Habari za Punde

Siku ya wanaushirika duniani kusherehekewa leo

Na Rahma Khamis-Maelezo

Vyama vya Ushirika vimetajwa kuwa Sehemu muhimu ya kupata ajira na kujifunza mambo mbalimbali ikiwemo njia bora ya kuiongoza jamii.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Tawala  wa Wilaya ya Kusini Kibibi Mwinyi Hassan huko Kizimkazi  Mkunguni Mkoa wa Kusini wakati alopokuwa akizingumza na Wanaushirika wa kikundi  cha “Tufahamiane” ikiwa ni shamrashamra za kusheherekea siku ya wanaushirika Duniani ambapo kilele chake kinatarajiwa kufanyika hapo kesho.

Amesema Vyama hivyo hutoa elimu mbalimbali kwa wanachama wake ambapo Viongozi wa Vyama hivyo hujipatia uzoefu mkubwa wa kiuongozi unaowasaidia pale wanapopewa majukumu ya Kiserikali.

Katibu huyo amesema lengo la kuadhimisha siku hiyo ni kukumbuka  na kutathmini mchango mkubwa wa vyama  vya Ushirika  na kuunganisha nguvu  za wanaushirika  mbalimbali Duniani ambapo kauli mbiu ya mwaka  huu ni chagua ushirika upate usawa.

Ameelezea kuwa Vyama hivyo husaidia kwa kiasi kikubwa tatizo la ajira ambalo limekuwa kubwa na kwamba ni njia sahihi ya Vijana kuitumia kujiajiri badala ya kuitegemea serikali.

Katibu Kibibi ametoa wito kwa Wanajamii ambao bado hawajiunga na Vyama vya Ushirika kuitumia fursa hiyo ili iwasaidie katika kupambana na changamoto za maisha.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Ushirika wa TUFAHAMIANE Aziza Miraji Haji alielezea faida walizozipata katika kikundi chao kuwa ni pamoja na kugawana Pesa taslim baada ya kuuza bidhaa wanazozalisha ambazo huwaendeleza kiuchumi.

Faida nyingine ni pamoja na kumiliki Jengo la Ofisi, Gari sambamba na kugawana mavuno kwa mashirikiano makubwa ya Mbunge na  Mwakiklishi wa Jimbo la Makunduchi.

Ahmeid Ilias Haji ambae ni mmoja wa Wanaushirika huo alisema licha faida walizozipata, wanakabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa vifaa vya kujiendeleza kimafunzo kama vile kompyuta jambo ambalo linadumaza vipaji vyao walivyovipata kupitia ushirika huo.

Mwanachama huyo aliwataka vijana wenzake kuachana na Vigenge vya kihuni badala yake wajiunge na vikundi mbalimbali vya Ushirika vilivyopo nchini ili kuepuka tatizo la kutegemea ajira kutoka Serikalini.

Ushirika wa Tufahamiane uliopo Kizimkazi Mkunguni una jumla ya Wanachama 30 wakike na wakiume ambao wanajishughulisha na mambo mbalimbali ya kimaendeleo ikiwemo uatikaji wa miche ya minazi na kilimo cha mbogamboga za muhogo na viazi Vikuu.

Imetolewa na Maelezo Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.