HOTUBA YA RAIS WA
ZANZIBAR NA
MWENYEKITI WA BARAZA
LA MAPINDUZI
MHESHIMIWA DK. ALI
MOHAMED SHEIN,
WAKATI WA KULIVUNJA
BARAZA LA NANE LA
WAWAKILISHI, TAREHE
26 JUNI, 2015
Mheshimiwa Pandu Ameir Kificho,
Spika wa Baraza la Wawakilishi,
Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi,
Makamu wa Pili wa Rais,
Mheshimiwa Omar Othman Makungu,
Jaji Mkuu wa Zanzibar,
Waheshimiwa Wenyeviti wa Baraza la
Wawakilishi,
Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza la
Wawakilishi,
Waheshimiwa Mabalozi wadogo mlioko Zanzibar,
Wawakilishi wa Mashirika mbali mbali ya
Kimataifa,
Waheshimiwa Viongozi wa Vyama vya Siasa,
Ndugu Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana,
Assalam Aleikum
UTANGULIZI:
Mheshimiwa
Spika,
Awali ya yote, naanza hotuba yangu kwa
kumshukuru Mwenyezi Mungu; Mwingi wa Rehema na Utukufu kwa kutujaalia afya
njema na uhai tukaweza kukutana katika hadhara hii muhimu. Namuomba Mwenyezi Mungu atujaalie kila la
kheri katika utekelezaji wa wajibu wetu huu wa kikatiba.
Kadhalika, nawapa pole wale wote
walioathirika na maafa ya kipindi cha mvua kubwa za hivi karibuni zilizopelekea
watu watatu kupoteza maisha na wengine kupoteza mali na uharibifu mkubwa wa
nyumba na mazingira. Aidha, tunawashukuru
wale wote walioungana na Serikali katika kutoa misaada mbali mbali ya
kuwafariji ndugu zetu waliofikwa na maafa hayo.
Tunawaomba ndugu zetu hao walioathirika waendelee kuwa na nyoyo za
subira na Mwenyezi Mungu awape uwezo wa kukabiliana na mitihani iliyowasibu.
Mheshimiwa
Spika,
Napenda kutoa shukrani za dhati kwako na
Baraza lako tukufu kwa kunipa nafasi hii ya kuja kulihutubia Baraza hili la
Nane kabla ya kulivunja. Kwa hivyo,
kikao hiki cha leo kimeitishwa kwa ajili ya kutekeleza matakwa ya Kikatiba kwa
mujibu wa mamlaka niliyopewa katika Kifungu cha 91(2) (a) cha Katiba ya
Zanzibar ya mwaka 1984. Kadhalika, kikao
chetu hiki ni utekelezaji wa Kifungu cha 92(1) cha Katiba ya Zanzibar kuhusiana
na uhai wa Baraza la Wawakilishi kuwa ni kipindi cha miaka mitano tangu
ulipoitishwa mkutano wa kwanza na leo tarehe 26 Juni, 2015 ndiyo nalihutubia Baraza
la Nane kwa mara ya mwisho kabla ya kulivunja ili kupisha Uchaguzi Mkuu wa
mwaka 2015.
Napenda nitumie fursa hii ili nitoe shukrani
zangu za dhati kwako Mheshimiwa Spika kwa uongozi wako bora na kwa kazi kubwa
uliyoifanya katika kipindi cha miaka mitano ya Baraza hili, kwa kusimamia na
kwa kuziendesha kazi za Baraza kwa mafanikio makubwa. Hongera sana.
Shukrani zangu za dhati ziwaendee
Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza hili kwa kuzitekeleza kazi zao kwa moyo wa
kujituma, kwa kushirikiana na kwa uvumilivu mkubwa. Ni imani yangu kwamba wananchi wameridhika na
namna mnavyowawakilisha mawazo na maelekezo yao katika Baraza hili. Licha ya kuwa na wajumbe wapya wengi katika
Baraza hili na upya wa mfumo wa kisiasa tulionao na muundo mpya wa Serikali,
mmeweza kuifanya kazi yenu kwa ufanisi mkubwa.
Mheshimiwa
Spika,
Nachukua fursa hii, mimi mwenyewe na kwa
niaba ya Serikali kutoa mkono wa pole na rambi rambi kwako, wajumbe wa Baraza
lako, ndugu, jamaa na wananchi wa Jimbo la Magomeni na Watanzania wote kwa kifo
cha kiongozi mwenzetu Marehemu Salmin Awadh Salmin; aliyekuwa Mwakilishi wa
Jimbo la Magomeni na Mnadhimu wa CCM hapa Barazani. Hekima, busara na mchango wake katika
kuwatumikia wananchi wa Zanzibar na kuliendeleza Taifa letu, hautasahaulika na
utaendelea kuthaminiwa. Namuomba
Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi - Amin.
Mheshimiwa
Spika,
Katika hotuba yangu ya uzinduzi wa Baraza
hili la Nane tarehe 11 Novemba, 2010, nilieleza mwelekeo wa mipango ya Serikali
nitakayoiunda baada ya wananchi wa Zanzibar kunichagua kwa kura nyingi, kupitia
Chama changu cha Mapinduzi, kuwa Rais wa Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu
uliofanyika tarehe 31 Oktoba, 2010.
Kadhalika, katika hotuba yangu hiyo,
nilisema kuwa tunaianza Awamu ya Saba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
tukiwa na dhima ya msingi ya kuwatumikia wananchi waliotuchagua kwa kipindi cha
miaka mitano. Matumaini ya wananchi kwa
Serikali yao yalikuwa ni kuyaendeleza mafanikio yote yaliyoletwa na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar kwa awamu zote zilizotangulia na kutekeleza sera na
mipango itakayowezesha kukuza uchumi na kuimarisha ustawi wa jamii.
Ili kuyafikia malengo hayo, Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba inaongozwa kwa kuzingatia mipango mikuu ya
kitaifa ambayo ni Dira ya Maendeleo ya 2020, Malengo ya Milenia, MKUZA na Ilani
ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 hadi 2015.
Sambamba na hayo, utekelezaji wa ahadi nilizozitoa katika kampeni ya
uchaguzi ya mwaka 2010 ilikuwa ni miongoni mwa vipaumbele muhimu katika
utendaji wa serikali niliyoiunda.
Mheshimiwa
Spika,
Leo nitaelezea kwa muhtasari mafanikio ya
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, katika nyanja zote za
maendeleo, kisiasa, kiuchumi na ustawi wa jamii. Ni dhahiri kuwa mafanikio hayo yanatokana na
mchango wenu katika kutekeleza wajibu, kufuatana na Mipango mikuu ya kitaifa
niliyoeleza hapo mwanzo na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 – 2015. Ilani hiyo ni mkataba baina ya wananchi na
Serikali yetu. Ni jambo la kufurahisha
kwamba hadi leo hii, Ilani hiyo imeshatekelezwa kwa kiwango kinachokadiriwa
kufikia asilimia 90. Natoa pongezi kwa
wale wote walioshiriki katika utekelezaji wa Ilani hii.
Siri kubwa ya mafanikio yetu ni kuwa sisi
tuliingia katika muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa tukiwa tayari tunayo
Katiba iliyoandaliwa kwa ajili ya Muundo huo. Lakini zaidi ya hayo, tulidhamiria kwa dhati
kuitekeleza azma na shabaha ya muundo huo.
Tulijenga heshima na mapenzi baina yetu. Tulijenga misingi ya
kuvumiliana. Kwa kufanikisha uendeshaji wa serikali, nilipanga Wizara na kuteua
Mawaziri kwa uwiano wa matakwa ya Katiba ya Zanzibar.
MAFANIKIO
YA UTEKELEZAJI WA MIPANGO YA SERIKALI:
HALI YA UCHUMI:
Mheshimiwa
Spika,
Katika kipindi
hiki kuanzia mwaka 2010 – 2014, Pato la Taifa kwa bei za miaka hio limekua
kutoka TZS bilioni 1,050.8 hadi kufikia TZS bilioni 2,133.5. Kwa bei za kudumu, Pato la Taifa limekua
kutoka TZS bilioni 848.2 hadi kufikia TZS bilioni 1,115.4 sawa na ukuaji wa
asilimia 31.5 kwa kipindi hicho. Uchumi
wetu umekua kutoka asilimia 4.3 mwaka 2010 hadi kufikia asilimia 7.0 mwaka 2014
sawa na ongezeko la asilimia 2.7. Pato
la Taifa kwa mwananchi mmoja, kwa bei za miaka 2010 – 2014, limekua kutoka TZS 856,000
($613) mwaka 2010 hadi kufikia TZS 1,552,000 ($939) kwa mwaka 2014.
Katika kipindi
cha mwaka 2010/2011 hadi 2014/2015, mapato ya ndani yameongezeka kutoka TZS
bilioni 181.4 hadi kufikia TZS bilioni 360.4, sawa na ukuaji wa asilimia 98.7
kwa kipindi hicho au wastani wa asilimia 19.7 kwa kila mwaka.
Mheshimiwa Spika,
Kwa upande wa
mfumko wa bei, tunaendelea kuwa na mfumko wa bei ulio katika tarakimu
moja. Katika mwaka 2010, mfumko wa bei
ulikuwa wa wastani wa asilimia 6.1 na umeshuka kufikia wastani wa asilimia 5.6
kwa mwaka 2014.
Mheshimiwa Spika,
Kwa mwaka wa
fedha wa 2015/2016, Bajeti yetu itaendelea kuzingatia malengo makuu ya
Serikali. Malengo hayo ni kujenga jamii: (i) Iliyoelimika kwa elimu bora na
inayotoa wataalamu wenye hadhi ya kimataifa; (ii) Yenye siha, (ii) Iliyoimarika
kiuchumi; na (iv) Inayojali Umoja wa Kitaifa na kufuata misingi ya Utawala
Bora. Mambo haya ndio yanayojenga
falsafa iliyomo katika Dira ya Maendeleo ya 2020 ambayo inatekelezwa kwa sasa
kupitia MKUZA II na Mpango wake wa utekelezaji.
Utendaji wa sekta zote umejielekeza katika kufikiwa kwa malengo hayo
makuu.
Mheshimiwa Spika,
Katika kuinua uchumi wetu,
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeanzisha Idara ya Mipango, Sera na Utafiti
katika kila wizara kwa lengo la kutilia mkazo umuhimu wa utafiti katika
maendeleo yetu. Serikali, kwa
kushirikiana na Tume ya Sayansi na Teknolojia ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania (COSTECH) imeendeleza tafiti katika taasisi mbali mbali ikiwemo
Kilimo, Elimu, Uvuvi na Nyanja nyenginezo.
MATOKEO KWA USTAWI: (RESULTS FOR PROSPERITY - R4P)
Mheshimiwa Spika,
Katika kutafuta mbinu bora za
kutekeleza mipango yetu, Serikali imeanzisha utaratibu wa kuwakutanisha wataalamu
wa sekta mbali mbali kwa mfumo uliopewa jina la Mpango wa Maabara kwa ajili ya
kujadili, kupanga na kupitisha maazimio ya utelekezaji wa mipango mbali mbali
ya maendeleo. Utaratibu huu, hapa petu, tumeufuata na tumeupa jina la Matokeo
kwa Ustawi (Results for Prosperity - R4P) ambao umeonesha kuwa na mafanikio
makubwa kwa nchi zilizouanzisha na kuufuata. Hivi karibuni Serikali imeanza
kutekeleza programu mbali mbali zinazotayarishwa katika Mpango wa Matokeo kwa
Ustawi. Programu zilizoanza kutekelezwa ni
pamoja na Programu Mjumuisho ya Kuendeleza Utalii, Programu ya Kuimarisha
Mazingira ya Biashara na Mkakati wa Utafutaji Rasilimali Fedha. Kwa sasa
mchakato unaendelea wa matayarisho kwa ajili ya sekta afya na elimu ambazo tunatarajia
zitaanza katika mwaka huu.
MIRADI
YA MASHIRIKIANO BAINA SEKTA YA UMMA NA SEKTA BINAFSI:
Mheshimiwa
Spika,
Katika kipindi cha miaka mitano, tumefanya
jitihada kubwa za kuiimarisha na kuishirikisha Sekta binafsi katika mipango yetu
ya maendeleo. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tayari imeanzisha kitengo cha “PPP”
katika Tume ya Mipango kwa ajili ya kushughulikia miradi itakayoanzishwa kwa
mfumo huo. Serikali imejiandaa kuanzisha
Idara kamili ya “PPP” ambayo itahusika na utekelezaji na usimamizi wa shughuli
zote za miradi ya mashirikiano baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi.
UWEKEZAJI VITEGA UCHUMI:
Mheshimiwa
Spika,
Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar, Awamu ya Saba, kupitia Mamlaka ya Vitega Uchumi (ZIPA) ilifanya kazi
nzuri katika kuwavutia wawekezaji wa nje na ndani kuja kuwekeza katika sekta
mbali mbali za kiuchumi na kijamii. Kwa
Kipindi cha miaka mitano (2010 – 2015), tumeweza kusajili miradi 187 yenye
thamani ya TZS milioni 38,560.50, sawa na USD 1,881,00 milioni ambayo inakadiriwa
kuwapatia ajira watu 9,192. Wawekezaji
kutoka Uturuki, China, Italia, Ujerumani na India wameonesha dhamira ya dhati ya
kutuunga mkono na nimetumia fursa niliyoipata kuwakaribisha waje kuwekeza,
wakati nilipotembelea nchi zao, vile vile wawekezaji wa ndani nao wamehamasika
katika uwekezaji kwenye nyanja mbali mbali.
Mheshimiwa
Spika,
Serikali kupitia Mamlaka ya
Uwekezaji na Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA), kuanzia mwaka wa fedha 2014/2015,
imeweka mkazo mkubwa katika kukamilisha dhamira ya kuendeleza maeneo huru ya
uchumi. Ni dhahiri kwamba mpango huu tangu
ulipobuniwa na hatimae kutolewa tangazo la Sheria Namba 5 la mwaka 1993 bado
hazijachukuliwa juhudi za kutosha za kutekeleza kwa vitendo uendelezaji wa
maeneo hayo.
Kwa hakika hivi sasa
tumejidhatiti kuitekeleza dhana ya maeneo huru ya uchumi kwa vitendo. Mipango yetu ni kuibadilisha taswira ya eneo
la Fumba. Tumepanga kuutekeleza Mradi wa
Ujenzi wa Mji wa Kisasa wa Fumba (Fumba Bay Satellite City Project). Mji huu mpya wa kisasa na wa kibiashara
utakuwa na mtaa mkubwa wa biashara (High Street), nyumba za kisasa za
kibiashara za kuishi wageni na wenyeji na uwanja wa kuchezea mchezo wa gofu. Vile vile, kutakuwa na hoteli moja kubwa ya
nyota tano yenye vyumba 400 na tutajenga eneo la shughuli za biashara ambalo
litakuwa na maghala ya kisasa na mfumo wa usafirishaji wa bidhaa wa kisasa.
Aidha, katika mji huu
kutakuwa na uwanja wa mpira wa kisasa ambao utakuwa na uwezo wa kuchukua kiasi
cha watu 45,000. Pamoja na huduma za
kijamii za ulinzi, afya na elimu, mradi huo unakusudia kuanzisha bandari ndogo
kwa ajili ya huduma za usafiri wa majini kati ya Zanzibar - Pemba na Zanzibar -
Dar es Salaam. Jumla ya hekta 700
zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huu. Serikali imeanza mazungumzo na Muwekezaji wa
Kampuni mama ya Bakhresa Group juu ya kushirikiana katika uwekezaji wa mradi
huu kwa mfumo wa ubia (joint venture company).
