Habari za Punde

Wito: Iandikeni historia ya Pemba ili isipotee

Na Haji Nassor, Pemba

WASOMI na watafiti nchini, wameshauriwa kufanya tafiti zenye lengo la kuandika vitabu vya historia ya Kisiwa cha Pemba, kwa lengo la kukuza upatikanaji wa historia hiyo, ambayo imetajwa kuanza kupotea taratibu.
Wito huo umetolewa na Kaimu Mkuu wa Idara ya Mambo ya Kale kisiwani humo Salim Seif, wakati alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi mjini Chaka Chake, juu ukosefu wa waandishi wa vitabu vya historia ya Pemba.
Alisema kisiwa cha Pemba, kinahistori kubwa ya watawala wa kigeni wakiwemo washirazi na warabu, ilioanzia tokea karne ya tisa, sawa na miaka 1200 iliopita, ambapo hakuna waandishi wazalendo walioandika historia ya kisiwa hicho, karibu miaka 50 sasa.
Alieleza kuwa mtafiti wa mwisho kufanya utafiti na kuandika kitabu ni raia kutoka Uengereza alietambulika kwa jina la John Kick, katika mwaka 1966, ambapo baadae utafiti mwengine usioambatana na kuandikwa kitabu ulifanya miaka 12 iliopita.
Kaimu huyo Mkuu wa Idara ya Mambo ya Kale Pemba, Salum Seif, alisema utafiti ambao haukuandikiwa kitabu ni ule uliofanywa mwaka 2003, ambapo hadi mwaka huu 2015, hakuna mtafiti mwengine alifika kisiwani humo.

“Kwa kweli kuna ufinyu wa wasomi na watafiti wetu kufanya tafiti kwa lengo la kuandika vitabu, ambapo kama vikiwempo naamini vitawasaidia wananchi walau kusoma na kuelewa’’,alielezea.
Hata hivyo alisema kitabu hicho ambacho kimeandikwa na Muengereza  huyo mwaka 1966, kipo makao makuu ya Mambo ya Kale Unguja, na kuongeza kuwa, lazima wasomi wazalengo waone umuhimu wa kuandika vitabu.
Katika hatua nyengine ameitaka jamii, kujenge utamaduni wa kutembelea maeneo ya kishistoria, hasa yaliokaribu nao, ili kuelewa kwa kina historia za watalawa waliopita hapa Zanzibar.

Kisiwa cha Pemba kina maeneo yanayozidi 44 ya kihistoria ambayo mengine tokea karne ya tisa, 14, 15 na hata 18, ambapo wilaya ya Chake chake, ina maeneo 10, wilaya za Mkoani na Wete13, wakati wilaya ya Micheweni 12, likiwemo la msikiti wa Mkiang’ombe uliojengwa karne ya 13 sawa na miaka 800 sasa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.