Habari za Punde

Wataalamu wa Kilimo washauriwa kutafuta vifaa mbadala vya kuchumia karafuu

STATE HOUSE ZANZIBAR

OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                            30 Agosti, 2015
---
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewataka wataalamu wa kilimo kutafuta mbadala wa vifaa vya asili vya kuchumia karafuu ili karafuu za Zanzibar ziendelee kuwa na ubora wake.

Akizungumza wakati alipokuwa akiangalia maonesho ya kilimo cha karafuu muda mfupi kabla ya kuzindua mfuko wa kuuendeleza zao hilo juzi, Dk. Shein alisema iko haja ya kutafuta mbadala wa vifaa hivyo kama vile pakacha ambazo ndio kifaa asili cha kuchumia karafuu zikiwa mtini.

“Hivi sasa watu wengi hawajui hata kusuka pakacha lakini ni ukweli kuwa hata minazi ya kukata makuti ya kutengeneza pakacha imekuwa ikipungua hivyo tunahitaji mbadala wake” alisema Dk. Shein.

Katika maelezo yake Afisa Misitu na Maliasili zisizorejesheka Badru Kombo Mwamvura alisema kuwa ili karafuu ziweze kukaa katika ubora wake kwa muda mrefu kabla ya kuchambuliwa matumizi ya pakacha ni jambo muhimu la kuzingatiwa.

Alibainisha kuwa pakacha zinaziweka karafuu zikiwa mbichi (bila kunyauka) kwa muda mrefu na kuwa rahisi kuzichambua kutoka kwenye vikonyo vyake tofauti ikiwa karafuu hizo zitakuwa zimewekwa kwenye vyombo vingine kama viroba au magunia ambapo hunyauka haraka na kuwa shida kuzichambua.

Katika maonesho hayo, Dk. Shein alishuhudia hatua mbalimbali za uimarishaji kilimo cha karafuu ikiwemo kazi za kitafiti kama vile aina ya udongo unaofaa katika kuotesha vitalu vya miti hiyo katika sehemu mbalimbali za kisiwa cha Pemba.


Aidha aliangalia njia bora za kushughulikia karafuu kuanzia wakati wa kuchuma hadi kuzikausha na kuzipelekea katika vituo vya manunuzi ili kupata daraja za juu na kuongeza thamani ya zao hilo.

Ilielezwa kuwa ili karafuu ziweze kuwa na ubora wake mkulima anapaswa kuzianika kwenye mikeka na majamvi na kuepuka kuzianika katika maeneo kama vile barabarani, juu ya bati au sehemu nyingine ambazo zinaweza kuharibu ubora wake.

Naye Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Biashara la Taifa (ZSTC) Bibi Mwanahija Almasi Ali akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Mfuko wa Kuendeleza Karafuu alieleza kuwa shirika lake limepata mafanikio makubwa katika kutekeleza majukumu yake hadi kufikia kutambuliwa kimataifa.

“Tumetunukiwa tuzo ya kimataifa iliyoambatana na cheti kutoka taasisi ya kimataifa ya Global Trade Leaders Club ya Hispania kutokana na utendaji wa shirika, utoaji wa bidhaa bora na huduma nzuri zinazotolewa na shirika”alieleza Bi Mwanahija.

Alisema shirika lake linajivunia maendeleo hayo na kutambua mchango mkubwa wa Mheshimiwa Rais katika kuhakikisha kuwa zao la karafuu linarejea katika nafasi yake ya uchumi wa Zanzibar na pia kuendelea kuwa nembo ya visiwa vya Unguja na Pemba.

Alizitaja kazi za Mfuko Maendeleo ya Karafuu kuwa ni pamoja na kutoa mikopo kwa wakulima wa zao hilo, kutoa fidia kwa wanaoanguka mikarafuu kupitia bima ya ajali na kusaidia upatikanaji wa vifaa vya uatikaji miche kwa vitalu binafsi na vya serikali ili kuongeza idadi ya miche ya mikarafuu.

Kazi nyingine alizitaja kuwa ni kutoa elimu kwa wakulima kuanzia uatikaji, upandaji na huduma za miche ya mikarafuu, kusaidia tafiti na utibabu wa mikarafuu pamoja na kusaidia miradi ya maendeleo ya miundombinu katika mashamba ya maeneo ya mikarafuu.

Katika hafla hiyo ya uzinduzi iliyofanyika katika viwanja vya kiwanda cha makonyo Wawi Chake Chake Pemba, Mkurugenzi huyo mwendeshaji wa ZSTC alieleza kuwa kuongezeka kwa mapato ya wakulima wa karafuu katika misimu mine iliyopita kumebadili kwa kiwango kikubwa maishaya wakulima wa zao hilo hivyo kukutekeleza azma ya serikali ya kupunguza umasikini.

Alifafanua kuwa kuimarika na kukua kwa sekta ya kilimo cha zao la karafuu kumesaidia kuongeza ajira, ustawi wa wananchi na kutoa matumaini mazuri kwa Serikali.

Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 
  E-mail: saidameir@ikuluzanzibar.go.tz

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.