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akisalimiana na Mwanariadha mkongwe wa Kimataifa wa Zanzibar  Suleiman Ame { Nyambui  } mara alipowasili katika Kijiji cha Filbert Bayi kufunga mashindano ya 54 ya Taifa ya Riadha Zanzibar.Kushoto ya Balozi Seif ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarest Lihilo.

Washindi wa mbio za Mita 1,500 kwenye mashindano ya riadha Taifa wakati ni mshindai wa kwanza wa mbio za Mita 1,500 Gabriel Gerald wa Mkoa wa Arusha, Kushoto yake mshindi wa pili Agostino Sudi wa Mkoa wa Arusha na kulia yake Silvester Simon wa Mkoa wa Kilimanjaro.
Balozi Seif akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Shirikisho la Riadha Tanzania pamoja na washindi wa mbio za Mita 1,500 alizozishuhudia mwishoni mwa fainali za mashindano ya Riadha Taifa.Kulia ya Balozi Seif ni Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo wa SMT MH. Juma Suleiman Ngamia, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Kanali Mstaafu Juma Kassim Tindwa,Mwenyekiti wa shirikisho la Riadha Zanzibar Abdulhakim Cosmas wakati kushoto yake ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarest Lihilo na Mkuu wa Wilaya ya  Kibaha Halima Kihemba.Nyuma ya Babozi Seif Kati kati ni mshindai wa kwanza wa mbio za Mita 1,500 Gabriel Gerald wa Mkoa wa Arusha, Kushoto yake mshindi wa pili Agostino Sudi wa Mkoa wa Arusha na kulia yake Silvester Simon wa Mkoa wa Kilimanjaro.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kati kati waliosimama akiwa katika picha ya pamoja na Mabingwa wa Mashindano ya 54 ya Taifa Riadha Tanzania Mkoa wa Mjini Magharibi mara baada ya kuyafunga mashindano hayo Mkoani Pwani.
(Picha na OMPR)

Na Othman Khamis OMPR
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema wakati umewadia kwa wanamichezo Nchini kufanyakazi kisayansi ili kuodoa mapungufu yanayopatikana katika sekta hiyo na kuirejeshea Heshima yake Tanzania katika Nyanja ya michezo Kimataifa.

Alisema Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imewahi kujiwekea rekodi nzuri ya ushindi Kimataifa hasa katika Mchezo wa Riadha ambapo ilipata nafasi ya kunyakua Medali mbali mbali kutokana na juhudi kubwa iliyokuwa ikifanywa na shirikisho la Riadha Nchini Tanzania.

Balozi Seif alieleza hayo wakati akiyafunga mashindano ya 54 ya Taifa ya mchezo wa Riadha yaliyokuwa yakifanyika kwa siku Tatu katika Shule ya Filbert Bayi Mkuza Kibaha Mkoani Pwani ambapo Mikoa 21 kati ya 30 ya Tanzania Bara na Zanzibar ilishiriki kwenye mashindano hayo.

Alisema wanamichezo lazima wajiwekee malengo ya muda mfupi na mrefu wakati wanapohitaji mafanikio kwenye michezo yao na Serikali iko tayari kushirikiana kwa karibu na wanamichezo hao kwa nia ya kurejesha Heshima ya Tanzania iliyojengeka zamani.

Balozi Seif alifahamisha kwamba yapo mashindano mbali mbali ya Kimataifa ambayo Tanzania itawajibika kushiriki. Hivyo matayarisho ya mapema ni jambo la lazima katika hatma ya kufanikisha ushindi  kwenye mashindano hayo.

“ Tunayo mashindano ya Riadha ya Dunia yanayotarajiwa kufanyika mwezi Agosti mwaka huu Nchini China, mashindano ya Afrika Mwezi Septemba mwaka huu Nchini Congo Brazaville ya yale ya Olympiki 2016 Reo De Janairo Brazil  ambapo tutalazimika kujizatiti ili kushiriki vyema na kurudi na ushindi “. Alisema Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kuwa Taifa linatambua umuhimu wa Michezo na ndio maana Serikali zote mbili ile ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Mapinduzi ya Zanzibar ziliamuwa kuunda Wizara Maalum zinazosimamia na kushughulikia sekta ya Michezo.

Alifahamisha kwamba Michezo imeweza kuwaunganisha Watanzania kuwa kitu kimoja pamoja na kujenga ujirani mwema na urafiki kati yake na wenzao wa mataifa jirani.

Balozi Seif ambaye aliwahi kuwa mwanamichezo wakati wa enzi zake aliwanasihi washiriki walioshinda kwenye mashindano hayo ya kitaifa wasiridhike na ushindi walioupata na badala yake wajiwekee malengo ya kushinda katika michezo mengine ya Kimataifa watakayobahatika kushiriki.

1 comment:

  1. Wanamichezo hao wanapaswa kuzingatia ushauri huo kwani ndiyo mwelekeo wa wao kufikia hatua wanayoitaka

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.