STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Pemba 25.8.2015
RAIS wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein leo amelizindua Tawi
la Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA), Kampasi ya Benjamin William Mkapa,
Pemba na kueleza kuwa wananchi wa Pemba
watarajie kupata fursa ya kuchangia maendeleo yao na ya nchi kwa jumla
kwani uzinduzi huo ni hatua kubwa katika
maendeleo ya elimu hapa nchini.
Katika hotuba
yake aliyoitoa mara baada ya uzinduzi huo hapo katika viwanja vya Tawi hilo,
Dk. Shein alisema kuwa Chuo Kikuu ni Taasisi muhimu na taasisi kubwa katika
nchi yoyote duniani kutokana na majukumu
yake ya kuongeza kasi ya maendeleo katika jamii.
Dk. Shein alisema
kuwa kuna kila sababu ya kusherehekea uzinduzi huo kwani vijana wengi kutoka
Pemba walikuwa wakifuata elimu ya juu katika vyuo vilivyoko Unguja, Tanzania
Bara na nchi za nje.
"Leo siku ya
sikukuu kwa kufungua ukurasa mpya wa
maendeleo. Ni dhahiri kuwa tuna haki na wajibu wa kusherehekea kwamba
hatimae tumefikia hatua ya kuipata fursa ya masomo ya elimu ya juu katika Chuo
Kikuu cha Taifa hapa hapa Pemba",alisema Dk. Shein.
Aidha, Dk. Shein
alisema kuwa mbali ya kuwepo kwa mafunzo ya kitaaluma ya ngazi mbali mbali na
fani tafauti, chuo kikuu kina wajibu muhimu wa kufanya tafiti zenye lengo la
kutafuta ufumbuzi wa changamoto mbali mbali zinazoikabili jamii sambamba na
kutoa ushauri.
Alisema kuwa hatua hiyo ni lazima iongeze ari ya wazazi,
walezi na vijana katika skuli za Zanzibar sambamba na kuongeza jitihada katika
masomo ili kupata sifa za kujiunga na chuo hicho.
Alieleza kuwa
kuwepo kwa Tawi hilo la SUZA hapa Pemba ni sawa na mlango wa fursa pekee ambao
vijana na wananchi wengi kwa jumla wautumie huku akisisitiza kuwa kuongeza
idadi ya Kampasi za Chuo ni hatua ya maendeleo ambapo sasa SUZA itakuwa na
jumla ya Kamsasi 4 ambazo ni Kampasi ya Tunguu, Vuga, Nkruma na Kampasi ya
Benjamin Willium Mkapa.
Dk. Shein
alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa viongozi wa Chuo Kikuu cha SUZA kwa kazi
nzuri katika kutekeleza majukumu yao na kuanzisha kozi na mafunzo mbali mbali
kwa kuzingatia mahitaji ya soko la ajira na mipango ya maendeleo.
Pamoja na hayo,
Dk. Shein alisema kuwa ni jambo la faraja zaidi kuona kuwa asilimia kubwa ya
wanafunzi wanaojiunga na chuo hicho ni wanawake kwani ni hatua kubwa ya
mafanikio na utekelezaji wa lengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuona
kuwa watoto wa kike wanapata fursa ya juu.
Dk. Shein alitoa
wito kwa jumuiya ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kuyaendeleza
mafanikio yote yaliofikiwa na chuo hicho tangu kuasisiwa kwake miaka 14
iliyopita na kuutaka uongozi wa chuo hicho kuendeleza urafiki na mashirikiano
na wananchi wa Mchangamdogo pamoja na vijiji vya jirani ili wanufaike na fursa
mbali mbali zitokanazo na chuo hicho.
Sambamba na hayo,
alisisitiza haja kwa chuo kuongeza jitihada katika kufanya tafiti mbali mbali
za maendeleo ya jamii na wanachi kwa akushirikiana na Tume ya Sayansi na
Teknolojia Tanzania (COSTECH), taasisi mbali mbalizinazofanya tafiti pamoja na
kuimarisha mahusiano na vyuo vyengine vya ndani na nje ya Tanzania.
