Habari za Punde

Hotuba ya Dk Shein katika Baraza la Idd leo

HOTUBA YA RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI, MHE. AL-HAJJ DK. ALI MOHAMED SHEIN, KATIKA
BARAZA LA IDD- EL-HAJJ: 24 SEPTEMBA, 2015
SAWA NA MWEZI 10 MFUNGUO TATU, 1436 HIJRIA


BISMILLAH RAHMAN RAHIM

Naanza kwa kushuhudia kuwa hapana Mola anayestahiki kuabudiwa kwa haki na viumbe vyote isipokuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu Subhana Wataala.  Yeye ndiye Muumba wa Dunia na Akhera na kwake Yeye ndiyo marejeo ya viumbe vyote.  Tunakiri kwa kauli na kuitakidi kwa moyo kuwa Mtume Muhammad (S.A.W) ni Mtume wake wa haki na kigezo chema cha uchamungu kwa waumini sote.

Rehema na amani ya Mwenyezi Mungu zimshukie Mtukufu wa daraja na mbora wa viumbe; Sayyidna Muhammad (S.A.W), Aali na Sahaba zake pamoja na waumini wote waliofuata njia yake ya uongofu hadi siku ya kiama.  Tumuombe Mola wetu (SW) atujaalie na sisi tulio hai, ndugu, jamaa na wale wote waliokwishatangulia mbele ya haki tuwe miongoni mwao.  Atupe ubainifu wa kuyafanya mambo ya kheri  na tuyaepuke mambo ya shari na maovu, ili tuweze kufanikiwa hapa Duniani na huko Akhera tuendako.  Amin!

Mheshimiwa Sheikh Khamis Haji Khamis;
Kadhi Mkuu wa Zanzibar.

Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad;
Makamu wa Kwanza wa Rais,

Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi;
Makamu wa Pili wa Rais,


Mheshimiwa Dk. Amani Abeid Karume,
Rais Mstaafu wa Zanzibar;

Mheshimiwa Pandu Ameir Kificho;
Spika wa Baraza la Wawakilishi,

Mheshimiwa Omar Othman Makungu;
Jaji Mkuu wa Zanzibar,

Waheshimiwa Mawaziri,

Waheshimiwa Mabalozi,

Wageni Waalikwa,

Ndugu Wananchi,

Mabibi na Mabwana,


Assalamu Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh

IDDI MUBARAK

Ndugu Wananchi,
Nimeanza hotuba yangu kwa kumtukuza Mola wetu (SW) na kukiri kuwa Bwana Mtume Muhammad (S.A.W) ni Mtume wa haki wa Mwenyezi Mungu ambaye ni wajibu wetu kumsalia, kuyazingatia na kuyafuata mafundisho yake ili tuweze kufanikiwa katika kuyatekeleza maamrisho ya Mwenyezi Mungu na tujiepushe na yale yote tunayokatazwa kuyafanya.

Kupitia mafundisho ya Mtume (S.A.W) kutoka kwa Mwenyezi Mungu, tumetakiwa tuitekeleze ibada ya Hijja kwa kila mwenye uwezo katika nyumba tukufu iliyopo Makka huko Saud Arabia.  Mwenyezi Mungu katika aya ya 97 ya Surat Aali Imran anatufahamisha uzito na umuhimu wa kuitekeleza ibada ya Hijja kwa kusema:
“Na kwa ajili ya Mwenyezi Mungu imewawajibikia watu wafanye Hijja katika nyumba hiyo, kwa yule awezaye kwenda huko.  Na atakayekufuru (atakayekanusha) basi Mwenyezi Mungu si muhitaji kuwahitaji walimwengu”.

Ndugu Wananchi,
Leo tunaungana katika furaha ya sikukuu ya Idd el Hajj na waislamu wenzetu kwa maelfu kutoka mataifa mbali mbali, wa rangi na hadhi mbali mbali walioitikia wito wa Mola wetu kwenda kuitekeleza Ibada ya Hijja katika mji Mtukufu wa Makka.  Kwa hakika, hii ni neema kubwa kwetu kwani wapo wenzetu wengi miongoni mwetu ambao hawakuweza kuifikia siku hii.  Kwa hivyo, ni wajibu wetu kumshukuru Mola wetu kwa kuturuzuku neema hii ya kuifikia siku hii,  ambapo ni miezi michache tu iliyopita, tulijaaliwa kuisherehekea sikukuu ya Idd-el-Fitri kwa amani na salama.  Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaaliya siku hizi za furaha na kuwa pamoja katika kuzisherehekea.