Mheshimiwa
Spika,
Vile vile, katika eneo hili tutatekeleza Mradi wa Mtaa wa
Viwanda. Jumla ya hekta
100 zimetengwa katika maeneo ya Dimani, Kusini pamoja na Ndambani kwa ajili ya
uendelezaji wa shughuli za viwanda vidogo na vya kati. Mazungumzo yanaendelea kati ya Mamlaka ya
Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA) na Kampuni ya CPC ya Misri juu ya mfumo na
utaratibu na ushirikiano wa uwekezaji wa Miundombinu katika eneo hilo.
Kadhalika, Hekta 60 zimetengwa kwa ajili ya
Kituo cha Kimataifa cha Mikutano na kukabidhiwa Wizara ya Biashara, Viwanda na
Masoko kwa ajili ya kuandaa maelezo maalum ya mradi wa uwekezaji. Maelezo hayo
yakiwa tayari, Mamlaka itashirikiana na Wizara hiyo kuhamasisha ushiriki wa
sekta binafsi katika uwekezaji utakaopangwa.
Mheshimiwa
Spika,
Vile vile, Serikali imebuni mpango wa
kutekeleza Mradi
wa Uendelezaji wa Mji wa Nyamanzi – Fumba. Mradi huu umetengewa
kiasi cha hekta 63 ambazo zitatumika kwa ajili ya nyumba za makaazi na biashara
mbali mbali ikiwemo maeneo ya makaazi ya kijamii, majengo ya kuishi, huduma za
hoteli na kumbi za mikutano, huduma za masoko na mawasiliano, maofisi na maduka
pamoja na maegesho ya magari, vituo vya ferry, maeneo ya burudani afya
na michezo. Maeneo ya asili ya vijiji vya eneo hilo vikiwemo Fumba, Bweleo,
Dimani na vijiji vyengine vidogo vidogo yataheshimiwa na kuendelezwa kwa
mashauriano na wanavijiji wenyewe.
Mheshimiwa Spika,
Katika Mkoa wa Kaskazini Unguja, tumeshaanza Mradi wa Maendeleo ya Mji
wa Kisasa Kijini – Matemwe. Mradi
huu unaendelea kutekelezwa na Kampuni ya “Penny Royal” katika maeneo ya Matemwe
Muyuni, ambapo utagharimu jumla ya Dola za Kimarekani milioni 220. Mradi huo
unajumuisha ujenzi wa Hoteli ya kimataifa yenye hadhi ya nyota tano. Aidha,
mradi huo utahusisha ujenzi wa kiwanja cha kimataifa cha gofu, chenye jumla ya
vishimo 18 na ujenzi wa nyumba za makaazi kwa watu wenye kipato cha juu ambazo
zitatumia nishati ya nguvu ya upepo. Hivi sasa Kampuni hiyo inaisaidia Serikali
katika ujenzi wa barabara yenye urefu wa km 20.2 kutoka Matemwe kupitia Kijini
kuelekea maeneo ya mradi hadi Kidoti. Ujenzi wa barabara hio unaendelea vizuri.
Mheshimiwa Spika,
Katika eneo la Mjini Unguja, katika kipindi hiki, Serikali imepanga
kutekeleza Mradi wa Kuendeleza Hoteli ya Bwawani na eneo linaloambatana nalo. Serikali italiendeleza eneo hilo
kupitia Muwekezaji wa Kampuni ya “Quality Group” alieshinda zabuni. Kampuni
hii inakusudia kuendeleza eneo la Bwawani kwa kujenga Hoteli ya Kisasa ya nyota
tano, majengo ya kisasa ya makaazi, majengo ya biashara, mikahawa, soko la
Kizanzibari na maegesho ya magari. Jengo la sasa la hoteli ya Bwawani
litakarabatiwa kwa ajili ya kupokea wageni mashuhuri. Uendelezaji wa eneo la Bwawani utazingatia
ipasavyo athari za Kimazingira na urithi wa kale.
SEKTA YA BIASHARA NA
VIWANDA:
Mheshimiwa Spika,
Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Awamu ya Saba, yenye Muundo wa Umoja wa Kitaifa
inaendelea kuimarisha mazingira ya biashara kwa kushirikiana na sekta binafsi.
Usafirishaji wa bidhaa unaendelea kuimarika mwaka hadi mwaka. Katika mwaka 2014 tumeweza kuuza nje bidhaa
zenye thamani ya TZS milioni 133,591.7 kutoka bidhaa zenye thamani ya TZS
milioni 87,799.6 mwaka 2013, sawa na ongezeko la asilimia 52.14. Usafirishaji
huo umeongezeka kwa kiasi kikubwa kutokana na jitihada zetu za kuimarisha
uzalishaji wa zao la karafuu na mwani ambayo usafirishaji wake ulifikia TZS
milioni 103,079.2 kutoka TZS milioni 75,392.6 mwaka 2013. Hili ni ongezeko la
asilimia 77.8 ya usafirishaji wote kwa mwaka 2014. Licha ya kuwepo kwa urari kwa bidhaa kwa
usafirishaji nje, takwimu hizi zinatupa matumaini mazuri juu ya mwenendo na
ukuaji wa biashara nchini.
Kuhusu
biashara baina Zanzibar na Tanzania Bara, jumla ya bidhaa zenye thamani ya TZS
milioni 23,268.7 ziliingizwa Zanzibar kutoka Tanzania Bara mwaka 2010
ikilinganisha na bidhaa zenye thamani ya TZS milioni 64,296.4 mwaka 2014. Vile vile, bidhaa zenye thamani ya TZS
milioni 2,203.8 zilisafirishwa kwenda Tanzania Bara mwaka 2010 ikilinganishwa na
bidhaa zenye thamani ya TZS 366,354.2 mwaka 2014. Kwa jumla, katika kipindi hiki cha kwanza cha
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, urari wa biashara kati ya
Zanzibar na Tanzania Bara unaendelea kuwa mzuri kwa upande wa Zanzibar.
Mheshimiwa
Spika,
Ni dhahiri kuwa juhudi zilizochukuliwa na
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Awamu ya Saba, za kufufua zao la Karafuu
zimezaa matunda mazuri. Mpango wa miaka kumi wa kufufua zao hili, tumekuwa
tukiutekeleza kwa mafanikio. Katika
kipindi cha miaka mitatu ya kwanza ya mpango huo; 2011/12 - 2013/2014, jumla ya
tani 11,477 za karafuu zenye thamani ya Dola za Marekani milioni 130.82
zilisafirishwa na kuuzwa nje ya nchi. Kiwango hicho ni sawa na ongezeko la tani
2,792 ambalo ni sawa na asilimia 32.1 ikilinganishwa na mwaka 2008/09 -
2010/2011. Hadi kufikia tarehe 12 Juni, 2015 jumla ya tani 2, 822 zenye thamani
ya TZS bilioni 39.48 zilinunuliwa kutoka
kwa wakulima.
Mheshimiwa
Spika,
Serikali imetimiza ahadi niliyoitoa mwaka
2011 ya kuwalipa wakulima wa zao la Karafuu asilimia 80 ya bei ya karafuu ya
Soko la Dunia. Karafuu za Daraja la Kwanza
zinanunuliwa kwa bei ya TZS 14,000 kwa kilo badala ya TZS 5,000 kwa kilo, bei
iliyokuwepo mwaka 2010. Ongezeko hili ni
sawa na asilimia 180. Kadhalika, vituo
vipya vya ununuzi na uuzaji wa karafuu vimejengwa Unguja na Pemba, vituo vya
zamani vimekarabatiwa na huduma zote muhimu zinapatikana kwenye vituo hivyo. Tumefanikiwa
sana katika kupambana na Magendo ya Karafuu na wananchi wanauza Karafuu zao
katika Vituo vya ZSTC. Tunawashukuru Wananchi na Vikosi vyetu vya Ulinzi na
Usalama kwa kazi nzuri, walioifanya ya kushirikiana na Serikali katika
kupambana na Magendo ya Karafuu.
Mheshimiwa
Spika,
Maamuzi ya Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar, Awamu ya Saba, ya kulifanyia mageuzi Shirika la ZSTC yamekuwa na
manufaa makubwa kwetu. Ni habari njema kwetu sisi viongozi na wananchi kutambua
kwamba Shirika limegeuka kutoka kuendeshwa kwa hasara kuwa Shirika lenye
kuendesha shughuli zake kwa faida. Hivi
sasa Shirika linalipa kodi ya mapato na kulipa faida nyengine Serikalini. Imebainishwa kuwa kwa hesabu zilizokaguliwa
katika mwaka wa 2011/2012, 2012/2013 pamoja na makadirio kwa hesabu za
2013/2014 Shirika limelipa jumla ya TZS 1.8 bilioni kama kodi ya mapato na
kulipa gawio la TZS milioni 500 kwa mwaka 2013/2014. Nachukua nafasi hii kutoa
pongezi kwa Uongozi na Wafanyakazi wa ZSTC kwa mafanikio haya.
Mafanikio yaliyopatikana katika kuliimarisha
zao la karafuu, kupambana na magendo na kulifanyia mabadiliko Shirika la ZSTC,
yametokana na Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu ya 2010/2015 ya kutolibinafsisha
zao la karafuu, lakini uandaliwe mpango madhubuti wa maendeleo ya karafuu.
Mheshimiwa Spika,
Kwa kutambua umuhimu wa viwanda katika
kukuza uchumi na kuimarisha Soko la Ajira, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,
Awamu ya Saba, ilipanga na kutekeleza mipango mbali mbali yenye lengo la kukuza
sekta ya viwanda. Ongezeko la bidhaa zinazozalishwa viwandani katika kipindi
hiki cha miaka mitano linatupa matumaini na ari ya kuendeleza kwa kasi zaidi.
Thamani ya bidhaa zilizozalishwa viwandani
imeongezeka kutoka TZS bilioni 128 mwaka 2013 hadi kufikia TZS 136 bilioni
mwaka 2014. Hili ni sawa na ongezeko la asilimia 5.5. Wawekezaji wamekuwa
wakiwekeza katika viwanda vya usafishaji nafaka, usindakaji maziwa, uzalishaji
sukari, maji ya kunywa na vinywaji mbali mbali.
Aidha, pamekuwa na ongezeko la ukuaji wa viwanda vidogo vidogo
vinavyozalishwa na wajasiriamali wanaozalisha sabuni, vifaa vya ujenzi, samani
na bidhaa za viungo Unguja na Pemba.
Ukuaji huo vile vile umepelekea kuwepo kwa
ongezeko la mchango wa sekta hii kwa Pato la Taifa ambapo katika mwaka 2014 ulifikia
asilimia 9.9 kutoka asilimia 6.9 mwaka 2013. Taasisi ya Viwango tuliyoianzisha
baada ya kupitisha Sheria ya Viwango Namba 1 ya mwaka 2011 imeanza kazi zake
katika kuimarisha bidhaa zinazozalishwa na kuingizwa nchini.
Tunaendelea kushirikiana na sekta binafsi
katika kuimarisha sekta ya Viwanda na Biashara ikiwa ni pamoja na kuyafanyia
kazi mapendekezo yanayotolewa na Baraza la Biashara la Zanzibar (ZNBC) katika
mikutano ya kila mwaka tunayoendelea kuifanya. Natoa shukurani kwa wajumbe wa
ZNBC na wale wote wanaoshiriki katika mikutano ya mwaka ya Baraza hili kwa
michango na mashirikiano wanayotoa kwa lengo la kukuza sekta zetu muhimu za
uchumi hasa Biashara, Viwanda na Utalii. Aidha, natumai kwamba juhudi zetu za
kuanzisha Tamasha la Biashara zitakuwa na mchango mkubwa katika kutangaza na
kukuza biashara, viwanda na shughuli mbali mbali za ujasiriamali zinazoendeshwa
nchini.
UTALII:
Mheshimiwa Spika,
Katika kipindi cha miaka mitano, tumefanikiwa
sana kuiendeleza sekta ya utalii.
Tumeitekeleza kwa mafanikio dhana ya utalii kwa wote niliyoitangaza
rasmi tarehe 16 Oktoba, 2011. Serikali
imeifanyia marekebisho Sheria ya utalii ya mwaka 2009, na kupelekea kuundwa kwa
Sheria mpya Namba 7 ya mwaka 2012 ambayo inakidhi haja na kwenda sambamba na
dhana ya utalii kwa wote na kutoa miongozo imara ya kuiendesha sekta hiyo.
Takwimu
zinaonesha kuwa Idadi ya watalii 132,836 walitembelea Zanzibar katika mwaka
2010; ambapo katika mwaka 2014 watalii wapatao 311,801 waliwasili Zanzibar.
Hili ni ongezeko la asilimia 134 katika kipindi cha miaka minne. Katika kuhakikisha usalama wa wananchi na
wageni wanaotutembelea, Serikali imeandaa Mradi wa usalama katika maeneo ya Mji
wa Unguja. Jumla ya fedha kwa mradi wote
kwa kipindi cha miaka mitano ni Dola za Marekani Milioni 28.9. Fedha zilizotengwa kwa matumizi ya mwaka wa
kwanza ni TZS bilioni 10. Mradi huu utatupatia
vifaa vya CCTV, magari ya zimamoto, boti za doria na mashine ya kukagulia vifaa
vya hatari vilivyofichwa katika magari.
Vifaa hivyo tayari vimeshaagiziwa na Kampuni ya RAVITALCO ya Romania na
ROM SOLUTION iliyosajiliwa Zanzibar.
Vile vile, kwa kushirikiana na Kampuni ya Mawasiliano ya ZTE ya China
tayari tumeshafunga kamera maalum za usalama (CCTV) katika maeneo ya Mji wa
Unguja. Kadhalika, kwa lengo la kuimarisha ulinzi kwa
watalii, Serikali imeanzisha Kampuni ya Ulinzi ya JKU, ambayo itatoa huduma kwa
sekta binafsi kwenye mahoteli.
Mheshimiwa Spika,
Katika kipindi
hiki cha miaka mitano, tumeshuhudia ongezeko la wawekezaji katika ujenzi wa
hoteli za kisasa zenye hadhi ya juu. Aidha, tumeshuhudia ongezeko la vivutio
vya utalii ikiwa ni pamoja na ujenzi wa viwanja vya mchezo wa gofu ambao unapendwa na watalii. Kumekuwa na ongezeko la idadi ya wageni
wanaotoka Mashariki ya Kati na Mashariki ya mbali baada ya kuongeza juhudi za
kuitangaza Zanzibar katika maeneo hayo mapya. Chuo cha Maendeleo ya Utalii nacho
kimeimarishwa ili kiendelee kutoa rasilimali watu wenye ujuzi, taaluma na stadi
zinazohitajika na wawekezaji wanaokuja nchini.
MAKUMBUSHO NA MAMBO YA
KALE:
Mheshimiwa
Spika,
Katika kipindi cha miaka mitano, tumefanya jitihada
za pamoja katika kufanya matengenezo ya makumbusho na kuyatunza mapango mbali
mbali. Serikali iko katika hatua za mwisho za kukamilisha Sera ya Urithi wa
Utamaduni itakayotoa muongozo wa matumizi bora ya maeneo ya urithi ili kuimarisha shughuli za utalii.
Miongoni mwa maeneo ya historia, mambo ya kale na urithi wa utamaduni
tuliyoweza kuyaimarisha ni Mangapwani, Kuumbi Jambiani na Kwa Bi. Khole kwa
upande wa Unguja na Chwaka - Tumbe kwa upande wa Pemba. Natoa wito kwa wananchi waendeleze utamaduni
wa kuyatembelea maeneo yetu hayo ili kuimarisha utalii wa ndani.