Dk. Shein katika
hotuba yake hiyo alisisitiza zana muhimu ya mabadiliko katika maendeleo huku
akiziangiza Wizara ya Elimu na Mfyunzo ya Amali pamoja na uongozi wa chuo hicho
kukaa pamoja ili kujadili suala la Skuli ya Sekondari ya Mchangamdogo ili iwe
skuli ya SUZA kwa Pemba na kuwa na wanafunzi wenye vipaji na hatimae kujiunga
na vyuo mbali mbali ndani na nje ya nchi.
Pia, aliiagiza
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Wizara ya Kilimo na Maliasili, Wizara ya
Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati kukaa pamoja ili kuangalia uwezekano wa kupatikana
nafasi katika eneo la Tawi hilo kwa kukaa na wananchi wa eneo hilo kuzzungumzia
suala hilo.
Nae, Waziri wa
Elimu na Mafunzo ya Amali Mhe. Ali Juma
Shamuhuna alitoa pongezi kwa Dk. Shein kwa kutimiza ahadi yake kwa vitendo aliyoitoa
ya kuanzisha Tawi la Chuo Kikuu cha SUZA katika Kampasi hiyo.
Nae, Makamu Mkuu
wa Chuo cha Taifa cha Zanzibar SUZA, Profesa Idrisa Ahmada Rai alisema kuwa
uchambuzi wa Kitaalamu unaonesha wazi kwamba Dk. Shein alipoingia madarakani
kuongoza Serikali ya Awamu ya Saba alikuwa na dhamira ya kuwaletea maendeleo
wananchi wa Zanzibar kwa kupitia mambo mawili makubwa yakiwemo kudumisha umoja
na amani pamoja na kuwataka Wazanzibari wabadilike.
Profesa Rai
alisema kuwa Kampasi hiyo itaanza kwa kuendeleza masomo ya Ualimu katika ngazi
ya Diploma ya Msingi yanayotolewa Chuoni hapo, na kuanzia mwaka huu wa Taaluma,
masomo ya Diploma ya Sayansi na Elimu ya miaka miwili na miaka mitatu
yatasomeshwa chuoni hapo.
Aidha, Tawi hilo
linaanza kutoa mafunzo ya utaalamu ya muda mfupi kwa taaluma mbali mbali kama
vile masomo ya matumizi ya teknolojia ya Tehama, mafunzo ya ujasiriamali,
mafunzo ya lugha za kigeni na mafunzo mengineyo.
Profesa Rais
alieleza kuwa lengo la SUZA, kwa kuzingatia dhamira ya Serikali ya kuanzishwa
kwa Chuo cha Ualimu cha Benjamin Willium Mkapa, ni kutanua mafunzo ya ualimu
katika Kampasi hiyo na hatua zitakazofuata ni kuhamasisha masomo yote ya
Diploma ya Ualimu yanayotolewa Unguja kwenye Kampasi hiyo ndani ya miaka
michache ijayo lakini pia, kuanza kutoa masomo katika ngazi ya Shahada ya
kwanza hadi PhD.
Mapema Katibu
Mkuu wa Wizara ya Elimu Khadija Bakari alisema kuwa kuwepo kwa Kampasi ya SUZA
Pemba, kutaongeza wanafunzi wanaojiunga na chuo katoka kisiwani humo na
kupunguza usumbufu wa kufuata mafunzo vyuo vya mbali huku akisisitiza kuwa
Wizara ya Elimu na Maafaunzo ya Amali itaendelea kuunga mkono juhudi za SUZA na
kuisaidia kufikia malengo iliyojiwekea.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024
2231822
E-mail:
rajabmkasaba@yahoo.co.uk
mwaka huu ndio mnakumbuka vitu vyote hivi kwani miaka yote hiyo mlikuwa hamuoni its late ,tutafanya wenyewe fungeni virago vyenu vyenu muondoke kwani hatuna shida nayo.
ReplyDelete