Ndugu Wananchi,
Ni jambo la kutia moyo na kumshukuru Mwenyezi Mungu kuona kwamba idadi ya mahujaji wa Zanzibar imekuwa ikiongezeka kila mwaka. Katika mwaka huu wa 2015, taasisi zinazosafirisha mahujaji hapa Zanzibar kutokana na uongozi bora na uzoefu wa kuzifanya shughuli za Hijja za Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana zimeweza kusafirisha mahujaji 1,502, kati ya mahujaji 3,000 waliosafirishwa kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.  Idadi hii ni ziada ya mahujaji 222 ikilinganishwa na idadi ya mwaka jana ambapo taasisi za Zanzibar zilisafirisha mahujaji 1,280 kati ya 2,500 kwa Tanzania nzima.  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imewekewa fursa ya kupeleka katika Hijja,  mahujaji 25,000 kwa mujibu wa makubaliano ya OIC.  Ni dhahiri kuwa idadi ya mahujaji wetu kwa sasa ni ndogo ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika ya Mashariki.  Aidha, imebainika kuwa mahujaji wetu wengi wanaokwenda Hijja ni watu wa hali za kati na hali za chini kiuchumi. Wengi wao huifanya ibada hii baada ya kupata fedha zao za kiinua mgongo.

Kwa lengo la kuwasaidia wananchi wengi zaidi waweze kupata fursa ya kuitekeleza ibada ya Hijja kwa wepesi na mapema zaidi, tayari Serikali imeanza kazi ya kufanya upembuzi yakinifu ili kuanzisha Mfuko wa Hijja Zanzibar. Mfuko huo utakapoanzishwa, watu wengi zaidi watapata nafasi na uwezo wa kuweka fedha kidogo kidogo kwa mujibu wa uwezo wao. Hatimae, watamudu kutekeleza ibada za Hijja na Umra kwa mujibu wa makubaliano na taratibu zitakazowekwa na mfuko.  Nchi nyingi ambazo zimeanzisha mifuko ya aina hii ikiwemo Malaysia, wanamudu kumaliza idadi yote ya nafasi za mahujaji walizowekewa.

Bila ya shaka, kwa kupitia utaratibu wa mfuko huu, mahujaji wetu watapata uwezo wa kufanya maandalizi mazuri ya misafara ya Hijja. Kadhalika, kwa miezi yote Waumini wengi watapata nafasi ya kwenda kutekeleza ibada za Umra na ziara.  Mifuko hii pamoja na kuwawezesha Waislamu kuhiji husaidia sana shughuli za kidini na kijamii.  Tayari Kamisheni ya Wakfu ya Mali ya Amana kwa kushirikiana na Benki ya Kiislamu ya PBZ, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (ZSSF), Shirika la Bima la Zanzibar (ZIC), Umoja wa Taasisi za Hijja Zanzibar na wataalamu wa Uchumi na Utawala kutoka taasisi za kiislamu wanalifanyia kazi suala hili na  matarajio ni kuanza kufanya kazi kabla ya Hijja ijayo. Tumuombe Mwenyezi Mungu atufanyie wepesi katika kulitekeleza jambo hili la kheri.

Ndugu Wananchi,
Ibada ya Hijja waliyoitekeleza ndugu zetu mahujaji huko Makka ina mchango muhimu wa kukuza imani ya mja na uchamungu wake kutokana na mafunzo muhimu yanayotokana na ibada hiyo yenye historia ndefu tangu kwa baba wa Mitume Nabii Ibrahim (AS).

