Mwashungi Tahir Maelezo
Katibu Mtendaji Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA) Mwanahija Haji Juma amesema kwamba jamii inahitaji kuhamasishwa kuthamini na kuenzi Utamaduni wa Zanzibar ili uweze kuimarika na kukua zaidi .
Hayo ameyasema leo huko katika Ukumbi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) Kampasi ya Vuga alipokuwa akifungua Kongamano la Tamasha la 20 la Utamaduni la Mzanzibari lililohudhuriwa na wanafunzi wa Vyuo Vikuu mbali mbali nchini.
Amesema Kongamano hilo ambalo ni mfululizo wa Tamasha la Zanzibar lililozinduliwa rasmi na Makamu wa Pili wa Rais tarehe 21 katika Ukumbi wa Salama Bwawani linasisitiza kuendelezwa, kuenziwa na kuthaminiwa na watu wote.
“Tamasha hili lilianzishwa nakuszinduliwa rasmi na Rais wa awamu ya tano Mh. Salmin Amour Juma mwaka 1994 katika Uwanja wa Amani,”alisema Katibu Mtendaji.
Aidha alisema lengo kuu la Tamasha hilo linalofanyika kila mwaka ni kulinda, kuenzi na kuwahamasisha wananchi kuelewa Utamaduni wao kwa undani zaidi kwani ni kioo cha wananchi.
Amesema Utamaduni ni mfumo wa maisha wa jamii husika na sio ngoma pekee kwani yapo mambo mengi katika utamaduni yakiwemo mavazi, vyakula , malezi , kusoma vitabu vya historia, kutunga mashairi na mengineo.
Nae Mkuu wa Idara ya Kiswahili wa SUZA Dkt. Maulid Omar amesema iko haja ya wananchi kufahamu changamoto zinazokabili Utamaduni wa Zanzibar kwani baadhi ya mambo yanaingizwa kuharibu utamaduni huo.
Mada mbili ziliwasilishwa na kujadiliwa katika Kongamano hilo ambazo ni athari za Utalii katika kuendeleza Utamaduni iliyotolewa na Bi. Mwanahamisi Hassan wa Idara ya sayansi jamii SUZA na mada ya pili iliyotolewa na Mhadhiri Msaidizi Omar Salum Mohd ilizungumzia mshikamano wa Utamaduni na Uislamu.
Kongamano hilo lilifungwa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili Bi. Mwanahija Haji Juma na kauli mbiu ya Tamasha la mwaka huu ni Utamaduni kwa Furaha, Amani na Utulivu
No comments:
Post a Comment