SEKTA YA KILIMO:
Mheshimiwa
Spika,
Kwa kutambua kuwa, kilimo ndio chanzo kikuu
cha ajira za wananchi kwa asilimia 70 ya ajira na kinatoa asilimia 27.3 katika
Pato la Taifa, niliahidi Serikali itafanya juhudi ya kuiendeleza sekta hii kwa
kauli mbiu ya Mapinduzi ya Kilimo.
Serikali imefanya jitihada mbali mbali ili kuongeza uzalishaji wa mazao
hasa mpunga ili kuwa na uhakika wa chakula na lishe. Serikali imenunua pembejeo mbali mbali za
kilimo, imeajiri wataalamu wa ugani na imetekeleza programu niliyoianzisha
mwaka 2011 ya kuwapa ruzuku wakulima ya asilimia 75 ya gharama za bei ya
mbolea, mbegu, dawa ya magugu na huduma za matrekta.
Jitihada hizo za Serikali ziliweza kuzaa
matunda kwa kuongezeka kiwango cha uzalishaji.
Mavuno ya zao la mpunga kwa jumla yameongezeka kutoka tani 21,014 mwaka
2010 hadi tani 33,655 mwaka 2013. Hili
ni sawa na ongezeko la asilimia 60.
Katika kipindi hiki Zanzibar imepata mafanikio makubwa ya uzalishaji wa
mazao muhimu ya chakula hadi kufikia tani 674,334.
Mheshimiwa
Spika,
Katika kipindi cha miaka mitano, Serikali
imefanya jitihada za kuimarisha kilimo cha umwagiliaji maji ili kupunguza
tatizo linalotukumba katika kilimo cha kutegemea mvua zisizo za uhakika. Ujenzi
wa miundombinu ya umwagiliaji maji wa hekta 2,200 katika mabonde ya Cheju,
Kibokwa, Kilombero, Mlemele na Makwararani umeanza kushughulikiwa kwa hatua
mbali mbali.
Kadhalika, kwa kutambua umuhimu wa utafiti
katika kuleta maendeleo ya kilimo, Serikali imefanya jitihada za kukiimarisha
kituo cha utafiti wa kilimo Kizimbani kwa kukipandisha hadhi kuwa Taasisi ya
Utafiti ya Kizimbani. Taasisi hii
imeshirikiana vyema na Tume ya Sayansi na Teknolojia ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania (COSTECH) katika shughuli za utafiti.
Jumla ya mbegu 43 zimefanyiwa utafiti kwa kushirikiana na Taasisi ya
Utafiti wa zao la Mpunga wa Kimataifa (IRRI).
Kadhalika, Taasisi hii imefanya tafiti juu ya mbegu za mazao ya mizizi
na kutoa mbegu zinazostahamili maradhi na kunawiri katika mazingira yetu.
Katika kuhakikisha upatikanaji wa mbegu bora
za mazao mbali mbali, Serikali imekuwa ikiendeleza majaribio ya mbegu ya mpunga
ya NERICA katika vituo vya Mwera na Kizimbani.
Hivi sasa wakulima tayari wameshapatiwa mbegu hii kwa ajili ya
uzalishaji na kuiendeleza. Tafiti mbali
mbali zimeonesha kuwa hii ni mbegu bora kwa mazingira yetu kwa kuwa
inastahamili ukame na inastawi hata katika ardhi isiyo ya mabondeni.
Mheshimiwa
Spika,
Serikali imefanya juhudi kubwa katika
kuhifadhi misitu na miti yetu ya asili.
Zanzibar imejaaliwa kuwa na miti ya aina mbali mbali ya asili ambayo
idadi yake imeanza kupotea na hatukuwa na utaratibu bora wa kuitunza. Katika
kukabiliana na hali hiyo, Serikali ilifanya jitihada za kuendesha sensa ya miti
mwaka 2013 ili kujua idadi ya miti iliyopo.
Pamoja na jitihada hizo, Serikali imeongeza
juhudi za uhifadhi wa misitu yetu ya asili ikiwa ni pamoja na msitu wa Jozani, Ufufuma, Kiwengwa na Makangale
pamoja na kusimamia Mradi wa Hifadhi ya Misitu ya Asili (HIMA) katika maeneo
mbali mbali, Unguja na Pemba. Kwa lengo
la kuongeza idadi ya miti tuliyonayo, katika kipindi hiki jumla ya miti milioni
5 ya misitu ilioteshwa katika vitalu vya Serikali na miche milioni 8 katika
vitalu vya watu binafsi.
Jitihada maalum zimefanywa katika kuimarisha
kilimo cha karafuu, ambalo ni zao letu kuu la uchumi. Serikali imewahamasisha wakulima wa zao hilo
kuyaendeleza mashamba yao na kuwapatia miche bila ya malipo. Hatua hiyo ni miongoni mwa utekelezaji wa mpango
wa miaka kumi wa kulifufua zao la karafuu.
Katika kipindi cha 2010-2014
jumla ya miche ya mikarafuu milioni 3.7 iligawiwa kwa wakulima katika lengo
lilokusudiwa la kutoa miche milioni 3.8.
MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimwa
Spika,
Katika sekta ya mifugo, Serikali iliweka
malengo ya kuleta mapinduzi ya ufugaji ili kuongeza tija na ubora wa mazao
yanayotokana na shughuli hiyo. Dhamira
ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuwa na ufugaji wa kisasa wa ng’ombe wa
maziwa, mbuzi na kuku kwa lengo la kuongeza tija na kipato cha wafugaji
wetu. Soko la maziwa sasa limekua
kutokana na muwekezaji Mzalendo (kufungua kiwanda cha maziwa) Fumba.
Serikali vile vile, imeimarisha maabara ya
mifugo Maruhubi kwa kuifanyia matengenezo makubwa, kuweka vifaa vya kisasa vya
kuhifadhia mbegu bora za ng’ombe na kuendeleza mradi wa upandishaji ng’ombe kwa
shindano ili kupata ng’ombe bora.
Kadhalika, Serikali iliendesha mradi wa kudhibiti maradhi ya mifugo
yasiyo na mipaka ambapo ng’ombe 20,000 walichanjwa kwa kuwakinga na maradhi ya
chambavu na kimeta na kuku 80,000 walichanjwa ili kuwakinga na mahepe.
Mheshimiwa
Spika,
Nilianzisha Mapinduzi ya uvuvi kama
nilivyotamka katika Hotuba yangu ya tarehe 11 Novemba, 2010, katika Baraza hili.
Mwaka 2010 tuliahidi kufanya jitihada za kuziimarisha shughuli za uvuvi kwa
kutambua umuhimu wake katika kutoa ajira, kutupatia lishe bora na kuongeza
mchango wake katika Pato la Taifa. Nina
furaha kuwa Serikali imepata mafanikio katika utekelezaji wa azma hiyo ambapo mchango
wa sekta hiyo katika Pato la Taifa umefikia asilimia 7.2. Jumla ya tani 148,535 za samaki zenye thamani
ya TZS bilioni 527.5 zimevuliwa hadi mwaka 2014.
Ni jambo la kutia moyo, kuona kuwa jitihada
za Serikali za kushirikiana na wananchi katika kukabiliana na vitendo vya uvuvi
haramu na kuimarisha hifadhi ya mazingira ya bahari zimesaidia sana kuongeza
kiwango cha samaki wanaovuliwa. Jumla ya
wavuvi wapatao 2,520 wamepatiwa mafunzo ya uvuvi bora yakiwemo ufugaji wa
samaki na viumbe wengine wa baharini.
Serikali imeandaa mpango wa ujenzi wa kituo
cha kutotolea vifaranga vya samaki katika eneo la Beit - el-Ras na imetoa mafunzo kwa wafugaji wa samaki 69
kuhusu utengenezaji wa chakula, ulishaji, uchimbaji wa mabwawa na utunzaji bora
wa samaki.
Mheshimiwa
Spika,
Wakati huo huo, zao la mwani ni miongoni mwa
mazao ya baharini na kutupatia fedha za kigeni.
Jumla ya tani 51,687 za mwani mkavu zenye thamani ya TZS bilioni 187
zimesafirishwa nje ya nchi katika kipindi hiki.
Serikali imewapatia vihori wakulima wa mwani
wa Unguja na Pemba kwa ajili ya kubebea mwani. Tunafanya juhudi kuwapa nguvu
wakulima wa mwani ili kuhakikisha zao hili linasarifiwa hapa nchini kwa lengo
la kukuza uchumi wetu na kuongeza kipato cha wakulima wetu. Aidha, kufuatia safari yangu ya China na
Vietnam niliwashajihisha wawekezaji kushiriki katika sekta hiyo. Matumaini yetu ya utekelezaji ni mazuri.
Kwa lengo la kuongeza mapato yanayotokana na
uvuvi, Serikali imejiwekea lengo la kuanzisha programu ya uvuvi wa bahari
kuu. Programu hii inakusudiwa
kuwawezesha wavuvi wetu kuvua katika kina kirefu cha maji ili kuongeza kiwango
cha samaki wanaovuliwa na kuongeza fursa za ajira, biashara na kuchangia katika
ukuaji wa uchumi. Programu hiyo
itaendeshwa kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Japan (JICA). Maandalizi ya programu hiyo yamekwishaanza.
Mheshimiwa
Spika,
Serikali imeandaa mpango wa kuendeleza uvuvi
wa bahari kuu kwa lengo la kuwawezesha wavuvi na vifaa kuongeza kipato chao. Serikali imefikia makubaliano na Serikali ya
Japan kupitia Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) kuimarisha diko na soko la
samaki la Malindi ili liwe la kisasa na lenye uwezo wa kuhudumia vyombo vya
uvuvi ikiwemo vinavyovua bahari kuu.
Utekelezaji wa mradi huo utakaogharimu Dola za Marekani 244,500 na
utaanza mwaka huu. Utakapomalizika utawanufaisha wananchi wengi.
Kadhalika, Serikali imewakaribisha
wawekezaji kwa makubaliano ya kuwashirikisha wavuvi wazalendo. Katika mwaka 2015, Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar, imefikia makubaliano ya awali na Mwekezaji (Hairu Fisheries Management
Company) kutoka Sri Lanka ya kuleta vyombo 20 vya urefu wa mita 18 ambavyo vina
uwezo wa kuvua katika kina kirefu na kukaa baharini kwa muda mrefu. Aidha, Mwekezaji huyo atajenga Kiwanda cha
Boti za Uvuvi za mita 6 na mita 9 ambazo watauziwa wavuvi wetu.
Hatua hizo zitaimarisha juhudi za Serikali
za kuwawezesha wananchi kuitumia raslimali ya bahari kuu kujiongezea kipato
chao.
MAZINGIRA:
Mheshimiwa
Spika,
Serikali inatambua umuhimu wa hifadhi ya
mazingira katika utekelezaji wa mipango yetu yote ya maendeleo na imechukua
jitihada za kukabiliana na uharibifu wake unaosababishwa na wanadamu na ule
unaotokana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.
Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na
Serikali ni kuandaa Sera mpya ya Mazingira ya mwaka 2013 yenye kutoa muongozo
kwa shughuli za uhifadhi wa mazingira nchini na kutayarisha Sheria mpya ya
usimamizi wa mazingira ya mwaka 2015.
Serikali imezingatia haja ya kufanya
tathmini ya athari za mazingira katika miradi ya uwekezaji ambapo jumla ya
tathmini 71 za athari za mazingira zimefanywa na wahusika kupewa vyeti. Kadhalika, miradi 221 imefanyiwa ufuatiliaji
wa kimazingira na kutolewa ushauri. Vile
vile, Serikali imechukua hatua za kukabiliana na athari za tabia nchi.
Mheshimiwa
Spika,
Mnamo mwezi Septemba, mwaka 2014
nilihudhuria mkutano wa nchi ndogo za visiwa zinazoendelea nchini Samoa,
kumuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dk. Jakaya Mrisho
Kikwete. Tanzania ilipata heshima ya
kuchaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa mkutano na nikapewa heshima ya kuhutubia
kikao cha ufunguzi uliofanywa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mhe. Ban ki
Moon.
Tukio moja wapo muhimu wakati wa mkutano huo
ni uzinduzi wa Mpango wa Magharibi ya Bahari ya Hindi wa changamoto za Ukanda
wa Pwani na Mabadiliko ya Tabianchi (Western Indian Ocean Coastal Challenge
(WIOCC). Visiwa vinavyoshiriki mpango
huo ni pamoja na Sychelles, Comoro, Mauritius, Reunion na Zanzibar. Uzinduzi huo ulihudhuriwa na viongozi mbali
mbali wa nchi za visiwa pamoja na Washirika wa Maendeleo wakiwemo Island
Partnership (GLISPA).
VYAMA
VYA USHIRIKA NA SACCOS:
Mheshimiwa
Spika,
Wananchi wamefaidika na taasisi hizo kwa
kujipatia ajira na mikopo ya kujiendeleza.
Ili kukuza taaluma ya vyama vya ushirika na SACCOS zilizopo, Serikali
imeandaa mpango mkuu wa mafunzo wa miaka mitatu (Training Master Plan), pamoja
na kuandaa miongozo ya aina 13 ya kufundishia kwa mujibu wa mahitaji ya mafunzo
yaliyoibuliwa.
KAZI, AJIRA NA UTUMISHI WA
UMMA:
Mheshimiwa
Spika,
Katika kukabiliana na tatizo la ukosefu wa
ajira kwa vijana na wanawake na kuwajengea uezo wa kipato wananchi, katika
kipindi hiki cha miaka mitano Serikali imeanzisha Mfuko wa Uwezeshaji hapo
tarehe 21 Disemba, 2013 ukiwa na jumla ya fedha TZS bilioni 2.413, baada ya
kuunganishwa Mfuko wa Kujitegemea, Mfuko wa JK na AK na Mfuko wa Vijana. Kati ya fedha hizo, TZS milioni 973
zilipatikana kwa kuchangishwa kupitia Kamati niliyoiunda, TZS bilioni 1.2
zilitokana na mfuko wa AK/JK na jumla ya TZS milioni 140 ni za Mfuko wa Rais wa
Kujitegemea na TZS milioni 100 zilitokana na Mfuko wa Vijana. Lengo kuu kuunda Mfuko wa Kujitegemea ni kuwa
na Mfuko ulio imara zaidi katika kuwasaidia vijana, wanawake na vikundi mbali
mbali vya wajasiriamali katika shughuli zao za kujiendeleza kiuchumi.
Katika kuhakikisha kuwa vijana wanapata
fursa za ajira, tumefanikiwa kuzindua Mpango Mkakati wa Ajira kwa vijana wa
mwaka 2014/2018. Mpango huu umeweka
vipaumbele katika sekta za ujasiriamali, elimu ya amali pamoja na ufundi stadi. Tumepata mafanikio katika kutekeleza Programu
ya Ajira kwa vijana katika sekta ya kilimo kupitia mashamba darasa, shughuli za
uvuvi, ufugaji na utalii. Nachukua fursa hii
kuwapongeza vijana na wanawake kwa ari na moyo walioonesha katika kuunga mkono
jitihada hizi na kwa kutumia vizuri fursa tulizowaandalia.
Mheshimiwa
Spika,
Katika kipindi hiki cha miaka mitano
tumefanikisha kupatikana kwa nafasi za ajira 25,019 Serikalini na katika Sekta
Binafsi. Kati ya hizo, nafasi za ajira 4,850 zilikuwa za taasisi mbali mbali za
Serikali na nafasi za ajira 20,169 zilitokana na sekta binafsi, zikijumuisha
ajira za nje ya nchi na taasisi zinazojitegemea kwa wananchi wa Zanzibar wenye
sifa zilizohitajika. Ajira bado ni
changamoto nchini kwetu na katika nchi za nje hata zile zilizoendelea. Kwa kiasi kikubwa tumefanikiwa kupambana na
tatizo hilo na mipango yetu chini ya mkakati wa ajira unatoa matumaini mazuri.