Miongoni mwa mafunzo muhimu ya ibada ya Hijja ni kudhihirika kwa umoja wa Waislamu duniani ambao wanakutanika katika Mji wa Makka kwa kuitikia wito wa Mwenyezi Mungu. Umoja wa waislamu umebainishwa katika aya mbali mbali za Kurani ambapo katika aya 92 ya Surat Al-Anbiyaa, Mwenyezi Mungu ametuthibitishia hilo na kututaka tumuabudu Yeye kwa kusema,
“Hakika umma wenu huu ni umma mmoja tu, na mimi ni Mola wenu, basi niabuduni”.

Hali hii ya umoja, tunapaswa tuione umuhimu wake na tuiendeleze katika maisha yetu ya kila siku hasa sisi tunaoishi katika nchi moja na watu wa nasabu moja.  Sote tuna wajibu wa kuimarisha umoja wetu na kuepukana na masuala yote yanayohatarisha umoja na mshikamano wetu kwa lengo la kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu na kupiga hatua kubwa zaidi za maendeleo.

Ndugu Wananchi,
Jambo jengine muhimu linalotokea katika kipindi cha ibada ya Hijja ni Waislamu kutoka sehemu mbali mbali duniani kupata fursa ya kukutana na kujadili masuala yanayohusu maendeleo ya jamii ya kiislamu katika nyanja za kisiasa, kiuchumi na ustawi wa jamii.  Katika hali kama hii, masuala mengi ya msingi huzungumzwa na Waislamu wenye taaluma, maarifa, uzoefu na kubadilishana mawazo kwa njia ya majadiliano na kupata njia za kukabiliana na changamoto za maendeleo zilizopo.  Fatwa zinazotolewa miongoni mwa maulamaa wa kiislamu, huwa ni dira muhimu katika kuleta ustawi wa jamii zetu.

Hili nalo ni jambo la kuliendeleza katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto mbali mbali zilizomo katika jamii yetu.  Majadiliano ni njia nzuri na ya pekee katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto zetu za maendeleo ndani ya jamii yetu.  Ni wazi kwamba, jamii haiwezi kupata maendeleo kama watu watakosa kushirikiana na kuaminiana.  Kwa hivyo, kwa kutumia maarifa yanayotokana na mafunzo ya Ibada ya Hijja ni miongoni mwa faida tunazozipata katika utekelezaji wa Ibada hii na ni wajibu wetu tuyatumie mafunzo hayo katika maisha yetu ya kila siku.

Ndugu Wananchi,
Vile vile, katika ibada ya Hijja  tunajifunza umuhimu wa mahujaji kuwa  na subira na kwa wale tunaobaki nasi huwa tunawasubiri ndugu, jamaa na marafiki zetu waliokwenda kuitekeleza ibada hii kwa lengo la kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu.  Ibada ya Hijja inajumuisha taratibu nyingi pamoja na ugumu wa safari, gharama na haja ya kuwa na uzima wa afya na ustahamilivu.  Yote haya yanahitaji kuwa na subira ambayo ni sifa muhimu ya Mitume yote na Masahaba.  Kwa wale wanaoondokewa na ndugu na jamaa zao kwa ajili ya kwenda kuitikia wito huo wa Mwenyezi Mungu nao hulazimika kuwa na subira.

Kuwa na subira ni jambo lililosisitizwa sana katika Kurani na Sunnah kupitia visa vya Mitume wa Mwenyezi Mungu na Masahaba ili iwe ni mafunzo kwetu.  Katika kusisitiza faida ya kuwa na subira kwa muumini, Bwana Mtume (S.A.W) katika hadithi iliyopokelewa na Al-Bukhaariy na Ahmad amesema:
“Kubakia katika subira kwa siku moja katika njia ya Mwenyezi Mungu ni bora zaidi kuliko dunia na vyote vilivyomo ndani yake”

Ni dhahiri kuwa kuna fadhila kubwa katika kusubiri kwa siku hizi ambazo wenzetu wanatekeleza ibada ya Hijja huko Makka na sisi tunaowasubiri tukiwaombea dua ili ibada zao zikubaliwe.  Aidha, masheikh wetu wanatuelekeza kuwa subira yenye malipo zaidi ni ile ya kusubiri kwa kujizuwia kutekeleza mambo mabaya kwa kutegemea malipo mema kutoka kwa Mola wetu Subhana Wataala.  Tumuombe Mwenyezi Mungu atupe subira kwa kutegemea fadhila na kufuata maamrisho ya Mola wetu.

