Habari za Punde

Hubirini AmaniI, Usalama, Demokrasia na Maendeleo Endelevu - BAN KI MOON

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon,  akifungua mkutano wa Nne wa  Maspika wa Mabunge  Duniani, siku ya Jumatatu, kulia kwake ni Rais wa IPU   Bw.  Saber Chowdhury na Katibu Mkuu wa IPU Bw. Martin Chungong 
Spika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Ann Makinda akiwa na ujumbe wake  akifuatilia kwa makini hotuba za  ufunguzi wa Mkutano wa Nne wa Maspika wa  Mabunge Duniani ulioanza siku ya jumatatu hapa Makao  Makuu ya Umoja wa mataifa
Maspika wa Mabunge kutoka  Mataifa yanayoendelea na  yaliyoendelea wakiwa katika  ufunguzi wa Mkutano wao wa Nne ambao  hufanyika kila baada ya miaka  mitano. Ufunguzi wa Mkutano huu umefanyika katika Ukumbi Mkuu wa  Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa


Na MwandishiMaalum, New York
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,  mewaasa Maspika wa Mabunge Duniani kuhakikisha kwamba wanakuwa mstari wa mbele katika utekelezaji wa Malengo na Ajenda Mpya za Maendeleo Endelevu,  kwa kushirikiana na Serikali zao na Asasi za Kijamii.
“ Mnakutana katika kipindi ambacho dunia inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwamo ya wimbi kubwa la wakimbizi wanaokimbia  vita na machafuko katika nchi zao,  wimbi ambalo halijawahi kutokea tangu vita kuu ya pili ya dunia”.

Ban Ki Moon  ameyasema hayo siku ya jumatatu wakati akifungua mkutano wa Nne wa Maspika wa Mabunge Duniani ambao hufanyika kila baadaya miaka mitano. Mkutano huu wa siku tatu unafanyika hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa na umeandaliwa na  Chama cha Kimataifa cha Wabunge ( IPU).

Na kuongeza. “ Tunachagizwa kuimarisha jitihada na juhudi za kuhubiri Amani,  usalama, maendeleo endelevu na haki zabinadamu duniani kote”.

“Watu wanataka elimu,  wanataka huduma bora za afya, nafursa zaidi za ajira. Wanataka kuishi pasipo kuwa na hofu.  Wanataka kuziamini Serikali zao na Taasisi zake.  Wanataka kuheshimiwa kwa haki za binadamu na haki ya kuzungumza nakusikilizwa katika maamuzi yanayohusu maisha yao ”akasema Ban ki Moon.


Maspika wanaohudhuria mkutano huu, wanatoka katika mataifa yaliyoendelea na yanayoendelea. Ujumbe wa Tanzania,  unaongozwa na Mhe. Anna Makinda, Spika wa Bunge  la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Na pengine jambo muhimu kwenu na ambalo linawiana na majukumu yenu ni hili.  Hiki ni kipindi ambacho mifumo ya kiserikali katika sehemu kubwa ya dunia inakabiliwa na changamoto ya kukosa kuaminiwa,  uwakilishi na ushiriki” anaeleza katibu Mkuu

Akizungumzia kuhusu ajenda na malengo mapya ya maendeleo, Ban Ki  Moon amesema kuwa malengo hayo ambayo yapo  17 yamelenga zaidi katika maisha ya watu na sayari dunia. Na yanatoa mpango wa utekelezaji katika kumaliza umaskini, njaa na kujenga maisha yenye hadhi kwa wote bila ya kumwacha yeyote nyuma.
      
Aidha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,  amesema lengo namba 16 linazungumzia demokrasia,   kwa kutoa wito jamii na taasisi jumuishi.  Na kwamba suala la demkorasia limetawala katika andiko lote la malengo mapya ya maendeleo kama upande wa fedha kwa kutia msisitizo wa upatikanaji wa raslimali,   huduma za afya, elimu na fursa za ajira na zenye hadhi kwa wote.

Akasisitiza kwamba kazi ya kutekeleza na kusimamia malengo haya ni kubwa, inayohitaji Serikali kufanya kazi na kwa ushirikiano wa karibu na Asasi za Kijamii, uhusiano ambao anasema una toweka ama haupo kutokana na baadhi ya nchi kuweka masharti magumu dhidi ya Asasi za Kijamii.

Mbali ya  Ban Ki Moon, viongozi wengine waliozungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano huu wa Maspika wa Mabunge ni pamoja na Rais wa Baraza Kuu la 69 la Umoja wa Mataifa.

Baada ya ufunguzi Maspika waliendelea na majadiliano ya jumla yaliyojikita katika maudhui ya  Amani, demokrasia na maendeleo endelevu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.