Mheshimiwa
Spika,
Wakati huo huo, Serikali imefanikiwa
kupandisha mishahara ya watumishi wa umma kutoka kima cha chini cha mshahara wa
Tsh.100,000 hadi TZS 125,000 kwa mwezi
sawa na asilimia ishirini na tano (25%) pamoja na kufanya marekebisho ya
mishahara ya wataalamu na wafanyakazi mbali mbali wakiwemo Madaktari, Walimu wa
Sayansi na kadhalika. Serikali ilifanya
marekebisho hayo ya mwanzo katika mwaka 2011.
Vile vile, mwishoni mwa mwaka 2013 na
mwanzoni mwa mwaka 2014, Serikali ilipandisha kima cha chini cha mshahara
kutoka TZS 125,000 hadi TZS 150,000 sawa na asilimia ishirini (20%) pamoja na
kurekebisha mishahara ya watumishi wazoefu, waliotumikia katika utumishi wa
umma kwa miaka kumi na tano (15) na zaidi ambao wana mishahara kati ya TZS 150,000
hadi TZS 225,000 katika jitihada za kunyanyua kipato cha mfanyakazi, Serikali
imeidhinisha posho mbali mbali ambazo tayari zimeanza kutolewa. Malimbikizo ya
mishahara ya walimu yatalipwa kutoka bajeti ya mwaka wa fedha wa 2015/2016
iliyopitishwa na Baraza hili.
MIUNDO YA UTUMISHI:
Mheshimiwa
Spika,
Katika kuimarisha utendaji kazi, Serikali imerudisha
tena utaratibu wa kuwa na Miundo ya Utumishi katika Mawizara na Taasisi mbali
mbali za Serikali. Wizara zote tayari zimeshatengeneza Miundo yao ya Utumishi
na zimewasilishwa katika Kamisheni ya Utumishi wa Umma kwa kuthibitishwa.
Taasisi nyengine za Serikali yakiwemo mashirika na taasisi zinazojitegemea zimo
katika hatua za utayarishaji wa Miundo yao ya Utumishi kwa kushirikiana na
Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi na Utumishi wa Umma. Serikali imetoa
miongozo mbali mbali kwa ajili ya kurekebisha mapungufu yaliyojitokeza katika
marekebisho ya mishahara na maposho ili kuhakikisha kwamba hakuna mfanyakazi
atakayedhulumiwa haki yake.
Mheshimiwa
Spika,
Vile vile, katika kipindi cha miaka mitano, Serikali
imeimarisha maslahi ya wananchi wanaofanyakazi katika sekta Binafsi kwa kuitaka
iongeze mishahara na posho za wafanyakazi wao.
Wafanyakazi wa sekta hiyo wameongezewa kiwango cha mishahara yao kutoka TZS
70,000 mwaka 2010 hadi 145,000 kwa sasa, sawa na ongezeko la asilimia 107.
Mheshimiwa
Spika,
Natumia fursa hili kulipongeza Baraza lako
Tukufu kwa kupitisha Sheria Namba 2 ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2011. Sheria hii imetuwezesha kuweka Miundo imara
ya uendeshaji na usimamizi wa Utumishi wa Umma na mambo mengine yanayohusiana na
hayo.
Kutokana na sheria hii, Serikali imeunda
Kamisheni ya Utumishi wa Umma pamoja na Tume ya Utumishi Serikalini, Tume ya
Utumishi ya Mahakama, Tume ya Utumishi ya Baraza la Wawakilishi na Tume ya
Utumishi ya Idara Maalum. Taasisi hizi
ni muhimu katika kulinda maslahi na haki za wafanyakazi hapa nchini na zimetoa
mchango mkubwa katika kuweka misingi mikuu ya maadili ya Utumishi wa Umma na
usimamizi wa rasilimali watu.
Jumla ya Sheria za kazi 12 zimetungwa na
zimeanza kutumika, zikiwemo kanuni za mwaka 2014 za Sheria ya Utumishi wa Umma
Nambari 2 ya mwaka 2011.
Haya yote ni mafanikio ya utekelezaji wa ahadi nilizozitoa za kulinda na
kukuza maslahi ya wafanyakazi Serikalini na katika Sekta Binafsi.
Mheshimiwa
Spika,
Katika kuimarisha ustawi wa kinamama na
watoto, kuanzia tarehe 21 Aprili 2015 tulianzisha utaratibu
unaowawezesha akina mama wanachama wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (ZSSF), kulipwa
mafao ya uzazi wanapokwenda
kujifungua ili yawasaidie kuimarisha
afya zao na za watoto katika kipindi hicho muhimu. Malipo ya mafao ya uzazi
hayaathiri malipo ya mafao, ambayo muhusika atapata wakati atakapostaafu.
Mheshimiwa
Spika,
Tunamaliza miaka mitano ikiwa tumo katika
hatua za mwisho za kukamilisha Sera ya Usalama na Afya Kazini ili kuweka mfumo
mzuri wa afya katika maeneo ya kazi kwa lengo la kuwakinga wafanyakazi na ajali
na majanga mengine yanayotokea katika sehemu za kazi. Aidha, tunamaliza kipindi hiki ikiwa tupo
katika hatua za kuanzisha Bima ya Afya.
Tumeshafikia hatua nzuri katika kuifikia azma hiyo.
SEKTA YA MIUNDOMBINU:
Mheshimiwa
Spika,
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya
Saba ilitambua kuwa lengo lake la kukuza uchumi wa Zanzibar halitaweza
kufanikiwa bila ya azma hiyo kwenda sambamba na uimarishaji wa miundo mbinu ya
uchumi kama vile barabara, bandari, viwanja vya ndege, kuimarisha maeneo huru
ya uwekezaji pamoja na kuwa na nishati ya uhakika ya umeme. Kwa hivyo, katika kipindi hiki cha miaka
mitano, jitihada kubwa zimefanywa katika kuimarisha miundo mbinu hiyo ya
uchumi.
Mheshimiwa
Spika,
Kuhusu miundo mbinu ya barabara, Serikali
imeendeleza na imekamilisha kazi za ujenzi wa barabara zote kuu zinazoingia
mjini. Kadhalika, tumeweza kujenga
barabara ndogo ndogo za mijini na mashamba na kuifanya Zanzibar kuwa mfano wa
nchi zenye mtandao mzuri wa barabara unaounganisha miji na mashamba na kuwa ni
kichocheo muhimu cha maendeleo ya uchumi na kurahisisha shughuli za usafiri wa
wananchi na mizigo.
Mheshimiwa
Spika,
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya
Saba, imekamilisha kazi ya ujenzi wa barabara 11 zenye urefu wa (km 102) katika
Kisiwa cha Pemba na barabara 4 zenye urefu wa km 34.85 katika Kisiwa cha
Unguja. Barabara hizi zimejengwa kwa
msaada wa MCC ya Marekani, BADEA na Saud Fund na SMZ. Hivi karibuni tunatarajia kufanya uzinduzi wa
barabara ya Wete hadi Gando (km 15) na barabara ya Wete hadi Konde (km 15),
ujenzi ambao utakuwa ni suluhisho la tatizo la barabara la muda mrefu
lililokuwa likiwasumbuwa wananchi wanaoishi katika maeneo mbali mbali. Kadhalika, kupitia Mfuko wa Barabara Serikali
ilikamilisha ujenzi wa barabara ya Amani hadi Mtoni (km 4) na barabara ya njia
nne hadi Umbuji yenye urefu wa (km 5).
Kazi ya ujenzi wa barabara ya Jendele, kupitia Cheju hadi Unguja Ukuu
(km 11.7) na barabara ya Koani hadi Jumbi (km 6.3) kwa msaada wa BADEA unaendelea. Kadhalika, ujenzi wa barabara ya Ole hadi
Kengeja yenye urefu wa (km 35) inayojengwa kwa msaada wa OPEC Fund umeshaanza
na ujenzi wa barabara kuu kutoka Chake chake hadi Wete unatarajiwa kuanza hivi
karibuni.
Mheshimiwa
Spika,
Uimarishaji wa usafiri wa anga ni miongoni
mwa masuala yaliyozingatiwa na Serikali ya Awamu ya Saba kama nilivyoahidi
wakati wa uzinduzi wa Baraza hili mwaka 2010.
Jitihada kubwa zimefanywa katika kukamilisha kazi ya ujenzi wa Uwanja wa
Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume ikiwa ni pamoja na ya kurukia ndege,
maegesho ya ndege, ujenzi wa uzio, sehemu ya kuegesha magari, ujenzi wa jengo
la abiria na kuimarisha huduma mbali mbali zinazohusiana na matumizi ya uwanja
huo. Ujenzi wa njia ya kurukia ndege na sehemu ya kuegesha ndege imekamilika na
ujenzi wa jengo jipya la Abiria katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid
Amani Karume umefikia hatua nzuri ya utekelezaji ambao tayari umeshafikia
asilimia sabini na Oktoba mwaka huu tutakabidhiwa, hii niahadi niliyopewa na uongozi
wa Serikali ya China.
Mheshimiwa
Spika,
Kuhusu kiwanja cha ndege cha Pemba, Serikali
inaendeleza mipango mbali mbali kwa ajili ya kukiimarisha kiwanja hiki ili
kiweze kutumika usiku na mchana na baadae kiweze kutumiwa na ndege zilizo kubwa
zaidi.
Katika juhudi tunazoendelea kuchukua za
kuimarisha kiwanja hicho, tarehe 16 Machi 2015 Serikali iliingia mkataba na
Kampuni ya Safegate ya Ujerumani kwa ajili ya uletaji wa vifaa pamoja na
kusimamia uwekaji wa taa katika kiwanja kwa gharama ya Dola za Kimarekani 508,219.45.
Hivi sasa, Kampuni hiyo imeshalipwa malipo ya awali ya aslimia 20.
Vifaa mbali mbali kwa ajili ya uwekaji taa
hizo vimeshafika Pemba na kazi ya uchimbaji misingi kwa ajili ya kulaza nyaya
imeanza. Kwa upande wa usimamizi wa “civil work” mtaalamu wa Kampuni hiyo
tayari amewasili katika kiwanja cha ndege cha Pemba kusimamia kazi ya uchimbaji
misingi na mashimo. Kazi ya uwekaji taa
inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi wa Julai.
Sambamba na juhudi hizi Serikali, inaendelea
kufanya mazungumzo na washirika wa maendeleo mbali mbali ili kupata fedha kwa
ajili ya kuimarisha zaidi Uwanja wa Ndege wa Pemba. Benki ya Maendeleo ya
Afrika (AfDB) imekubali kufadhili kazi ya Upembuzi Yakinufu na mpango mkuu wa
kiwanja hicho; kazi ambayo inatarajiwa kuanza ndani ya kipindi cha miezi sita
ijayo. Kukamilika kwa mradi huu kutasaidia sana katika jitihada zinazoendelea
kuchukuliwa na Serikali za kuitangaza Pemba katika masoko ya utalii duniani na
kuimarisha biashara na huduma za usafiri kwa wananchi wa Unguja na Pemba.
Mheshimiwa
Spika,
Serikali imezingatia umuhimu wa bandari, kwa
hivyo kwa kushirikiana na Kampuni ya Azam Marine imejenga majengo mapya ya
kupumzikia abiria katika Bandari ya Malindi.
Aidha, vifaa mbali mbali vimenunuliwa ili kuongeza ufanisi na kasi ya
upakiaji na uteremshaji wa mizigo katika meli zinazofika Bandari ya
Malindi. Serikali vile vile imeifanyia
matengenezo makubwa gati ya Mkoani Pemba ili kurahisisha shughuli za usafiri wa
vyombo na abiria wanaoitumia bandari hiyo.
Ujenzi wa gati ya Tumbatu unaendelea na
ujenzi wa gati ndogo ya Mkokotoni unategemewa kuanza katika mwaka wa fedha,
2015/2016. Katika kukabiliana na tatizo
la uhaba wa nafasi katika Bandari ya Malindi na kuwa na Bandari ya kisasa yenye
huduma bora zaidi, tayari Serikali imeanza hatua za awali za ujenzi wa Bandari
mpya ya Mpiga duri. Serikali ya Jamhuri
ya Watu wa China imekubali kushirikiana nasi katika ujenzi huo kupitia Benki ya
Exim ambapo hatua ya Upembuzi Yakinifu zimeshafanywa na Kampuni ya Chec ya China
ndio itakayojenga bandari hio kwa kushirikiana na Serikali.
Mheshimiwa
Spika,
Tumefikia hatua nzuri
katika kutekeleza Ujenzi wa bandari hiyo ambao ulibuniwa kabla ya mwaka 2000
wakati wa uongozi wa Dk. Salmin Amour Juma. Serikali imepanga kujenga Bandari
hiyo kubwa na ya kisasa ili Zanzibar iweze kwenda sambamba na mabadiliko ya
biashara na uchumi yanayotokea duniani.
Bandari hii mpya itahudumia meli
zenye uzito wa Tani 50, 000 (Deadweight tonnage) na itakuwa na urefu wa mita 300 na upana wa mita 490. Ujenzi wa
bandari hio utaanza mara tu baada ya kukamilika kwa ujenzi wa jengo jipya la
abiria la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume (Terminal 2).
Kwa lengo la kuimarisha usafiri wa baharini,
Serikali iliamua kujenga Meli ya abiria na mizigo ili kupunguza tatizo kwa
wananchi na wafanyabiashara. Meli hiyo
inayojengwa katika Jamhuri ya Korea inayotarajiwa kufika nchini katika mwezi wa
Julai, 2015 ina uwezo wa kuchukua abiria 1,200 na mizigo yenye uzito wa tani
200.
Mheshimiwa
Spika,
Nishati ya umeme ni muhimu katika kuimarisha
ukuaji wa uchumi wa nchi na ustawi wa maendeleo ya wananchi wetu. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika
awamu zake mbali mbali imefanya jitihada kadhaa za kuhakikisha Zanzibar inakuwa
na huduma ya nishati ya umeme ya uhakika. Katika kipindi cha uongozi wa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, tumeweza kukamilisha hatua
hizo zilizoanzishwa na Awamu ya sita za
kuwa na umeme wa MW 100 kwa Unguja na MW 20 kwa Pemba, viwango ambavyo ni zaidi
ya mahitaji halisi ya nishati hiyo kwa sasa.
Katika hotuba ya tarehe 11 Novemba, 2010
nilipolizinduwa Baraza la nane, niliahidi kuwa Serikali itapeleka umeme katika
maeneo yote ambayo bado hayajapata nishati hiyo ikiwa ni pamoja na kisiwa cha
Makoongwe, Kisiwa Panza na Kisiwa cha Shamiani huko Pemba. Utekelezaji wa azma hii umefikia hatua ya
kuridhisha. Nina furaha kuelezea mafanikio makubwa ambayo Serikali imeyapata
katika utekelezaji wa usambazaji wa umeme.
Hivi sasa huduma za umeme zinapatikana katika miji yote na zimefikia
zaidi ya vijiji 129 badala 123 vilivyokadiriwa mwanzo.