Ndugu Wananchi,
Miongoni mwa masuala muhimu tuliyosuniwa katika sikukuu hii ya Idd el Hajj ni kuchinja mnyama.  Uchinjaji huu unatupa funzo la utiifu wa Nabii Ibrahim (AS) na kutawakali kwake pamoja na mwanawe Ismail (AS) katika kutekeleza amri ya Allah kupitia ndoto aliyooteshwa.  Utiifu wao wa kweli kwa Mwenyezi Mungu uliwawezesha kufuzu, jambo ambalo la mazingatio kwetu sote na kujifunza ili tuweze kufanikiwa katika masuala yetu mbali mbali ya kimaisha.

Mafundisho ya uislamu yanasisitiza umuhimu wa kuitekeleza suna hii ambayo ni ibada na hatua ya kumkurubisha mja na Mola wake.  Siku hii ya leo imesuniwa kuchinja mnyama baada ya sala ya Idd na kutumia sehemu ya nyama na nyengine kuwapa marafiki na wahitaji wengine waliokuwa hawana uwezo katika jamii.

Ni wajibu wetu kuyaendeleza mambo kama haya ya kheri na uchamungu ili iwe ni sababu ya kukuza mapenzi mema baina yetu na kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu kwa kufanya anayoyaridhia na kujiepusha na makatazo yake.  Kadhalika, tuendelee kuyatumia mafunzo yanayotokana na ibada zetu kwa vitendo ili iwe ndiyo dira ya kuleta ufanisi katika maisha yetu ya kila siku. 

Ndugu Wananchi,
Tuna wajibu mkubwa wa kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kutuwezesha kuungana na waislamu wenzetu duniani katika kuisherehekea sikukuu hii ya Idd el Hajj katika hali ya amani na salama.  Nimepata faraja kubwa kuweza kushirikiana na waislamu wenzetu wa Mkoa huu wa Kaskazini Unguja kwa kusali pamoja sala ya Iddi leo asubuhi katika kiwanja cha mpira cha Polisi Mkokotoni na hivi sasa kwa pamoja tumejumuika katika kituo hiki cha Mafunzo ya Amali kwa ajili ya Baraza la Iddi.

Natoa shukurani zangu na naipongeza Kamati ya Maandalizi kwa kushirikiana vyema na uongozi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja pamoja na Wilaya zake katika kuifanikisha shughuli hii.  Kadhalika, nawapongeza kwa dhati wananchi wote wa Mkoa huu kwa kujitokeza kwa wingi katika sala ya Idd na kwa mashirikiano yenu mnayoendelea kutupa. Tumuombe Mwenyezi Mungu azidishe ushirikiano huu katika kuifanikisha mipango yetu ya maendeleo na kuimarisha ustawi wa wananchi wote.

Ndugu Wananchi,
Nimefarajika na hatua kubwa ya maendeleo tuliyoyafikia katika Mkoa huu wa Kaskazini Unguja katika sekta za kiuchumi, huduma za jamii na muamko wa wananchi katika kuzitumia fursa mbali mbali za kujiendeleza kiuchumi kwa kushirikiana na Serikali.  Napenda nikupongezeni sana kwa mafanikio hayo.

Katika kuhakikisha kuwa, Mikoa yetu inazidi kuimarika kiuchumi, kuongeza fursa za ajira hasa kwa vijana na kuimarisha upatikanaji mzuri wa huduma za jamii, Serikali imeazimia kujenga mji wa kisasa katika Mkoa huu wa Kaskazini kwenye vijiji vya Kijini na Matemwe.  Ujenzi wa barabara wenye urefu wa kilomita 20.2 kutoka Matemwe kupitia Kijini hadi Kidoti umekwishaanza. Wananchi wa Mkoa huu wananufaika na kuwepo kwa idadi kubwa ya hoteli za kitalii kwa kuzingatia kauli mbiu ya utalii kwa wote.

