Na. Miza Othman Maelezo.
Jumuia ya Wazee Zanzibar imeiomba Serikali kutunga sheria maalum ya kuwalinda na kupewa nafasi katika chombo cha kutunga sheria ili waweze kuwakilisha maoni yao na kutafutiwa ufumbuzi unaofaa.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) Rahaleo, Mwenyekiti wa Jumuia hiyo Bi. Salma Saleh Ismail amesema wazee wanakabili na changamoto nyingi zinazohitaji kuwa na sheria maalum na uwakilishi ndani ya Baraza la kutunga sheria.
Amesema vijana pamoja na watoto wametungiwa sheria zao hivyo na wazee wanahaki ya kuandaliwa sheria ili kuepukana na unyanyasaji na udhalilishaji wanaofanyiwa wazee.
“Vijana na watoto wamepewa kipaumbele kwa kutungiwa sheria za kuwalinda na sisi wazee tunahitaji sheria kama hizo na kupatiwa nafasi ili tuweze kuwakilishwa katika chombo cha kutunga Sheria,” amefahamisha Mwenyekiti huyo.
Aidha amesema lengo la Jumuiya ya Wazee Zanzibar ni kuboresha maisha ya wazee na kupambana na unyanyasaji na kudharauliwa na kuhakikisha wazee wanaenziwa na kupatiwa huduma muhimu katika meneo wanayoishi.
“Hakuna kitu muhimu kama kumenzi mzee kwani unapata fadhila nyingi, na sisi tumeona kuwa wazee wamesahaulika na ndio sababu tumeamua kuanzisha Jumuia hii kwa kushirikana na Serikali tuweze kuwasaidia,” ameeleza Bi Salma
Amefahamisha kuwa Jumuiya imeanzisha utaratibu wa kuwsajili wazee wote wenye umri kuanzia miaka 60 kupitia kwa masheha wao na kwa kuanzia tunawaombea pencheni ya kila mwezi ili waweza kujisaidia kimaisha.
Wazee wameishauri Serikali kuwaandalia utaratibu maalum katika vituo vya afya kwa kuwawekea sehemu yao ya matibabu ili kuepukana na msongamano wa wagonjwa katika vituo na hali zao za kiafya.
Nae Katibu wa Jumuiya hiyo Amani Suleiman Kombo amesema Jumuiya imetoa elimu sehemu mbali mbali kupitia taasisi za dini kwa lengo la kuhamasisha wananchi umuhimu wa wazee ili kuepukana vitendo vya unyanyasaji na udhalishaji.
Siku ya wazee Duniani huadhimishwa kila ifikapo tarehe 01Oktoba ambapo Zanzibar mwaka huu itaadhimishwa kwa shughuli mbali mbali ikiwemo kuwatembelea wagonjwa, kutembelea sehemu za kihistoria na kutafanyika Bonaza la michezo.
No comments:
Post a Comment