UCHIMBAJI WA
MAFUTA NA GESI:
Mheshimiwa Spika,
Nimefurahi kuona kuwa Baraza hili la Nane limejadili kwa kina suala
la uchimbaji wa mafuta na gesi na
mmeweza kutoa michango na kuishauri
Serikali kwa namna mbali mbali kuhusiana na suala hili. Hivi sasa tumefikia
pazuri hasa tukizingatia kuwa Katiba Inayopendekezwa imezingatia matakwa ya
Zanzibar juu ya suala hili. Katika kipindi cha miaka mitano, Serikali imefanya
mazungumzo na kusaini makubaliano ya Awali na Kampuni zinajishughulisha na
uchimbaji mafuta, ikiwemo Kampuni ya RAK Gas ya Ras Al Khaima kufuatia ziara
yangu ya mwaka 2012 na kampuni ya Shell kufuatia ziara ya Uholanzi niliyoifanya
mwezi Agosti, 2013. Dhamira yetu ni
kuona kuwa katika kipindi kifupi kijacho mafuta na gesi yanachimbwa Zanzibar
baada ya kufanyiwa kazi masuala ya kisheria.
HUDUMA ZA JAMII:
Mheshimiwa
Spika,
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya
Saba, ilitambua wazi kuwa kuimarisha huduma za jamii ni jukumu lake la msingi
na hatua muhimu ya kuendeleza shabaha ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya
Januari 12, mwaka 1964. Katika kutekeleza
azma hiyo, Serikali imechukua jitihada mbali mbali katika kuimarisha
upatikanaji wa huduma bora za Elimu, Afya na Maji Safi na Salama katika maeneo
yote ya Unguja na Pemba, mijini na mashamba.
Mheshimiwa
Spika,
Kwa upande wa sekta ya elimu, niliahidi
kuendeleza mafanikio ya elimu yaliyopatikana katika Awamu zote za Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar zilizotangulia.
Kadhalika, Serikali yangu iliweka azma ya kuimarisha ubora wa elimu
inayotolewa katika ngazi zote kuanzia Maandalizi, Msingi, Sekondari, Elimu ya
Juu pamoja na Mafunzo ya Elimu Amali na Elimu Mbadala. Pamoja na hatua hizo, tulidhamiria kuimarisha
masomo ya sayansi hasa kwa watoto wa kike, mafunzo ya elimu maalum kwa watu
wenye ulemavu, kuimarisha maslahi ya walimu pamoja na kuyaimarisha mazingira ya
kusomea yakiwemo majengo na vifaa vya maabara na vitabu vya kiada na ziada.
Mheshimiwa
Spika,
Ni jambo la kufurahisha kuona mafanikio
makubwa ambayo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, imeweza
kuyapata katika utekelezaji wa malengo hayo niliyoyabainisha ikiwa ni utekelezaji
wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM mwaka 2010 – 2015 na mipango mingine ya Kitaifa
niliyoitaja hapo awali.
Wakati tukiwa katika mwaka wa tano wa
uongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, tunafarajika kwa
mafanikio ya kuandikisha watoto wote waliofikia umri wa kusoma. Serikali imeondoa michango ya wazazi katika
elimu ya msingi na kuondoa gharama za mitihani yote ya Sekondari kuanzia mwaka
wa fedha 2015/2016 ili kuwawezesha watoto wote kupata elimu bila ya malipo kwa
shabaha ile ile ya tamko la Mwasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar Marehemu Mzee
Abeid Amani Karume alilolitangaza tarehe 23 Septemba, 1964. Katika kipindi hiki cha miaka mitano,
tunajivunia kuongezeka kwa uandikishaji wa wanafunzi katika ngazi ya elimu ya
lazima; Maandalizi, Msingi na Sekondari kutoka jumla ya wanafunzi 317,278 mwaka
2010 hadi kufikia wanafunzi 390,464 mwaka 2015.
Mheshimiwa
Spika,
Serikali imepiga hatua kubwa katika
utekelezaji wa mradi wa uimarishaji wa elimu ya lazima kwa kutumia fedha zetu
na michango ya washirika wa maendeleo kwa kujenga majengo mapya ya skuli,
kununua vifaa vya maabara na samani.
Serikali imeweza kushirikiana vyema na wananchi pamoja na sekta binafsi
katika kuongeza nafasi na fursa za kupata elimu kwa watoto wa Zanzibar na
kupanua wigo wa mafunzo yanayotolewa katika elimu ya juu hususan katika Chuo
Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA).
Kadhalika, Serikali iliendelea kuchukua hatua ya kuwapatia mikopo vijana
wanaojiunga na taasisi za elimu ya juu kupitia Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu,
Zanzibar.
Idadi ya skuli zimeongezeka. Skuli za maandalizi sasa ni 270 kutoka 238
mwaka 2010. Skuli za msingi zimeongezeka
kutoka 299 mwaka 2010 hadi skuli 370 mwaka 2015. Serikali inajiandaa kujenga skuli mpya 10 za
ghorofa ili kuongeza nafasi kwa wanafunzi. Ili kwenda sambamba na mabadiliko ya sayansi
na teknolojia, Serikali inatekeleza mradi wa Tz – 21 unaohusiana na masomo ya
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika skuli za msingi 248. Skuli hizo zimepatiwa vifaa mbali mbali ikiwa
ni pamoja na Kompyuta, Vitabu na Vifaa vyengine vya ufundi wa TEHAMA pamoja na
kuwapatia mafunzo watendaji wanaosimamia mradi huo.
Mheshimiwa
Spika,
Katika hotuba yangu ya uzinduzi wa Baraza
hili, niliahidi kuchukua hatua madhubuti za kuimarisha Elimu ya Sekondari kwa
kuchukua hatua mbali mbali ikiwa ni pamoja na kuyaimarisha mazingira ya
ufundishaji na usomaji kwa kuwapatia walimu mafunzo, kujenga Skuli mpya 21 ili
kuongeza nafasi, kuzifanyia matengenezo makubwa skuli sita za sekondari na
kuzipatia vitabu na vifaa vya maabara skuli zetu pamoja na samani. Kadhalika, kwa lengo la kuwashajihisha watoto
wa kike kusoma masomo ya sayansi, niliahidi kuanzisha skuli maalum za sekondari
kwa ajili ya watoto wa kike, ambapo skuli ya sekondari ya Ben Bella kwa Unguja
na skuli ya Utaani kwa Pemba tayari zimeshaanzishwa kwa lengo hilo.
Idadi ya Skuli za Sekondari kuanzia kidatu
cha kwanza hadi cha Sita imeongezeka kutoka skuli 194 mwaka 2010 hadi skuli 263
mwaka 2015. Serikali imeweza kukamilisha
azma yake ya kuzifanyia matengenezo makubwa Skuli sita za zamani za Sekondari
za Unguja na Pemba na kuzipatia vifaa vya maabara na samani kama
ilivyoahidiwa. Aidha, tumeweza
kukamilisha ujenzi wa Skuli mpya za Sekondari 19 kama tulivyoahidi na tayari
skuli hizo zinatumika.
Serikali imechukua jitihada maalum katika
kuhakikisha watoto wenye mahitaji maalum wanapata haki yao ya elimu katika
skuli zetu mbali mbali, kupitia mpango wa elimu mjumuisho, pamoja na
kuyaimarisha mafunzo ya elimu ya amali na ufundi katika vituo vya
Mwanakwerekwe, Mkokotoni na Vitongoji. Vituo hivi vimetoa mchango mkubwa wa kuwapatia
vijana wetu mafunzo mbali mbali ya fani za ufundi zikiwemo uashi, useremala,
ushoni, uhunzi, upishi, uchoraji, ufundi bomba, ufundi umeme, magari, mafriji,
teknolojia ya habari na fani nyenginezo.
Mheshimiwa
Spika,
Mafanikio makubwa yamepatikana katika
kuimarisha fursa za elimu ya juu nchini ili kwenda sambamba na mahitaji ya
wataalamu wetu wenyewe. Wanafunzi
waliojiunga katika vyuo vikuu vitatu vya Zanzibar; imeongezeka kutoka vijana
3,624 mwaka 2010 na kufikia 6,367 mwaka 2015.
Mafanikio hayo ni pamoja na ongezeko la masomo katika viwango mbali
mbali kuanzia Ngazi ya Cheti hadi Shahada ya Uzamivu (PhD). Katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar
(SUZA) katika kipindi hiki, idadi ya skuli za masomo (faculties) imeongezeka
kutoka moja hadi tano. Kadhalika, chuo
hiki tayari kimeanza benchi ya pili ya Shahada ya Uzamivu ya Kiswahili pamoja
na kuanzisha kitivo cha masomo ya udaktari (Faculty of Medicine) katika mwaka
2013. Jambo kubwa zaidi ni ongezeko la
wasichana katika masomo ya juu. Katika
Mahafali ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) mwaka 2014, idadi ya
wahitimu wa kike ilikuwa ni asilimia 64 kati ya wahitimu 741 wa chuo hicho.
Mwaka huu wa 2015 chuo kina wanafunzi 2705 ambapo 1654 ni wanawake na 1051 ni
wanaume. Hayo ni miongoni mwa mafanikio
ambayo nchi yetu inapaswa kuyaendeleza.
Mheshimiwa
Spika,
Kwa lengo la kuhakikisha wanafunzi wanaopata
fursa ya elimu ya juu wanaendelea na masomo yao, Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar inatoa mikopo kila mwaka kwa wanafunzi wapya na wale
wanaoendelea. Hadi kufikia mwezi
Disemba, 2014 wanafunzi 4,678 walipewa mikopo yenye thamani ya TZS bilioni
19.4. Katika mwaka wa fedha
2014/2015. Serikali ilipanga kutoa
udhamini kwa wanafunzi wapya wa elimu ya juu 1,200. Hata hivyo, idadi halisi iliongezeka hadi
kufikia wanafunzi 1,611 sawa na ongezeko la asilimia 34 ya malengo.
Mheshimiwa
Spika,
Uimarishaji wa huduma za afya nchini ni
miongoni mwa vipaumbele vya Serikali ya Mapinduzi, Awamu ya Saba na Shabaha ya
Mapinduzi ya mwaka 1964. Miongoni mwa
jukumu la msingi la Serikali lilikuwa ni kuyaendeleza mafanikio ya Sekta ya
Afya ya Awamu za Serikali zilizopita na kutekeleza mikakati ya mipango ya
Kitaifa kupitia Ilani ya Uchaguzi ya CCM, MKUZA II, Dira ya 2020 na Malengo ya
Milenia pamoja na kuhakikisha Sera ya Afya inatekelezwa kwa vitendo kwa
kushirikiana na wananchi.
Miongoni mwa malengo makuu ya Serikali yalikuwa
ni kuimarisha huduma za Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja ili ifikie kuwa Hospitali
ya Rufaa, kuiimarisha Hospitali ya Abdalla Mzee na Hospitali ya Wete ili zifikie
hadhi ya kuwa Hospitali za Mkoa. Kwa
upande wa Hospitali ya “Cottage” ya Kivunge na Makunduchi kwa Unguja na
Micheweni na Vitongoji kwa Pemba, Serikali ilikusudia zifikie hadhi ya
Hospitali za Wilaya. Hospitali ya Koteji
ya Makunduchi imepiga hatua mbele zaidi. Malengo mengine ni kuanzisha Vitengo vya
matatizo ya Figo, Maradhi ya Moyo na Saratani ili huduma hizo ziweze kupatikana
nchini pamoja na kuziimarisha huduma za kinga na tiba.
Mheshimiwa
Spika,
Mabadiliko makubwa yamefanywa katika kipindi
cha miaka mitano katika kuimarisha mazingira na huduma zinazotolewa katika
Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja ili ifikie hadhi ya Hospitali ya Rufaa. Hatua zilizochukuliwa na Serikali ni pamoja
na kuipatia Hospitali hiyo vifaa vya kisasa katika Chumba cha Upasuaji, Maabara
ya Uchunguzi wa maradhi, Wodi ya Wagonjwa Mahatuti, Wodi ya Wazazi na Chumba
cha Wagonjwa wa dharura. Jengo jipya la huduma
za upasuaji wa Kichwa na Uti wa Mgongo limefunguliwa likiwa ni la huduma za
aina yake katika Afrika ya Mashariki. Kituo cha Meno cha Tabasam kwa ajili ya
kuwahudumia watu wenye matatizo ya midomo nacho kimeanzishwa.
Vile vile, Serikali imeanzisha Kitengo cha
uchunguzi wa maradhi ya mfumo wa chakula pamoja na Wodi mpya ya Wagonjwa
Mahututi. Hivi sasa, Serikali inaendelea
na mradi wa ujenzi wa jengo jipya la watoto ambalo pia litakuwa na huduma za
wagonjwa wa maradhi ya figo. Ni jambo
lililo wazi kuwa huduma katika Hospitali ya Mnazi Mmoja zimeimarika sana na
zimepunguza kwa kiasi kikubwa idadi ya wagonjwa ambao walikua wakifuata baadhi
ya huduma nje ya Zanzibar.
Mheshimiwa
Spika,
Serikali inaendelea na ujenzi mkubwa wa
Hospitali ya Abdalla Mzee kwa kuiwekea miundo mbinu ya kisasa na vifaa ili
iweze kukidhi kuwa Hospitali ya Rufaa Pemba. Katika Hospitali ya Wete, huduma zimeimarishwa za shughuli za
uchunguzi wa maradhi mbali mbali, ujenzi wa jengo la maabara mpya
umekamilika. Wodi mpya ya wazazi, wodi
ya wagonjwa wa akili na chumba cha upasuaji zimejengwa.
Mheshimiwa
Spika,
Mwamko wa wananchi juu ya elimu ya afya na
jitihada za Serikali katika kuimarisha huduma hizo kumechangia sana katika
kuongezeka kwa asilimia ya mama waja wazito wanaojifungua katika vituo vya afya
hadi kufikia asilimia 68.3 mwaka 2014. Hivi sasa huduma za kujifungua
zinapatikana bure katika vituo 41 nchini.
Vifo vya watoto wanaozaliwa hai chini ya
umri wa mwaka mmoja vimepungua kutoka 54/1000 mwaka 2010 hadi 46/1000 mwaka
2012 zaidi ya lengo lililokuwepo la vifo 48/1000. Vile vile kuna mafanikio katika kupunguza
vifo kwa watoto chini ya umri wa miaka 5 kutoka 73/1000 mwaka 2010, 66/1000
mwaka 2012. Lengo ni kufikia
50/1000. Vifo vya kinamama kutokana na
uzazi vinazidi kupungua.
Kadhalika, Serikali imeendelea kudhibiti
kiwango cha Malaria na VVU/UKIMWI kuwa chini ya asilimia moja. Kwa mujibu wa
tathmini ya kiwango cha maambukizo ya VVU, Zanzibar inakisiwa kuwa na asilimia
0.5 ya maambukizi kwa watu wenye umri kati ya miaka 15 hadi 24, asilimia 0.6
kwa wenye umri kati ya miaka 15 hadi 49.
Katika kipindi hiki Serikali imejenga ghala
la kisasa la kuhifadhia dawa katika eneo la Maruhubi. Serikali za Marekani na Denmark zimesaidia
ujenzi huu. Vile vile, Ofisi ya Mkemia
Mkuu hivi sasa imehamishiwa katika eneo hilo ili kupata fursa ya kufanya
shughuli zake katika mazingira yaliyo bora zaidi.
Mheshimiwa
Spika,
Jitihada kubwa zimefanywa katika
kukiimarisha Chuo cha Taaluma ya Sayansi za afya. Mafanikio yamepatikana ambapo
kwa sasa idadi ya madaktari wazalendo imefikia 102. Tunategemea idadi hiyo itaongezeka hasa baada
ya Serikali kuamua kuanzisha mafunzo ya udaktari katika Chuo Kikuu cha Taifa
cha Zanzibar (SUZA) na wanafunzi wanaosomea udaktari Tanzania Bara na nje ya
nchi. Kwa wastani daktari mmoja alikuwa
akihudumia wagonjwa 31,838 (1:31,838) mwaka 2010 na ambapo sasa anahudumia
wastani wa wagonjwa 18,810 (1:18,810).