Ndugu Wananchi,
Inatia moyo kuona vijana na kinamama wa Mkoa huu walivyojidhatiti kujiendeleza kiuchumi kwa kutengeneza bidhaa mbali mbali na kuzalisha mazao kwa ajili ya kuuza katika Hoteli za kitalii.  Aidha, wananchi wengi wa maeneo ya Bumbwini, Mkokotoni, Bwekunduni, Fungurefu na vijiji nyengine vya Mkoa huu wameimarisha uchumi wao kwa kujishughulisha na biashara ya madagaa ambayo nimearifiwa kuwa husafirishwa hadi Kongo na nchi nyengine za jirani.

Wito wangu kwenu ni kuwa muendelee kushirikiana na Serikali yenu katika kuziimarisha shughuli zetu hizi ili ziweze kutoa tija zaidi.  Kadhalika, vijana wanaokosa fursa ya kuendelea na masomo wakitumie kituo cha Mafunzo ya Amali cha Mkokotoni ili wajiendeleze kupata ujuzi wa kazi mbali mbali za amali unaotolewa na kituo hicho.  Kazi hizo ni pamoja na useremala, ushoni, uchoraji, uwashi, ufundi bomba, magari, mafriji, mapishi ya aina mbali mbali na huduma za mahoteli.  Vile vile, katika mwezi wa Agosti, 2015 tulifungua kituo cha ujasiriamali “Bare-foot College” kama kiliopo huko India, kituo kinachotengeneza vifaa vya umeme wa jua ndani ya Mkoa huu ambacho ni cha aina yake na maalum kwa kinamama.  Hizo ni fursa ambazo mnapaswa kuzitumia vyema katika kupiga hatua zaidi za maendeleo.

Ndugu Wananchi,
Serikali kwa kushirikiana na washirika wetu wa maendeleo pamoja na ushirikiano wa wananchi tumeweza kupiga hatua kubwa katika kuimarisha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika Mkoa huu kwa kutekeleza miradi mbali mbali.  Hali ya upatikanaji wa maji safi katika Mkoa huu imefikia asilimia 71.68.  Mafanikio hayo yamefikiwa baada ya kutekeleza miradi mikuu mitatu ya maji safi na salama katika Mkoa huu.  Miradi hiyo ni mradi wa Serikali kupitia Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA), Mradi wa Maji wa Ras-al-Khaimah na Mradi wa Maji wa ADB ambayo kwa pamoja imewanufaisha wananchi mbali mbali wa Mkoa huu kupata huduma za maji safi na salama.   

Kadhalika, Serikali imeimarisha huduma za hospitali ya Koteji ya Kivunge pamoja na vituo vya afya vyengine katika Mkoa huo ili kuziimarisha afya za wananchi.  Wajibu wa wananchi ni kuzitumia huduma hizi pamoja na wazazi na walezi kuhakikisha watoto wetu wanapelekwa kupata chanjo ili kuwakinga na maradhi mbali mbali na kinamama wajawazito wawe wanajifungulia hospitali katika azma ya kuziimarisha afya zao.

Ndugu Wananchi,
Pamoja na mafanikio hayo katika kuziimarisha huduma za jamii, napenda nitumie fursa hii, kuutaka uongozi wa Mkoa wa Kaskazini; Unguja kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi pamoja na taasisi zinazowasimamia madereva wachukue hatua madhubuti katika kukabiliana na tatizo la ajali za barabarani katika Mkoa huu. Taarifa kutoka Jeshi la Polisi zinabainisha kazi kubwa tuliyo nayo katika kukabiliana na tatizo la ajali za barabarani.  Kwa mujibu wa taarifa hiyo, katika kipindi cha kuanzia mwezi wa Januari hadi Agosti mwaka 2014, jumla ya ajali za barabarani 391 zimetokea Unguja na Pemba.  Ajali hizo zilizosababisha vifo vya watu 104 na watu 728 wamejeruhiwa.  Katika Mkoa huu wa Kaskazini Unguja zilitokea ajali 64 zilizosababisha vifo vya watu 16 na jumla ya watu 259 walijeruhiwa.

Katika mwaka huu wa 2015 kwenye kipindi kama hicho, tayari zimetokea ajali za barabarani 393 Unguja na Pemba ikiwa ni ziada ya ajali mbili ikilinganishwa na mwaka 2014.  Ajali hizo zimesababisha vifo vya watu 91 na watu 450 wamejeruhiwa.  Katika kipindi hiki kwenye Mkoa huu, kumetokea ajali za barabarani 73, zilizosababisha vifo vya watu 15 na kuwajeruhi watu 123.  Ni wazi kuwa takwimu hizo si za kufurahisha, kwa hivyo jitihada za pamoja zinahitajika ili kupunguza na hatimae kuliondoa kabisa tatizo la ajali za barabarani kwa vile asilimia kubwa ya ajali hizi zinasababishwa kwa kutokuzingatiwa kwa sheria za usalama barabarani na matumizi mazuri ya barabara zetu.

Ndugu Wananchi,  
Kwa mara nyengine napenda nikumbushe umuhimu wa sisi viongozi wa kisiasa, kijamii na wa madhehebu ya dini kuwasisitiza wafuasi wetu umuhimu wa kuilinda amani na kujiepusha na vitendo vyote vinavyoweza kutuondolea amani na utulivu tuliokuwa nao.  Nimekuwa nikisema mara kadhaa kuwa amani haina mbadala.  Bila ya amani hatuwezi kupata maendeleo yoyote.  Kutokuwepo kwa amani kunahatarisha uhai wa watu na ni sababu ya kuharibu miundombinu ya aina mbali mbali na kuzua fadhaa katika jamii.  Ni dhahiri kuwa kutoweka kwa amani huwaondolea wasaa hata waumini katika kutekeleza ibada za kumuwabudu Mola wao.  Katika aya ya 112 ya Suratun Nahl, Mwenyezi Mungu anatutanabahisha kwa kutupa mfano wa waliopewa neema ya amani na utulivu wakashindwa kuitunza kwa kusema:
“Na Mwenyezi Mungu anakupeni mfano wa mji uliokuwa na amani na utulivu, riziki yake ikiujia kwa wingi kutoka kila mahali.  Lakini ukazikufuru neema za Mwenyezi Mungu, kwa hivyo Mwenyezi Mungu akauvika vazi la njaa na khofu kwa sababu ya yale waliyokuwa wakiyafanya”.
Tumuombe Mwenyezi Mungu atuepushe na mtihani huo.

Napenda nikuhakikishieni kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zitaendelea  kukabiliana na wale wote watakaofanya vitendo vinavyoashiria kutaka kuvunja amani ya nchi yetu wakati wote na katika kipindi hiki cha Kampeni za Uchaguzi Mkuu, wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi.  Hakuna atakayeonewa au kudhulumiwa kwa njia yoyote ile lakini Serikali ina wajibu wa kikatiba wa kuwalinda watu wote na mali zao pamoja na wageni wanaoitembelea nchi yetu.

Ndugu Wananchi,
Hivi sasa tumo katika kusherehekea sikukuu, lakini kama tunavyofahamu baada ya siku chache zijazo tunatarajia kuanza kupata baraka za mvua za Vuli.  Mvua ni neema kubwa kwetu hasa kwa kuendeleza shughuli za kilimo na upatikanaji wa maji nchini. Kwa hivyo, ni vyema tukaanza maandalizi ya kilimo cha mazao na matunda mbali mbali yanayostawi na kunawiri katika msimu wa Vuli.

Kwa upande mwengine, ni muhimu tukazingatia kwamba baadhi ya nyakati, Mwenyezi Mungu hutupa neema ya mvua ambayo vile vile huwa na mitihani ili kuzipima nafsi zetu. Mwenyezi Mungu ametuambia katika Surat Muhammad aya ya 31 kwamba:
“Nitakufanyieni mitihani mpaka muwadhihirishe (wajulikane) wale wanaopigania dini miongoni mwenu, na wanaosubiri nasi tutadhihirisha habari zenu”.

Sote tunakumbuka jinsi baadhi ya wananchi wenzetu walivyopata mitihani ya mafuriko katika sehemu mbali mbali za Unguja na Pemba katika msimu wa mvua za Masika uliopita. Tulishuhudia matukio mengi ya kusikitisha katika maeneo ya Kwahani, Mwanakwerekwe, Tomondo na kadhalika, katika mwezi Mei, 2015.  Mimi na viongozi wengine tulipata fursa ya kuwatembelea wananchi waliopata maafa kwa ajili ya kuwafariji.