Pamoja na madaktari wazalendo, wapo madaktari wa kigeni 20 kutoka China
na 20 kutoka Cuba. Idadi hii inafanya
madaktari wote kuwa 151 ambapo wastani wa daktari mmoja anahudumia watu 9,093
(1:9,093).
Napenda nitoe shukurani zangu kwa washirika
wetu wa maendeleo wanaotuunga mkono katika azma yetu ya kuziimarisha huduma za
afya nchini. Tunathamini sana misaada
yao ya mafunzo na utaalamu, vifaa, wafanyakazi na nyenzo mbali mbali ambazo kwa
pamoja zimeweza kutuletea mafanikio tuliyoyapata. Zanzibar ina mtandao mzuri wa huduma za afya
zinazotolewa katika hospitali na vituo vya afya vya Serikali, Vikosi vya
Ulinzi, Taasisi za Kijamii na vituo vya watu binafsi kuliko nchi nyingi. Katika Bara la Afrika; mwananchi wa Zanzibar
hatembei umbali wa kilomita tano, bila ya kupata huduma za afya kwenye kituo
cha afya.
MAJI SAFI NA SALAMA:
Mheshimiwa
Spika,
Wakati nikilifungua Baraza hili, nilisema
kuwa maji ni uhai na hasa maji safi na salama.
Kwa hivyo, Serikali yangu imeendeleza jitihada za Serikali za Awamu
zilizopita na kuweka mikakati mipya katika kuwapatia wananchi huduma za maji
safi na salama. Mipango ya Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, ni pamoja na kukamilisha mradi wa
usambazaji wa maji katika Mkoa wa Mjini Magharibi, kupunguza upotevu wa maji na
kuvihifadhi vianzio vya maji.
Katika ahadi zangu nilibainisha kuwa kwa mujibu wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM
ya mwaka 2010 – 2015, Serikali inakusudia kusambaza huduma za maji safi na
salama kufikia asilimia 95 kutoka asilimia 75 katika miji na asilimia 80 kutoka
asilimia 60 katika vijiji ifikapo mwaka 2015. Hali ya uzalishaji wa maji
imefikia lita milioni 17.6 ambayo imewezesha kuongezeka kwa watu wanaopata maji
na kufikia 175,873 katika kipindi hiki.
Mahitaji yetu halisi ya maji ni lita milioni 214.6 ambapo uzalishaji
katika kipindi hiki umefikia lita milioni 163 sawa na asilimia 76 ya
mahitaji. Kutokana na takwimu hizi
upatikanaji wa maji katika Mkoa wa Mjini Magharibi umefikia asilimia 87.7, Mkoa
wa Kusini Unguja asilimia 76.45, Mkoa wa Kaskazini Unguja asilimia 71.68, Mkoa
wa Kusini Pemba asilimia 74.08 na Mkoa wa Kaskazini Pemba asilimia 56.42 ya
mahitaji halisi.
ARDHI NA MAKAAZI:
Mheshimiwa
Spika,
Serikali iliahidi kushughulikia suala la
matumizi bora ya ardhi kwa kuzingatia udogo wa ardhi tuliyonayo. Katika utekelezaji wa azma hii, Serikali
imetayarisha sera mpya ya ardhi ili kusimamia na kutekeleza mipango ya matumizi
bora ya ardhi. Sera hiyo pamoja na mambo
mengine imezingatia mabadiliko ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi yaliyopo na
yatakayokuja baadae.
Kazi ya usajili wa ardhi imeshafanywa katika
zaidi ya shehia 20 na zoezi la utambuzi linaendelea katika shehia 13. Jumla ya nyumba, viwanja na mashamba 22,398
vimeshatambuliwa sambamba na hatua hiyo, zoezi la utoaji wa Hati za matumizi ya
Ardhi linaendelea kwa kutoa hati mpya na kuzibadilisha zile za zamani. Hadi sasa jumla ya mikataba ya matumizi ya
ardhi 223 imeshasainiwa na kukabidhiwa wawekezaji. Vile vile, hati 1,310 za matumizi mbali mbali
ya ardhi zimetolewa na viwanja 1,691 vimepimwa, Unguja na Pemba.
Mheshimiwa
Spika,
Katika kukabiliana na tatizo la matumizi
mabaya ya ardhi, Serikali imeshakamilisha mpango mkuu wa matumizi ya Ardhi ya
Mji wa Zanzibar na Mpango Mkakati wa Maendeleo ya Ardhi Zanzibar, sambamba na
mipango ya matumizi ya ardhi ya Mikoa yote ya Zanzibar. Katika kuhakikisha uhifadhi wa Mji Mkongwe wa
Zanzibar, Serikali imeanzisha mfumo mpya kwa njia ya kuishirikisha Sekta ya
Umma na Sekta Binafsi (PPP) kwa ajili ya kuhifadhi nyumba ziliopo Mji
Mkongwe. Mfumo huo utafanywa kupitia
Kampuni itakayoitwa Hifadhi Zanzibar na tayari imeshasajiliwa na kuanza kazi
zake. Aidha, Serikali inaendelea na
matayarisho ya kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Miji ili kusimamia ustawi wa
maendeleo ya miji yetu.
Nina matumaini makubwa kuwa kupitia mipango
hiyo, wananchi wataelimika na watazidi kuifahamu mipango ya matumizi bora ya
ardhi na utaratibu huu utapunguza changamoto
zilizopo hivi sasa. Nawasihi sana
wananchi waendelee kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa mipango hii
ili tuweze kufikia azma yetu ya matumizi bora ya ardhi.
HABARI
NA MAWASILIANO:
Mheshimiwa
Spika,
Kwa upande wa habari, katika kipindi cha
miaka mitano, Serikali imeimarisha utoaji wa habari kwa wananchi ikiwa ni
pamoja na kurusha moja kwa moja matangazo yanayohusu vikao vya Baraza la
Wawakilishi. Tumeliwezesha Shirika la Utangazaji la Zanzibar (ZBC) kufanya
mageuzi ya kutoka mfumo wa "Analogue" kwenda "Digital" kwa
mafanikio na kwa wakati tuliopangiwa na Jumuiya za Kimataifa. Tumeongeza muda wa kutangaza, ambapo hivi
sasa ZBC Radio na TV zinakuwa hewani kwa saa 24. Vile vile, gazeti la Zanzibar Leo
linalotolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ubora wake wa habari na
uchapishaji umeongezeka na hivi sasa linapatikana kila siku katika maeneo mbali
mbali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aidha, Zanzibar imepiga hatua kubwa kwa kuongeza idadi ya vyombo vya
habari zikiwemo radio jamii 4 pamoja na vituo vya habari binafsi. Hali hii imechangia sana kuongezeka kwa uhuru
wa kupata habari na kusukuma maendeleo ya jamii yetu katika nyanja mbali mbali.
Vile vile, Serikali imetekeleza azma yake ya
kuwajengea wasanii wetu “Studio” za kisasa za kurekodia nyimbo na michezo ya
kuigiza kwenye jengo la zamani la Utangazaji la Sauti ya Tanzania Zanzibar,
baada ya kufanyiwa matengenezo makubwa.
Mheshimiwa
Spika,
Kwa lengo la kutekeleza azma ya Serikali ya
kukifufua Kiwanda cha Upigaji Chapa na Ofisi ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali
ili kurudisha hadhi yake na kuinua kiwango cha uzalishaji, jumla ya TZS milioni
5,532.40 zimetumika kwa matengenezo ya majengo yaliyokuwa kiwanda cha sigara
Maruhubi pamoja na ununuzi wa mashine mpya za kisasa za uchapishaji za kiwanda
hicho. Serikali ina lengo la kukiimarisha zaidi ili kiweze kuchapisha magazeti,
vitabu vikubwa na kadhalika. Fedha kwa ajili ya kazi hio tayari zimepatikana
kutokana na msaada wa Serikali ya Oman. Ni dhahiri kukamilika kwa kiwanda hiki
kumeipunguzia mzigo Serikali na kitaiwezesha kutoa huduma zenye ubora wa
kiwango kikubwa zaidi.
Mheshimiwa
Spika,
Kwa lengo la kuziimarisha huduma za
mawasiliano Serikalini, katika kipindi hiki cha kwanza cha Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, Serikali imeanzisha mradi wa
“e-government” ambao uliuzinduliwa mwezi wa Januari mwaka 2013. Hadi hivi sasa,
jumla ya majengo 86 ya Serikali yameunganishwa katika mtandao wa Serikali
(e-government) na tayari yameanza kupata huduma ya “internet” bila ya malipo. Awamu ya kwanza ya mradi huu inaendelea
vizuri na maandalizi ya awamu ya pili yamekamilika, ambapo huduma za “e-health”
na nyengine zitaanzishwa. Hivi sasa Serikali imo katika maandalizi ya
kuiunganisha Zanzibar na Tanzania Bara kupitia mkonga wa Taifa na ule wa
kimataifa (ESSY).
UTAMADUNI NA MICHEZO:
Mheshimiwa
Spika,
Kwa lengo la kudumisha na kutangaza
utamaduni wetu, silka na desturi zetu, Serikali imefanikiwa kuandaa matamasha
mbali mbali ambayo yamesaidia sana katika kuendeleza na kuhifadhi utamaduni wa
mambo ya asili. Kadhalika, kwa
kushirikiana na wana michezo, Serikali imefanikiwa na juhudi zake za kufufua na
kuimarisha michezo nchini. Ni jambo la
kufurahisha kuona kuwa baadhi ya wawakilishi katika Baraza la Wawakilishi
wamekuwa mstari wa mbele katika jambo hili kwa kuanzisha timu na vikundi vya
michezo na mazoezi katika majimbo yao na kuzipatia timu hizo vifaa mbali mbali.
Serikali imeanzisha mashindano ya riadha ya
Wilaya, kwa Wilaya zote kumi za Zanzibar na timu za michezo mbali mbali,
zimepatiwa vifaa. Viwanja vyetu vimeimarishwa
na hivi karibuni Serikali kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa
China imeanza kukijenga upya Kiwanja cha Mao- Tze Tung.
Ni jambo la kujivunia kuona kuwa, katika
kipindi hiki cha kwanza cha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba,
yenye Muundo wa Umoja wa Kitaifa tumeweza kuvijenga upya Viwanja viwili vikubwa
na vya kisasa; Kiwanja cha Kariakoo kwa Unguja na Kiwanja cha Tibirinzi kwa
upande wa Pemba. Kiwanja cha Kariakoo nilikifungua rasmi tarehe 8 Januari,
katika shamra shamra za Miaka 51 ya Mapinduzi.
Vile vile, Kiwanja cha Tibirinzi nacho tunaweza kukifungua wakati wowote
kuanzia Mwezi ujao. Viwanja hivi
vitawapa watoto wetu sehemu nzuri ya kwenda kucheza na kufurahia na kuwafanya
wakue wakiwa na afya bora.
Mheshimiwa
Spika,
Ujenzi wa Mnara wa Kumbukumbu ya Miaka 50 ya
Mapinduzi ulioko Michenzani umo katika hatua za mwisho za kumalizika. Niliweka
jiwe la Msingi la Ujenzi wa Mnara huu tarehe 11 Januari, 2014. Ni dhahiri kuwa kumalizika kwa Mnara huu
kutaongeza idadi ya maeneo ya kutembelea na kupumzikia kwa wananchi wa Zanzibar
na wageni wanaotutembelea na watapata fursa ya kujifunza historia ya Mapinduzi
yetu.
MAKUNDI
MAALUM:
Mheshimiwa
Spika,
Mashirikiano na mshikamano tuliouonesha
katika kipindi hiki cha miaka mitano katika Serikali yetu tumeweza kuinua hali
na ustawi wa wanawake, vijana na watoto, na wazee katika sehemu zote za Unguja
na Pemba. Serikali imeweza kuwahudumia na kuwatunza wazee kwa kuyaimarisha
makaazi yao na kuwapatia huduma muhimu za kila siku kwa maisha yao, kwa kiwango
cha kuridhisha. Sheria Namba. 6 ya Mwaka
2011 mlioyoipitisha imetupa mwongozo imara katika kuweka mazingira bora ya kupatikana
haki muhimu za watoto wanaishi na kukua katika mazingira mbali mbali. Mahakama
ya watoto tuliyoifungua rasmi mwezi Februari mwaka 2013 inaendelea kuimarisha
utoaji wa haki na kuongeza kasi katika uendeshaji wa kesi zinazohusu masuala ya
watoto. Pamoja na hatua hiyo, Serikali
imefungua vituo vya kushughulikia waathirika wa vitendo vya udhalilishaji wa
kijinsia katika Hospitali zetu za Mnazi Mmoja, Kivunge, Makunduchi na Chake
chake vikiwa na wataalamu wote wanaohusika katika kuchukua hatua.
Mheshimiwa
Spika,
Katika kuifanikisha Kampeni ya udhalilishaji
wa wanawake na watoto tuliyoizindua rasmi tarehe 6 Disemba, 2014. Mwamko uliopo
katika majimbo yenu umekuwa ni chachu ya mafanikio makubwa tunayoyashuhudia
katika Kampeni hii.
Katika juhudi zinazoendelea kuchukuliwa za
kuimarisha maslahi ya wazee. Serikali
imeamua kuanzisha malipo ya pencheni kwa wazee wote (Universal Pension). Kwa kuanzia malipo haya yatatolewa kwa wazee
wenye umri wa miaka sabiini (70). Tathmini ya awali imebainisha kuwa jumla ya
wazee 27,366 watafaidika na mpango huu kwa kulipwa kila mwezi. Serikali tayari imeweka TZS bilioni 1.65 kwa
ajili ya malipo hayo kwa muda wa miezi mitatu ya mwanzo. Zoezi hili linatarajiwa kuanza rasmi Aprili
Mosi mwezi, 2016. Katika mpango huu,
wazee wote wa Zanzibar waliofikia umri huu watafaidika kwa kupewa TZS
20,000 kila mwezi bila ya kujali historia ya kazi walizokuwa wakifanya kabla ya
kufika umri huo. Imani yangu ni kuwa
utaratibu huu mpya tuliounzisha utasaidia wazee wengi walikuwa katika ajira
zisizo za Kiserikali, hasa wakulima na wajasiriamali, ambao walikuwa wakijikuta
hawana msaada wowote wakati wanapostaafu.
Vile vile, katika kipindi hiki cha miaka
mitano, Serikali imefanya jitihada mbali mbali ili kuwasaidia watu wenye
ulemavu. Mfuko Maalum wa Watu Wenye
Ulemavu umeanzishwa na niliuzindua
mwaka 2012. Mfuko huu hivi sasa una
jumla ya TZS milioni 167.6 ambazo zitatumika kwa mahitaji mbali mbali ya watu
wenye ulemavu. Vile vile, Usajili wa watu wenye ulemavu uliofanywa kwenye
Wilaya zote za Unguja na Pemba sasa umekamilika, na umesaidia sana kuwatambua
ili kurahisisha upangaji na utekelezaji wa mipango yetu ya maendeleo. Kadhalika, Serikali inaendelea kutoa ruzuku
kwa Jumuiya za Watu wenye Ulemavu Unguja na Pemba ili ziweze kutimiza malengo
yao.
DEMOKRASIA
NA UTAWALA BORA:
Mheshimiwa
Spika,
Katika hotuba yangu ya uzinduzi wa Baraza
hili la Nane niliahidi kuwa Serikali nitakayoiongoza itazingatia utawala bora
wenye kuheshimu sheria na haki za binaadamu. Vile vile, nilieleza kwamba
nitaongoza nchi kwa misingi ya Katiba na Sheria za Zanzibar na Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania. Nimefarajika kwa
namna ambayo tumeweza kutekeleza dhamira hizo.
Katika kipindi hiki cha kwanza cha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,
Awamu ya Saba, tumeweza kutekeleza mipango mbali mbali kwa ajili ya kuimarisha
Utawala Bora ikiwemo kuendelea kuunda Wizara ya Nchi inayosimamia masuala ya
Utawala Bora.
Juhudi kubwa zilielekezwa katika kuhakikisha
kuwepo kwa taasisi zilizo huru zinazoendeshwa kwa kuzingatia Katiba na Sheria
zinatekeleza majukumu yake kwa uadilifu na mashirikiano. Serikali imeunda Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na
Uhujumu Uchumi baada ya Baraza hili kutunga Sheria Namba 1 ya mwaka 2012. Vile
vile, imeimarisha Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na
kuiwezesha kujenga na kuifungua Ofisi mpya Pemba kwa ajili ya kutekeleza majukumu
yake vizuri. Juhudi kubwa zimefanywa
kuimarisha Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ikiwa ni pamoja na kuiongezea idadi
ya wanasheria ili itekeleze majukumu yake kwa ufanisi. Tume ya kupitia Sheria imeendelea na
itaendelea na kazi zake za kushauri kuondosha zile zilizopitwa na wakati na
kuzifanyia marekebisho zenye kuhitajika.
Kukamilika kwa Sheria ya Maadili ya Viongozi
wa Umma kufuatia mswada wa Sheria hiyo uliopitishwa, tarehe 30 Januari,
2015, na Baraza hili ni hatua muhimu katika kuimarisha Utawala
Bora na demokrasia nchini. Nina imani kwamba viongozi wote watatekeleza
majukumu yao kwa kuzingatia sheria hii katika utendaji haki na utoaji wa huduma
zilizo bora kwa wananchi.
Mheshimiwa
Spika,
Serikali inaendelea kutekeleza mageuzi
kwenye mfumo wa kiutawala kwa kuzipa uwezo zaidi Serikali za Mitaa ikiwa ni
hatua muhimu ya kuimarisha Utawala Bora. Serikali imeandaa Sera ya Serikali za
Mitaa pamoja na Mpango wa Utekelezaji.
Natoa shukurani kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa michango mbali
mbali iliyowezesha kuifanyia marekebisho Sheria Namba 3 na 4 ya mwaka 1995
na Sheria Namba 1 ya mwaka 1998 hadi ikatungwa
Sheria mpya ya Tawala za Mikoa na Sheria mpya ya Serikali za Mitaa za
mwaka 2014. Aidha, natoa shukurani kwa wananchi kwa kutuunga mkono katika
utekelezaji wa mageuzi haya.
Ni dhahiri kuwa mafunzo yaliyotolewa kupitia
Semina Maalum kwa viongozi wa ngazi mbali mbali yalikuwa ni chachu ya kuwapa
maarifa mapya na kuongeza uzoefu wenu na hatimae yaliwezesha kutekeleza
majukumu yenu kwa ufanisi zadi. Utaratibu tulioanzisha wa kuziita Ikulu Wizara zote za Serikali kuja
kuwasilishaTararifa za Utelezaji wa
Mpango Kazi kila baada ya robo mwaka umetuwezesha kutekeleza majukumu yetu kwa uwazi na kuimarisha
uwajibikaji, mashirikiano na mahusiano
baina ya Idara mbali mbali za Wizara za Serikali.
Kadhalika, utaratibu huu umetusaidia kupunguza muingiliano wa majukumu baina ya
Wizara moja na Wizara nyengine. Aidha,
mpango huu umepanua upeo na maarifa katika
kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo kwa mujibu wa vipaumbele na upatikanaji wa rasilimali
fedha na watu. Haya yote ni mafanikio
tuliyoyapata katika kuleta uwazi na uwajibikaji ambayo ni mambo ya msingi
katika Mfumo wa Serikali ninayoiongoza.
Mheshimiwa
Spika,
Katika kipindi cha miaka mitano, Serikali
imechukua hatua mbali mbali za kuimarisha Manispaa ya Zanzibar pamoja na miji
ya Chake Chake, Wete na Mkoani, Serikali ilianzisha Mradi wa Huduma za Jamii
(ZUSP) mwaka 2011. ili kuimarisha
upatikanaji wa huduma muhimu katika miji hiyo, kuimarisha haiba, mazingira
pamoja na kuhifadhi eneo la urithi wa Mji Mkongwe.
SEKTA YA SHERIA:
Mheshimiwa
Spika,
Katika kipindi cha miaka mitano hii, Serikali
imechukua hatua kadhaa za kuimarisha mazingira ya utendaji kazi katika Mahkama
kwa lengo la kuongeza ufanisi katika kazi zake, kupunguza mrundikano wa kesi na
kuimarisha maslahi ya wafanyakazi.
Serikali imeyafanyia matengenezo makubwa majengo ya mahkama likiwemo
jengo la kihistoria la Mahkama Kuu Vuga na Mahkama nyengine nchini.
Kwa upande wa majaji, Serikali imefanikiwa
kuongeza idadi yao kutoka wawili mwaka 2011 hadi sita (wakiwemo wanawake
wawili) mwaka 2014, sawa na ongezeko la asilimia 200. Kwa upande wa
Mahakimu wa ngazi mbali mbali, Serikali imefanikwa kuongeza idadi
yao kutoka 43 mwaka 2010 hadi 85 mwaka 2015. Hii ni sawa na ongezeko la
asilimia 97.7. Kadhalika, Serikali
imeiongeza bajeti ya Mahakama kutoka TZS bilioni 1.3 mwaka 2010/2011 hadi TZS
bilioni 5 mwaka 2013/2014. Hii ni sawa
na ongezeko la asilimia 284.6.
Mheshimiwa
Spika,
Wakati huo huo, katika kipindi cha miaka
mitano, Afisi ya Mufti wa Zanzibar imeendelea kuratibu na kusimamia majukumu
yake ya kisheria. Katika kipindi cha
miaka mitano, watendaji wa Afisi ya Mufti wametembelea Madrasa za Kurani 164 na
Misikiti 166 na kutoa ushauri juu ya maendeleo ya taasisi hizo. Aidha, Madrasa 500 za taasisi za kidini 73
zimepatiwa usajili pamoja na kurushwa hewani kwa vipindi 124 vya nasaha na
mawaidha ya mafundisho ya kiislamu kupitia Radio ya ZBC. Vile vile, Afisi ya Mufti imeshughulikia na
kutatua migogoro mbali mbali pamoja na kuhamasisha amani na utulivu.
Kadhalika, Serikali imefanya jitihada mbali
mbali katika kipindi hiki cha miaka mitano ya kuziimarisha Mahakama za Kadhi
ili kuendesha shughuli zake kwa ufanisi na haraka. Jitihada hizo ni pamoja na kuongeza idadi ya
makadhi kutoka 12 hadi 15 na kuimarisha mazingira ya kufanyia kazi kwa
kuyafanyia matengenezo makubwa majengo ya Ofisi za Mahakama na kuzipatia vifaa
na samani. Hatua hizo zimechangia sana
katika kuongeza ufanisi na kupunguza malalamiko ya wananchi kuchelewa kufanyiwa
kazi mashauri yao.
Mheshimiwa
Spika,
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, imefanya
jitihada kubwa ya kuiimarisha Mahakama ya Ardhi ili kuiongezea uwezo wa kutatua
migogoro ya ardhi. Idadi ya Mahakimu
katika Mahakama hiyo imeongezwa kutoka Mahakimu wawili hadi wanane katika
kipindi hiki cha awamu ya saba. Hatua
hiyo imeiwezesha Mahakama kupunguza mrundikano wa kesi za migogoro ya ardhi
kutoka 800 hadi 200. Mazingira ya
kufanyia kazi yameimarishwa ambapo Mahakama hiyo inatumia jengo lilioko mjini
na Koani Unguja na kwa upande wa Pemba ipo Mahakama ya Wete na Chake
Chake. Hivi sasa mashauri ya migogoro ya
ardhi yanafanyika kwa haraka zaidi ikilinganishwa na miaka iliyopita jambo ambalo
limepunguza kwa kiasi kikubwa malalamiko ya wananchi.
Katika kipindi hiki cha miaka mitano,
Serikali imefanya jitihada za makusudi za kuimarisha Ofisi ya Mkurugenzi wa
Mashtaka kwa lengo la kuongeza uwajibikaji na umahiri wa kisheria katika
usimamizi wa mashtaka. Idadi ya
Wanasheria wa Serikali imeongezwa kutoka 28 waliokuwepo mwaka 2010 hadi kufikia
50 mwaka 2015. Ongezeko hili ni sawa na
asilimia 78.5. Ongezeko hilo limeiwezesha Ofisi ya DPP kuendeleza mashtaka ya
kiraia (kuwatumia Wanasheria badala ya polisi) katika mahkama za Mikoa yote na
Wilaya sita. Wilaya nne zilizobakia zinatarajiwa kuwa na utaratibu huu katika
utekelezaji wa mipango iliyobainishwa katia bajeti mliyoipitisha hivi karibuni ya
2015/2016. Nina imani kuwa hatua hiyo iliyofikiwa itazidisha imani ya wananchi
kwa Mahakama zetu na hukumu zinazotolewa.
BARAZA
LA WAWAKILISHI:
Mheshimiwa
Spika,
Natoa shukurani kwa mara
nyengine kwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Nane kwa kuendelea kuweka
misingi bora ya utawala bora na demokrasia. Kwa hakika mmeweza kutekeleza vyema
wajibu wenu wa kikatiba wa kutunga sheria na kuisimamia
Serikali kama
ilivyoainishwa katika kifungu cha 5A(1) na kufafanuliwa kifungu 5A(2) cha
Katiba ya Zanzibar ya 1984.
Katika kipindi cha miaka
mitano, mmefanya majukumu yenu kwa kufanya mikutano yenu katika hali ya salama
na utulivu. Licha ya kutofautiana kwa hoja na mitazamo kwa baadhi ya masuala
muhimu, mmeweza kupitisha miswada ya sheria 63 na baadae iliwasilishwa kwa Rais
kwa ajili ya kutia saini na sasa zimekuwa sheria kamili.
Takwimu zinaonesha kuwa
katika kipindi hiki cha miaka mitano, maswali 1558 ya msingi na maswala ya
nyongeza (3103) yameulizwa kwa Serikali na yalipatiwa majibu sahihi. Kamati
teule 5 mlizoziunda nazo zimetekeleza majukumu yake kwa uadilifu na umakini
mkubwa. Nawapongeza wajumbe wote wa kamati teule hizo kwa kufuatilia na kuibua
masuala juu mambo mbali na kuyaleta Barazani kwa kujadiliwa na baadae kuishauri
Serikali juu ya mambo yanayoibuka. Aidha, nalipongeza Baraza kwa kupokea na
kujadili hoja binafsi zinazowasilishwa.
Baraza hili la Nane
limeingia katika historia ya nchi yetu,
na litakumbukwa kwa kipindi kirefu
kijacho katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushiriki katika Bunge Maalum la Katiba kwa lengo la kuunda Katiba Inayopendekezwa ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Napenda nikushukuruni nyote Waheshimiwa
Wajumbe kwa ushiriki wenu huo uliotuwezesha kupata Katiba Inayopendekezwa
ambayo hivi sasa wananchi wanaisubiri kwa hamu kuipigia kura ya maoni.
Leo ni siku ya furaha kwa
upande mmoja na siku ya huzuni kwa upande mwengine. Nasema hivi kwasababu tunalivunja Baraza hili
kwa mbwembwe na madaha kutokana na mafanikio makubwa tuliyoyapata katika
kuiendeleza nchi yetu. Leo ni siku ya
huzuni kwa sababu tunaagana na nitalivunja rasmi Baraza hili la Nane na huenda
ikapita kipindi bila ya baadhi yetu kuonana ingawa tunategemeana kwa kiasi
kikubwa.
Mheshimiwa
Spika,
Kwa wale wenye dhamira ya
kurejea majimboni kwa ajili ya kutafuta ridhaa ya wananchi kwa mara nyengine,
nawatakia mafanikio ili warudi tena kwa miaka mitano myengine.
Kwa wale ambao wamefikia uamuzi
ya kutogombea tena, nawasihi waendelee kutumia maarifa na uzoefu walioupata
katika baraza hili katika kuongoza, kuhamasisha na kushiriki kikamilifu katika
harakati za maendeleo ya nchi yetu. Nyote mtabaki kuwa hazina kubwa katika
kupanga na kutekeleza mipango ya nchi hii.
Hata hivyo, kwa wale mtakaojaaliwa kuchaguliwa
tena na wananchi na kurudi Barazani, nataka nikunasihini na nikukumbusheni kuwa
mnapokuwa kwenye Baraza hili muendelee kuizingatia, kuitii na kuitekeleza kwa
vitendo Katiba ya Zanzibar, sheria ziliopo na kanuni za Baraza hili. Baraza la Wawakilishi ni muhimili uliowekwa
ndani ya Katiba. Hiki ni chombo kikubwa
kinachoendeshwa kwa misingi ya Utawala Bora.
Hakiendeshwi kwa kuendesha migomo au njia nyengine yoyote ya ubabe. Baraza ni chombo cha wananchi wa Zanzibar kwa
hivyo, suala lolote lenye maslahi ya wananchi, hapa ndipo pahala pa kisheria
pakulizungumza jambo hilo.
Kutoka nje ya Baraza si ufumbuzi wa tatizo
linalohusu hoja inayojadiliwa Barazani au hoja nyengine iliyokuwa haijadiliwi
na Baraza. Waheshimiwa Wajumbe nyinyi
ndio mnaotunga sheria za nchi, kwa hivyo nakunasihini msichanganye mambo. Kila sheria iliyotungwa na Baraza hili
matumizi yake yako wazi kwa kupitia taasisi iliyowekwa. Nyinyi ni Waheshimiwa
na wananchi na jamii kwa jumla wanakuheshimuni na vile vile wanaliheshimu
Baraza letu. Ni matarajio yangu kwamba
nanyi Waheshimiwa mtairejesha heshima hiyo kwao kwa kuwatimizia matarajio yao ili
tupate maendeleo zaidi.
Mheshimiwa
Spika,
Kila mmoja wetu anaelewa kwamba Baraza lako
linaendeshwa kwa misingi ya Sheria na Kanuni.
Hoja zinazotolewa na kujadiliwa na baraza hili zinaendeshwa kwa misingi
hiyo. Wakati Wajumbe wa Baraza la
Wawakilishi wa chama cha CUF waliposusia kikao cha tarehe 23 Juni, 2015, hoja
walizozitoa hazikuwa na mnasaba na hoja iliyokuwa imewasilishwa barazani ili
ijadiliwe kwa wakati huo. Siku hiyo Waziri wa Fedha alikuwa amewasilisha hoja
ya kujadiliwa kwa Mswada wa Sheria ya
Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2015/2016 ambao haukuwa na uhusiano wowo
hata kidogo na masuala ya kujiandikisha katika daftari la kudumu la kupiga
kura. Hoja yao ikuwa inahusiana na Sheria nyengine, Sheria ya Tume ya Uchaguzi
ya Zanzibar, Nam. 9 ya mwaka 1992 inayosimamiwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar
pamoja na Sheria ya Usajili wa Mzanzibari Mkaazi, Nam. 7 ya mwaka 2005. Waheshimiwa
Wajumbe msichanganye mambo.