Napenda niwakumbushe wananchi kwamba katika nyakati mbali mbali, Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini “Tanzania Meteorological Agency (TMA)”, imetahadharisha kwamba katika msimu wa mvua za Vuli, upo uwezekano mkubwa wa kutokea mvua kubwa za “El-Nino” kutokana na hali ya sasa ya kuongezeka kwa joto katika Bahari ya Pasifiki. Ongezeko hilo la joto katika bahari hiyo kama litaendelea kuwepo, linaweza kuenea hadi katika Bahari ya Hindi na kusababisha mvua kubwa za “El-Nino” katika ukanda wote unaopakana na bahari ya Hindi.

Kwa kawaida mvua kubwa za “El-Nino” zinapolikumba eneo la nchi husababisha mafuriko na kuacha madhara makubwa ya uharibifu wa miundombinu na mali za wananchi; hasa nyumba zilizojengwa katika maeneo ya mabondeni.  Wataalamu wetu wanatufahamisha kwamba kuna viasharia vingi sana vya kuonesha uwezekano wa mvua za “El Nino” kutokea mwaka huu katika Ukanda wa Afrika Mashariki.

Huu ni utabiri wa binaadamu lakini Mwenyezi Mungu ana kudra na shani yake. Utabiri huu unatokana na elimu na maarifa aliyotupa Subhana Wata’ala, ili kurahisisha maisha yetu. Ni vyema tukaitumia elimu hii vizuri kwa kuanza kuchukua tahadhari zinazofaa. Nasaha zangu kwenu wananchi ni kwamba tuzingatie hekima ya ule usemi maarufu kwamba, “Tahadhari kabla ya athari”.  Kwa hivyo, taasisi zinazoshugulikia usafi wa miji ziongeze kasi katika kusafisha misingi ya maji machafu na njia za maji, usafi wa mazingira yetu ili kuepukana na maradhi.  Ninawanasihi wananchi tuache ujenzi katika sehemu za mabonde na sote tuwe na moyo wa kusaidiana wakati wote, hasa pale Mwenyezi Mungu anapotupa mitihani mbali mbali.

Ndugu Wananchi,
Kwa baraka ya siku hii, tuwaombee mafanikio vijana wetu wa darasa la sita, la saba na Kidato cha Pili waliofanya mitihani yao hivi karibuni na Mwenyezi Mungu awape matayarisho mema vijana wetu wanaojiandaa na mitihani ya Taifa Kidatu cha Nne. Awajaalie wote wafaulu katika mitihani yao.  Awape wagonjwa wetu wote shifaa ya maradhi yao na aijaalie nchi yetu amani, upendo na masikilizano na mapenzi zaidi baina yetu.

Namalizia hotuba yangu kwa kukuombeeni nyote kila la kheri katika kuisherehekea sikukuu hii ya Idd-el-Hajj.  Tuisherehekee sikukuu hii kwa mambo ya kheri na kujiepusha na yale yote yanayomchukiza Mwenyezi Mungu.  Tumuombe Mwenyezi Mungu azikubali ibada za mahujaji wetu wote.  Tunapowasiliana nao tuwaombe waiombee nchi yetu iendelee kuwa ya amani na utulivu. Mwenyezi Mungu awape uwezo wale wote wenye azma ya kuitekeleza ibada ya Hijja waweze kufanya hivyo kama walivyokusudia na kupata fursa ya kuishi japo kwa siku chache katika miji mitukufu ya Makka na Madina Yarabbil Allamina 

Mwenyezi Mungu awarehemu wazee wetu, ndugu, jamaa na marafiki zetu wote waliotangulia mbele ya haki. Aijaze neema na baraka nchi yetu. Atupe uwezo na wepesi wa kuitekeleza mipango yetu ya maendeleo kama tulivyoipanga.  Atujaalie afya njema na riziki za halali. Mwenyezi Mungu atujaalie sote turudi nyumbani kwa salama na amani.

Ahsanteni kwa kunisikiliza.

IDD MUBARAK

KULLU AAM WAANTUM BIKHEIR


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.