Mheshimiwa
Spika na Waheshimiwa Wajumbe,
Uwamuzi wao wa kutoka nje ya Baraza
haukuzingatia uwamuzi wetu wa kuwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Mheshimiwa
Spika,
Uwamuzi wao wa kutoka nje haukuzingatia
mapenzi tuliyoyajenga baina yetu.
Mheshimiwa
Spika,
Uwamuzi wao wa kutoka nje haukuzingatia
umoja wetu mshikamano wetu tulioujenga katika miaka mitano.
Mheshimwia
Spika,
Uwamuzi wao wa kutoka nje haukuzingantia
sifa tulizozipata Zanzibar kutoka katika Jumuiya ya Kimataifa wa kuwa na
Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Mheshimiwa
Spika,
Uwamuzi wao wa kutoka nje haukuzingatia
maslahi ya Zanzibar.
Mhesimiwa
Spika na Waheshimiwa Wajumbe,
Tuwaulizeni wenzetu wa CUF ambao tuliamua
kwa pamoja kuianzisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa mujibu wa Katiba na
Sheria za Zanzibar, tuwaulize, kutoka hapa tulipofika tunakwenda wapi, hatima
ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa ikoje sasa, Wananchi wa Zanzibar wana hatima
gani ya nchi yao sasa, waulizeni maendeleo tuliyoyapata miaka mitano hatima
yake ikoje, tuwaache wananchi waamue na wananchi wataamua tarehe 25 Oktoba
mwaka huu, Wataamamua kuhusu hatima yao na maendeleo yao ya Zanzibar, watafanya
uchaguzi sahihi, watachagua viongozi wanaoweza kuongoza.
Waheshimiwa Wawakilishi mliobakia humu wa
Chama Cha Mapinduzi, nataka nikupongezeni sana sana, mmewawakilisha vizuri sana
wananchi wa Zanzibar, mmefanya kazi kubwa sana ya kuipitisha Bajeti,
mmeudhihirisha usemi wetu ‘zege halilali’. Mswaada wa Sheria wa Matumizi ya
Serikali kwa mwaka wa fedha 2015/2016 mmeupitisha kwa mafanikio makubwa na
mbwembwe kubwa sana, tutawahudumia wananchi wa Zanzibar bila ya matatizo.
Mhesimiwa
Spika,
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea
kuhakikisha kila mwananchi mwenye sifa ya kupiga kura anapewa haki yake hiyo. Nawanasihi sana na nawataka sana Wanasiasa
wasipotoshe wananchi juu ya haki hiyo.
Nawanasihi viongozi wote wa siasa waiache Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar
ifanye kazi yake ikiwa huru na isiingiliwe kwa namna yoyote ile. Ni wajibu wetu
sote kuheshimu sheria na kushirikiana na Tume ili kuhakikisha tunakuwa na
Uchaguzi ulio Huru na Haki. Jambo hilo nitahakikisha linatokea, na sio
vyenginevyo.
Kuanzia sasa macho ya ulimwengu
yanatuangalia. Tumefanya kazi na Jumuiya
ya Kimataifa, Mashirika mbali mbali duniani, nimetembea nchi mbali mbali
duniani, kote tunakokwenda na wale wanaokuja Zanzibar wanaipa sifa Zanzibar. Nasema
tusonge mbele kwa heshima na nia safi ya kuendeleza mafanikio yetu kama nilivyoyaeleza
muda mfupi uliopita.
MASUALA MENGINEYO:
AMANI NA USALAMA:
Mheshimiwa
Spika,
Siri kubwa ya mafanikio yetu katika sekta
zote za maendeleo nilizozielezea ni kuendelea kuimarika kwa hali ya amani na
utulivu nchini. Kwa nyakati mbali mbali
nimekuwa nikisisitiza umuhimu wa kusimamia amani na utulivu wa nchi yetu kwa
vile ni rasilimali ya msingi ambayo kila mwananchi anapaswa kuilinda
kuiendeleza na kuienzi kwa nguvu zake zote.
Katika hotuba yangu ya uzinduzi wa Baraza
hili la Nane la Wawakilishi nilisema, napenda ninukuu:
“Suala
la kudumisha amani si la Idara Maalum Na Vikosi vyetu vya Ulinzi Na Usalama
peke yake, lakini linashirikisha wananchi wote kwa jumla”
Nimefarajika na mafanikio makubwa tuliyoyafikia
katika kutekeleza wajibu wetu huo kwa vitendo.
Katika kipindi chote cha miaka mitano, Idara maalum za SMZ, Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
vimetekeleza vyema jukumu lao la kusimamia ulinzi, amani na utulivu kwa
kuhakikisha maisha ya watu na mali zao yamekuwa salama. Napenda nitumie fursa hii kuwapongeza sana
kwa utekelezaji mzuri wa dhamana zao hizo.
Mheshimiwa
Spika,
Hali ya amani na utulivu nchini imechangiwa
sana na wananchi walio wengi kutambua kuwa vitendo vinavyosababisha kuvunjika
kwa amani vina athari kubwa kwa maisha, uchumi na maendeleo ya ustawi wa jamii
yetu. Naamini kuwa wachache waliojaribu
kuichezea amani kwa visingizio mbali mbali hawakuwa wakifurahiwa na wananchi
wengine ila ni kwa sababu ya kukidhi malengo yao binafsi.
Napenda nisisitize kwamba kila mmoja wetu
atilie maanani kuwa utii wa sheria ni hatua muhimu katika kuhakikisha nchi yetu
inaendelea kuwa na amani, utulivu na kupata maendeleo zaidi. Kwa hivyo, ni jukumu la viongozi wote wa
Serikali, wanasiasa, viongozi wa madhehebu ya dini, viongozi wengine katika
jamii na wananchi wote kwa jumla kutekeleza wajibu wetu wa kuhakikisha
tunadumisha amani na utulivu na sheria zinafuatwa. Kutii Katiba ya Zanzibar na sheria zake si
jambo la hiari bali ni wajibu wetu sote na msingi muhimu wa kulinda amani na
utulivu wetu. Nataka nikuhakikishieni,
Waheshimiwa Wajumbe na niwahakikishie wananchi wote wa Zanzibar kwamba
nitaendelea kuisimamia amani na utulivu kwa nguvu zangu zote. Nitamchukulia hatua yeyote atakayejaribu
kuivunja amani ya Zanzibar.
MUUNGANO:
Mheshimiwa
Spika,
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya
Saba inatambua na inazingatia haja ya kuimarisha muungano wa Tanzania kama
nguzo ya pili muhimu baada ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964 kwa
malengo yale yale ya waasisi wetu, Marehemu Mzee Abeid Amani Karume na Marehemu
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Ni
dhahiri kuwa nguzo zetu hizi; Mapinduzi na Muungano ndizo zimetuwezesha kupiga
hatua kubwa za maendeleo yetu kisiasa, kiuchumi na kijamii na kuleta heshima ya
Wazanzibari na watanzania mbele ya mataifa mbali mbali katika kipindi cha miaka
51.
Katika kipindi hiki cha miaka mitano,
Muungano wetu umezidi kuimarika kutokana na hatua zinazochukuliwa na viongozi
wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania. Hatua hizo ni pamoja na
kuzifanyia kazi zile zinazotambuliwa kuwa ni kero za muungano. Masuala kadhaa yameshatatuliwa kupitia Kamati
inayoongozwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inawajumuisha
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar. Aidha, vikao vya kuimarisha
mashirikiano ya kisekta kati ya Wizara za Serikali ya Muungano wa Tanzania
vimeendelea kufanywa na kuratibiwa kupitia Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais.
Mheshimiwa
Spika,
Miongoni mwa mafanikio ya Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar ya Awamu ya Saba, ni mchango wa Serikali katika mchakato
wa kupata Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ulioasisiwa na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dk. Jakaya Mrisho Kikwete kwa lengo
la kuimarisha muungano wetu. Kwa mara nyengine, napenda nimpongeze Mheshimiwa Dk.
Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuanzisha mchakato wa Katiba mpya ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na kwa kushirikiana katika hatua zote na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar.
Sote tunatambua na tunathamini kazi nzuri
iliyofanywa na Waheshimiwa Wabunge wa Bunge la Katika la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kutupatia Katiba inayopendekezwa tuliyokabidhiwa mimi na Mhe. Dk.
Jakaya Mrisho Kikwete tarehe 08 Oktoba, 2014 katika Uwanja wa Jamhuri pale
Dodoma. Kazi iliyo mbele yetu wananchi
wote ni kushiriki katika Kura ya Maoni wakati utakapofika ili tuweze kunufaika
na mambo mengi ya msingi yaliyozingatiwa katika kuandaa Katiba inayopendekezwa.
USHIRIKIANO NA NCHI NYENGINE NA WAZANZIBARI
WANAOISHI NJE:
Mheshimiwa
Spika,
Zanzibar ikiwa ni sehemu ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania; imeendelea kushirikiana na nchi nyengine. Vile vile kitengo maalum kinachoratibu
masuala ya Wazanzibari wanaoishi nchi za nje, kimeanzishwa kwa kushirikiana na
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Maofisa wetu katika kipindi hiki wameshiriki
katika mikutano mbali mbali ya kikanda.
Wazanzibari wanaoishi nchi za nje wamekua wakitoa michango mbali mbali
ya fedha na kitaalamu hasa katika sekta ya elimu, afya, utalii, biashara na
uwekezaji. Vile vile, Ofisi ya Rais
Ikulu imeandaa utaratibu wa kukutana na Wana “Diaspora” kila mwaka kwa kualikwa
Ikulu kubadilishana mawazo pamoja na Rais.
Uhusiano wetu umezidi kuimarika kwa kupata
fursa ya kutembelewa na viongozi wa nchi kadhaa, taasisi za kimataifa, mabalozi
na kufanya ziara katika nchi mbali mbali mimi na viongozi wenzangu wakuu wa
Serikali. Kadhalika, kipindi hiki, cha
miaka mitano nilipata fursa ya kufanya ziara za kuzitembelea nchi kadhaa kwa
lengo la kuuimarisha uhusiano wetu.
Kadhalika, kwa nyakati tofauti nilikutana na
Mabalozi, Wawakilishi wa taasisi mbali mbali za Kimataifa na viongozi wa nchi
mbali mbali ambao walikuja kuonana nami na kufanya mazungumzo.
Katika mazungumzo yetu na viongozi hao
tuliweza kuimarisha uhusiano wetu katika nyanja mbali mbali za maendeleo
zikiwemo za kiuchumi na biashara, mazingira, elimu, na uimarishaji wa sekta ya
afya na utamaduni na sekta ya utalii.
Faida ya makubaliano yetu zimeanza kupatikana katika utekelezaji wa
mipango na miradi mbali mbali nchini.
MWISHO:
Baada ya maelezo yangu ya kina ya utendaji
na mafanikio ya Serikali ninayoiongoza tangu tarehe 3 Novemba, 2010 ambayo
imetekeleza asilimia 90 ya Ilani ya Chama tawala, Chama cha Mapinduzi ya mwaka
2010 – 2015, napenda kutoka shukurani zangu nyingi kwa Waheshimiwa Wajumbe kwa
kunisikiliza kwa makini. Safari yetu
bado haijafika mwisho na najua tumo katika matayarisho ya kuanza sehemu ya pili
ya Awamu hii.
Nachukua fursa hii kutoa shukurani kwenu
nyote kwa muda mlioutumikia kuzifanikisha shughuli za Baraza la Nane, kupitia
vikao vya Baraza na Kamati zake mbali mbali.
Sote tumetimiza wajibu wetu na tutaendelea kuwatumikia wananchi kila
tutakapopata fursa ya kuwatumikia.
Mheshimiwa
Spika,
Natoa shukurani za dhati kwa wasaidizi wangu
wakuu, Makamu wa Kwanza wa Rais; Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad na Makamu wa
Pili wa Rais; Mhe. Balozi Seif Ali Iddi kwa ushauri wao na kunisaidia katika
kuzifanikisha kazi za Serikali katika utekelezaji wa kazi zetu za kila siku.
Kadhalika, shukurani zangu ziende kwa Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri
wote, Makatibu Wakuu na Manaibu wao, Wakurugenzi, Watendaji na Watumishi wote
wa Serikali kwa ushirikiano walionipa na kwa kazi nzuri ya kuwatumikia
wananchi. Kadhalika, natoa shukurani maalum
kwa Wajumbe na Watendaji wa Mabaraza ya Miji na Halmashauri za Wilaya zote na
Wananchi kwa jumla kwa ushirikiano walioipa Serikali katika utekelezaji wa
mipango mbali mbali ya maendeleo.
Nathamini sana moyo wa uzalendo na kujituma
waliouonesha wananchi pamoja na kuendeleza hali ya amani na mshikamano. Jambo hili limepelekea kuwepo kwa
mashirikiano mazuri kwa Serikali na Wananchi katika kushughulikia masuala
muhimu ya maendeleo. Vile vile, kwa muda
wote Serikali yetu imepata sifa kubwa katika kusimamia amani, utulivu na
kuwaletea wananchi wake maendeleo. Sifa
nyingi na shukurani hizo ambazo hufikishwa kwangu na Viongozi, Mabalozi na
Washirika wetu wa Maendeleo ninaopata fursa ya kukutana nao ziwaendee wananchi
wa Zanzibar. Kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Wananchi wote
napenda Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza hili mzipokee shukurani hizo kwa mchango
wenu mkubwa na kwa kuunga mkono juhudi za Serikali za kutuletea maendeleo. Ahsanteni
Sana.
Nawatakia kheri wale Waheshimiwa ambao kwa
sababu mbali mbali hawatakuwemo katika Baraza lijalo baada ya Uchaguzi Mkuu wa
Oktoba 25, 2015. Wale wanaowania kurejea
pamoja na wengine ambao sasa si Wajumbe nawasihi wazingatie utunzaji wa amani
na utulivu katika harakati zao za uchaguzi.
Huu ni wakati wetu sote kudhihirisha ustaarabu katika siasa zetu, umoja
wetu, mshikamano na utiifu wa sheria.
Utunzaji wa amani ni dhamana yetu sote.
Kwa mara nyengine tena nasisitiza kwamba
Serikali zetu mbili na vyombo vyake vya sheria, ulinzi na usalama
havitomvumilia yeyote atakaehatarisha amani na kufanya fujo. Natoa wito kwa vijana wasishawishike kufanya
fujo kwa sababu yoyote ile.
Mheshimiwa
Spika,
Kwa mara nyengine tena natoa shukurani zangu
za dhati kwako Mhe. Pandu Ameir Kificho, Spika wa Baraza la Wawakilishi kwa
kuliongoza Baraza hili kwa busara, haki, uadilifu na ufanisi mkubwa. Umefanya kazi kubwa ya kuliendesha Baraza
hili kwa uadilifu mkubwa. Umetoa mchango
mkubwa katika kukuza demokrasia na Utawala Bora. Nakutakia kila la kheri katika maisha
yako.
Mheshimiwa
Spika,
Ili kutoa nafasi kwa matayarisho ya mwisho
kwa ajili ya uchaguzi mkuu ifikapo tarehe 25 Oktoba 2015, kwa madaraka niliyo
nayo kama ilivyoelezwa katika kifungu cha
91 (2) (a) cha Katiba ya Zanzibar ya
mwaka 1984, natamka kwamba kuanzia
Alkhamis tarehe 13 Agosti 2015 Baraza la Nane la Wawakilishi la Zanzibar
limevunjwa rasmi.
Nakutakieni
kila la kheri na Ramadhani njema
MUNGU
IBARIKI ZANZIBAR
MUNGU
IBARIKI TANZANIA
MUNGU
IBARIKI AFRIKA
Ahsanteni
kwa kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment