Habari za Punde

Simulizi ya Hujaaj - Katika Hijja kuna mazingatio makubwa

Ni simulizi ya moja wa mahujaji wa mwaka jana 2014 aliyebahatika kutulia na kuiweka ziara yake katika maandishi. Ni ndefu lakini imejaa mafundisho.

Alhamdulillaah nilibahatika kuwa miongoni mwa waliojaaliwa kuitekeleza Ibada ya Hajj mwaka 1435.(2014)

Nilikuwa kwenye mafunzo ya kivitendo ya siku sita kuanzia tarehe 8  Dhulhijjah -mfunguo tatu mpaka tarehe 13 Dhulhijjah 1435.

Kwa wale watakaombatana na safari yangu hii ni kwamba Hijja ni ibada ambayo hufanyika katika mji wa Makkah, Saudi Arabia ni matendo maalum, yanayofanyika katika wakati maalum, sehemu maalum na kwa ajili ya watu maalum. Ni nguzo ya tano katika nguzo za kiislamu ambayo humuwajibikia kila Muislamu mwenye uwezo mara moja katika maisha yake.

Naam ni siku sita tu lakini nimeweza kujifahamu na kujitambua katika kipindi cha siku sita ambazo zitabakia katika kumbukumbu ya maisha yangu. Kwani mafunzo yake ya kinadharia, kivitendo na kiroho ni mafundisho nadra unayoweza kuweza kuyapata kwa kipindi kifupi na yakaweza kuleta athari kubwa katika maisha ya Muislamu.

Nikikumbuka kwa mara ya pili nilipoivaa Ihraam siku ya Tarwiyah, tarehe 8 Dhulhijjah na kutia nia ya Hajj na kuanza Talbiyah “Labbayka Allaahumma Labbayka Labbayka Laa shariyka laka Labbayka Innal hamda Wanni’imata laka walmulk Laa shariyka laka”. Sikujikuta peke yangu, kila ninaemkuta njiani anatamka Talbiyah kama mimi. Kila ninaemkuta njiani amevaa Ihraam kama mimi shuka mbili tu nyeupe miongoni mwa wanaume hana kitu chochote ndani kwani ni haramu kuvaa nguo yoyote iliyoshonwa wakati upo katika Ihraamu. Sote tumevaa viatu vya kawaida tu mithili ya kanda mbili au viatu visivyofunika mguu wote na hakuna hata mwanamme mmoja aliyevaa kofia, ukishahirimia hutakiwi kuvaa kofia kichwani kwa mwanamme au kupaka manukato ya aina yoyote.

Kila ninamkuta njiani simjui jina lake wala wapi anapotoka, simjui kama ni Daktari au ni Mwalimu, Mpagazi au Mchuuzi, ni mheshimiwa au mtu wa kawaida, mweupe, mweusi mkubwa, mdogo  lakini namjua kama ni ndugu yangu Muislamu  na sote tumetamka Laa Ilaaha Illa Llaah Muhammadun Rasuulu Llaah. Kalima au neno hili ndilo lilitukutanisha katika ardhi ya Haram, Kalima hili ndilo litakalokutanisha peponi, Kalima hili ndilo litakalotuepusha na adhabu kali ya moto wa Allaah ‘Azza wa Jall ikiwa tutakamilisha masharti yake saba.

Tulipofika Mina huku tukiendeleza Talbiyah na kuomba dua kwa Allaah ‘Azza wa Jall, kila nikiirudia Talbiyah basi nafsi yangu inanikumbusha ujumbe mzito uliopo kwenye talbiyah nao ni wa Tauhiyd kumpwekesha Allaah ‘Azza wa Jall kwa ibada na kila kwa kila kitu.  Tunamhakikishia Allaah ‘Azza wa Jall kwamba hana mshirika huku tumemwitikia, tunamthibitishia Allaah ‘Azza wa Jall kwamba hakika himidi na shukrani, neema na ufalme vyote ni vyake pekee na hana mshirika.

Nikaikumbuka aya katika Qur’aan inayosema: “hakika Sala zangu, vichinjwa vyangu, uhai wangu na mauti yangu vyote ni vya Allaah Mola wa viumbe vyote, hana mshirika na hivyo nimeamrishwa kuwa Muislamu wa awali”. Naam Hijja ni darsa muhimu inayotufundisha somo la Tawhiyd kwani Mtume Muhammad Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam alihama Makkah kwenda Madina (kwa sababu ya kuisimamisha Tawhiyd) na aliporudi kuikomboa Makkah aliikomboa bila ya kumwaga damu na kuisimamisha Tawhiyd.

Naam Mina ni Masha’aril Haraam mojawapo katika sehemu takatifu kwa Waislamu ni sehemu ambayo ukiomba kwa Allaah ‘Azza wa Jall hutakabaliwa du’aa yako. Nilijitahidi kuomba na kila Muislamu ninaemuona yumo katika maombi, au dhikr au anasoma Qur’aan mpaka nafsi inanisuta mbona siku zote ulikuwa hufanyi Ibada kama hivi? Nikaijibu nipo katika sehemu takatifu na nimekuja kwenye mafunzo ya vitendo nafsi we. Naam nikajaaliwa kuzisali sala za Adhuhuri, Alasiri, Magharibi na Isha pamoja na Alfajiri Jamaa kwa kupunguza Sala zenye rakaa nne kama alivyofanya Mtume Swalla Allaahu ‘Alayhi Wasallam alipohiji.

Tulipoamka Alfajiri siku ya pili ya mafunzo, Siku ya Arafah siku adhimu katika masiku ya dunia, siku muhimu kwa mwenye kuhiji kwani ndiyo nguzo kuu ya Hajj ambayo ikikosekana basi aliyefanya safari hii hana Hajj, tulijiandaa kuelekea Arafah asubuhi na mapema kutoka Mina.

Tulipowasili viwanja vya ‘Arafah, nilihakikisha nipo katika mipaka yake ili Ibada yangu ikamilike. Tulibahatika mwaka huu siku ya ‘Arafah kuangukia Ijumaa kama ilivyokuwa kwa kipenzi chetu Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam miaka 1435 iliyopita hivyo tukapata fursa mbili za kuweza kukubaliwa duaa, maombi, shida na matlaba yetu – fusa ya ‘Arafah na fursa ya Ijumaa.

Ilipofika muda wa kuanza ‘Arafah (baada ya Zawaal yaani jua kutenguka) tulisali Adhuhuri na Alasiri jamaa ya kutanguliza na kupunguza kwa kuzisali rakaa mbili mbili. Kisha tukatangaziwa kwamba ule muda ambao shetani anaukasirikia kadri ya kukasirika umefika wa kupeleka maombi yetu, shahada zetu, maelezo yetu, CV zetu kwa Allaah ‘Azza wa Jall umeanza.

Siku ambayo Mtume wetu Swalla Allaahu ‘Alayhi wasallam ambaye tayari ameshasamehewa madhambi yake yaliotangulia na yatakayokuja alisimama kuanzia adhuhuri mpaka kuzama kwa jua akiomba tu huku mikono yake akiwa ameinyanyua kwa masaa takriban sita. Nikajiuliza wapi mimi na Mtume Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam?  Nikajiambia kimoyomoyo nijaribu kuiga mwenendo wake nikatoka nje ya hema nikaelekea qiblah na kuanza kuomba kila dua ninayoijua au niliyobahatika kuisikia na kuihakikisha si miongoni mwa dua zilizokuwa na walakini.

Ni siku ambayo niliingiwa na simanzi, mwili nikausikia una joto na huku chozi likinitoka ninamuomba Allaah ’Azza wa Jall kwani niliwahi kuisikia hadithi ya Mtume Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam inayosema jicho litalotoa machozi kwa ajili ya Allaah halitogusa moto siku ya kiama! Naam licha ya jitihada zangu sikumfikia au kuifikia rekodi ya Mtume Swalla Allaahu ‘alayhi Wasallam.

Kulikuwa na joto lakini sikujali, kwani sikuwa pekee yangu kwenye jua, mamilioni ya waislamu tulikuwepo ‘Arafah sote tukifanya jambo moja tu; Kuomba. Joto ni kitu gani mbele ya joto la moto wa Jahannam!

Naam ‘Arafah ni siku adhimu, ‘Arafah ni siku pekee ambayo haina mfano wake kwani hakuna siku katika masiku ya dunia ambayo Allaah ‘Azza wa Jall huwaachia huru waja wake na moto kwa wingi kama siku ya ‘Arafah. Ndio maana shetani huichukia.

Allaah ‘Azza wa Jall katika siku hii huwa karibu na Malaika na kuwauliza: “Wanataka kitu gani waja wangu hawa?” Allaahu Akbar.

Naam ikiwa ‘Allah ‘Azza wa Jall amewasamehe waja wake siku hii hata na mimi nilipokuwa nimesimama ‘Arafah nilimhakikishia Allaah ‘Azza wa Jall kwamba nimewasamehe wote walionikosea. Kwanini nisiwasamehe wakati nimehakikishiwa ikiwa Hijja yangu itakubaliwa basi nitarudi kama ndio kwanza nazaliwa? Nilipozaliwa sikuwa na niliemkosea wala alienikosea.

Kwanini nisiwasamehe wakati Mtume Swalla Allaahu ‘alayahi wasallam alipofika Makkah na kuikomboa aliwasamehe Maquraysh wote licha ya madhila, mateso na kila baya walilowatendea waislamu na aliwauliza: “Mnadhani nitakufanyeni nini leo?” Wakamjibu ‘Ndugu yetu uliye karimu , mtoto wa ndugu yetu aliye karimu’. Mtume Swalla Allaahu ‘Alayhi wasallam akawaambia: “Nendeni nyote mko huru” Hili ni darsa muhimu la kujifunza ndugu yangu tuwe ni wenye kusameheana kwa ajili ya kupata radhi zake Allaah ‘Azza wa Jalla. Kama angelikuwa Allaah ‘Azza wa Jall si mwenye kusamehe basi dunia hii isingelikalika ndio maana amejinasibu kuwa Yeye ni Ghaafir – mwingi wa kusamehe na pia Ghaffaar -anaendelea kusamehe (kila tukifanya makosa basi turudi kwake tuombe msamaha)

Ndugu yangu katika imani unaeusoma waraka huu, ukitaka upate mafunzo yatakayobadilisha mwenendo mzima wa maisha yako, jihimu uende Hijja na ukasimame ‘Arafah. Ukitaka ujihisi upo karibu na Allaah ‘Azza wa Jall na huku akisikia maombi na duaa zako, jihimu uende Hijja na umuombe Allaah ‘Azza wa Jall siku ya ‘Arafah. Ukitaka kuachiwa huru na moto, jihimu uende Hijja na uwepo katika viwanja vya ‘Arafah ukimuomba Allaah ‘Azza wa Jall maombi yanayotoka ndani ya moyo wako, yaliyojaa Ikhlaas na kumthibitishia Allaah ‘Azza wa Jall kwamba ni yeye pekee ndiye mwenye kupokea na kuyakubali maombi yote yawe makubwa au madogo.

Ilipofika magharibi mafunzo yetu yakaendelea kwa kwenda viwanja vya Muzdalifah kutekeleza moja katika mambo yaliyo wajibu katika Hijja.

Muzdalifah nimekutana na mafundisho kadhaa kama la kutakiwa kulala nje tena chini kwenye jangwa lisilo na kitu chochote. Ni fundisho kubwa sana kwani hapo kila aliyekuja Hijja bila ya kujali uwezo wake, ulwa wake, cheo chake anatakiwa kulala chini kama alivyolala Mtume wetu Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam na akatukumbusha kwamba: “chukueni kutoka kwangu matendo yenu ya Hajj”. Ndiyo nina kitanda cha sita kwa sita nyumbani lakini Muzdalifah nimelala chini kwa ajili ya kutekeleza Manaasik ya Hijja.

Muzdalifah hukutanika Mahujjaaj wote wakiwa dhalili wakiwa na shuka mbili tu licha ya utajiri waliojaaliwa nao, wakilala sehemu ya ardhi isiyokuwa na tandiko zaidi ya zulia au busati kwa atakayejaaliwa licha ya neema ambazo Allaah ‘Azza wa Jall amewajaalia baadhi ya waja wake. Yote ni kwa ajili ya kutufundisha fundisho muhimu katika maisha kwamba tuondokane na kiburi na majivuni kwani licha ya kujaaliwa kila tulichojaaliwa lakini utukufu ni wa Allaah ‘Azza wa Jall pekee - Mwenye nguvu na mshindi na kuwepo kwetu Muzdalifah tunauthibitisha utukufu huu kwa vitendo. Allaahu Akbar

Naam tulipofika Muzdalifah tukasali Magharibi na Isha kwa kuzichanganya na kupunguza Isha kwa kuisali rakaa mbili.

Kisha tukatakiwa kuokota vijiwe vidogo tu saizi ya kokwa ya ubuyu kwa ajili ya kupiga Minara ya Jamaraat. Nikaokota vijiwe sabini na kuongeza vichache.   Kwa nini sabini? Kwa sababu nitatakiwa kuvitumia kwa muda wa masiku matatu kama sina haraka na kama nina haraka ningetumia kwa masiku mawili. Ndivyo alivyotupa rukhsa Allaah ‘Azza wa jall katika Qur’aan.

Lakini nilipovipitia vitabu vikanikumbusha kwamba kama nikitaka hasa kumfuata Mtume Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam  yeye aliokota vijiwe saba tu Muzdalifah kwa ajili ya kupiga Jamaratul Kubra pekee ama vijiwe vyengine aliviokota Mina. Mina pia kumeruhusiwa kuokota vijiwe.

Nikapanda basi kurudi Mina nikitokea Muzdalifah huku nikiwapita maelfu na maelfu ya Mahujjaaj waliokuwa wakielekea Mina kwa miguu.! Namshukuru Subhaana kwa kujaaliwa usafiri lakini hapo nikajiuliza hivi Hijja yangu ni bora zaidi au Hijja ya waendao kwa miguu?

Nikamkumbuka Mtume Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam yeye alipohiji, alihiji akiwa juu ya Ngamia. Kwa hivyo nikajikinaisha kwamba ninaetekeleza Sunnah ya Mtume wetu Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam.

Tulipofika Mina nikaendelea na siku yangu ya tatu ya mafunzo, siku hii huitwa siku ya kuchinja – Yawmun Nahr. Ndio siku yenye mafundisho mengi kuliko siku nyengine za Hijja. Tuendelee

Nikaianza safari yangu kuelekea Jamaraat (kupiga mawe) nikitokea Mina kwa miguu ni mwendo wa nusu saa tu, lakini kutokana na msongamano wa watu jinsi walivyokuwa wengi ilinichukua saa 1.30 kufika Jamaraat.

Siku kila aliyekuja kuhiji hutakiwa kupiga mawe Jamaratul ‘Aqabah au kubra. Mnara mkubwa katika minara mitatu iliyopo eneo la Jamaraat.

Nilifika salama usalimini eneo la kupiga mawe (hii ni sehemu ya hatari katika sehemu zote za hijja kwa kuwepo msongamano mkubwa kila mwaka ambao mara nyingi hupelekea vifo vya mahujjaaj). Nikakoma kusema Talbiyah kwani kisheria nikifika sehemu ya Jamaratul ‘Aqabah ndiyo sehemu ya mwisho ya kusema Talbiyah ambayo niliikuwa nikiisoma tokea nilipovaa Ihraam siku ya tarehe 8 dhulhijjah.
Nikatafuta sehemu muwafaka ya kurusha mawe kutokana na wingi wa watu na nilipoipata nikaanza kurusha kijiwe cha kwanza huku nikisema: Bismillaah Allaahu Akbar. Nikafuatanisha na chengine kwa kusema Allaahu Akbar pekee bila ya bismillaah hadi nikamaliza vijiwe saba. Jamaratul kubra ukimaliza kupiga mawe hutakiwi kusimama baada yake na kuomba du’aa kama ilivyo kwa minara mengine na pia ni Jamarah pekee ambalo limeruhusiwa kupigwa kabla ya Zawaal siku ya iyd (kuchinja).

Nilipomaliza nikaendelea na safari yangu kwa miguu kutoka Jamaraat hadi ‘Aziziyah kitongoji kimojawapo kaskazini mwa Makkah tulipofikia. Kutokana na msongamano safari hii pia ilinichukua takriban saa nzima.

Alhamdulillah nikatumiwa ujumbe mfupi kwenye simu yangu (kutoka kwa kiongozi wa kundi letu) kwamba kichinjwa changu tayari kimeshachinjwa kwani hii pia ni mojawapo ya Ibada inayotakiwa kufanyika katika siku hii au ziku za Tashriyq (yaani tarehe 11,12 na 13 Dhulhijjah). Nikaulizia nini maana ya Tashriyq? Nikajuulishwa na wenye weledi na Hijja ni ile nyama inayochinjwa siku ya Eid huanikwa juani hadi kukauka na kuhifadhiwa ndiyo maana yake. (kumbuka miaka hiyo hawakuwa na majokofu ya kuhifadhi nyama kama tulivyo siku hizi)

Baada ya kupumzika kidogo, nilikoga na kuvua Ihraam zangu kwani hapa tayari nimekuwa nimetahallal (kutoka ihram) kidogo kwani nimeruhusiwa kufanya mambo yote isipokuwa kustarehe na mke nikatakiwa kuendelea na mafunzo yangu kwa siku kwa kuelekea Al Ka’abah kwa ajili ye kutekeleza nguzo mbili kuu za Hijja, kufanya tawaaf kufanya Sa’iy.

Safari yangu kutoka Aziziyah hadi Al Ka’abah ilinichukua saa 1.15 naam kwa miguu. Nilipofika Al Ka’abah ambapo umati uliokuwepo hapo siku hii ukiteleza nguzo za Hijja na umati mwengine ambao niliuacha Mina nikajisemea moyoni Alhamdulillaah, haya ndio matunda ya kazi aliyoifanya Mtume Muhammad Swalla ‘Allaahu ‘alayhi Wasallam. Ninayoshuhudia kwa macho yangu ni ushuhuda kwamba Mtume Muhammad Swalla ‘Allaahu ‘alayhi Wasallam amefikisha ujumbe na kutimiza amana aliyopewa na Allaah ‘Azz wa Jall. Nina imani Allaah ‘Azza wa Jall anashuhudia kwamba Mtume Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam amefikisha ujumbe kama alivyoagizwa.

Nikaingia msikitini kwa kuomba du’aa ya kuingia msikitini na kuelekea sehemu ya kuanzia Tawaaf.

Tawaaf ni ibada unayotakiwa uizunguke Al Ka’abah mara saba ukianzia sehemu lilipo jiwe jeusi (Hajarul aswad). Unatakiwa kuzunguka ilhali Al Ka’abah ipo upande wako kushoto ( anti clockwise). Ni mojawapo katika nguzo za Hijja na lazima ifanyike veynginevyo Hijja haitosihi.

Tawaaf ya nguzo huitwa Tawaaful Ifaadhah au Tawaafu Ziyaarah. Lazima uwe katika hali ya tohara kabla ya kufanya tawaaf (uwe na udhu).

Sehemu ya kuanzia imewekewa ishara ya taa rangi ya kijani pamoja na maelezo kwa kiarabu kwamba hapa ndipo sehemu ya kuanzia na kumalizia Tawaaf. Nikaelekea kona lilipo Hajarul Aswad (jiwe jeusi) na kuliashiria na kusema Allaahu ‘Akbar na kuanza Tawaaf huku Al Kaabah ikiwa kushoto kwangu.

Siku hii na umri huu na umati uliokuwepo sikuwa na ubavu wa kulifikia Hajarul aswad na kulibusu kama alivyofanya Mtume Muhammad Swalla ‘Allaahu ‘alayhi wasallam nikabaki kuliashiria tu ambayo pia inakubalika kisheria. Kila nikifika Ruknil Yamani (kona ya Yemen kona ya tatu kabla ya kona ya hajarul aswad) nilitakiwa kuomba dua’a aliyotufundisha Mtume Muhammad Swalla ‘Allaahu ‘alayhi Wasallam na kusema: ` Rabbanaa aatinaa fiddunyaa hasanatan wafil akhirati hasanatan waqinaa ‘adhaaba Nnaar. (Mola wetu tupe katika dunia yaliyo mazuri na katika akhera yaliyo mazuri na utuepushe na adhabu ya moto)

Umati uliokuwepo ukifanya Tawaaf ukanikumbusha kwamba kwenye Baytul Ma’amuur, mbinguni kuna umati kama huu wa Malaika nao ukifanya Tawaaf. Tofauti na umati uliokuwepo baytul haraam na baytul ma’amuur ni kwamba umati wa baytul maa’muur hufanya tawaaf mara moja katika uhai wao na hawarudi tena! Allaahu Akbar

Nikiendelea kufanya Tawaaf kwa kuizunguka Al Ka’abah mara saba na kila nikifika eneo la Hajarul aswad niliashiria na kusema Allaahu Akbar. Ilikuwa ni wakati wa adhuhuri jua likiwa kali na tayari nimeshapata kufanya mwendo tokea Mina hadi Jamaraat, Jamaraat hadi Aziziyah, Aziziyah hadi Al Ka’abah na sasa nikiendelea na mwendo wenye kheri na Baraka wa Tawaaf, sikuhisi machofu ya aina yoyote.

Nilipofanya Tawaaf na nikabahtika kuifanya kwenye Mataaf (sehemu ya chini ya kutufu karibu na ‘Al Ka’abah) nilikuwa nnajiuliza inawezekana katika mojawapo ya sehemu nimepita ni sehemu alipopita Mtume Swalla ‘Allaahu ‘alayhi wasallam alipofanya Hijja yake kwa hivyo nimeweza kupata angalau Sunnah. Ila nitajuaje kama nimeipatia?

Naam kwenye Mataaf kuna msongamano, kuna mchanganyiko wa wanawake na wanaume lakini yote haya hayakunijia katika mawazo yangu. Kilichokuwepo katika mawazo yangu ni kupata fursa nadra ya kuwa karibu sana na Al ka’abah – nyumba ya kwanza iliyoasisiwa kwa ajili ya Ibada. Allaahu Akbar! Kama ni unyenyekevu basi ukiwa karibu na Al Ka’abah utaupata wa hali ya juu. Kama ni udhalili basi ukiwa karibu na Al Ka’abah utaupata wa hali ya juu. Ni hisia ambazo haziwezi kuelezeka mpaka uwepo mwenyewe karibu na nyumba ya Allaah ‘Azza wa Jall ndipo utakapozifahamu hisia hizi. Kama bado hujafanya ibada ya Hijja ndugu yangu katika Imani, jihimu na fanya haraka.

Nilipomaliza kufanya Tawaaf ambayo ilinichukua takriban saa 1.15 nikatafuta sehemu nyuma ya Maqaamu Ibrahim kwa ajili kusali Sunnah rakaa mbili, sikuipata kutokana na zahma na msongamano. Nikatafuta sehemu tu na nikaswali rakaa mbili , rakaa ya kwanza nilisoma Alhamdu na Qul Yaa ayyuhal Kaafirun na rakaa ya pili nilisoma alhamdu na Qul huwa Llaahu ahad. Ndivyo alivyotufundisha Mtume wetu Swala Allaahu ‘alayhi wasallam.

Baada ya hapo nikaelekea sehemu yalipo maji ya zamzam, nikanywa kadri ya kiu yangu huku kila nikinywa huomba du’aa. Mtume Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam alituagiza tunapokunywa maji ya zamzam ni dawa ya maradhi na pia kujipangusa katika sehemu za mwili.

Nilipomaliza nilitakiwa kurudi tena na kulibusu Hajarul aswad lakini haikuwezekana kutokana na msongamano nikabakia kuliashiria tu.

Bado niko katika siku yangu ya tatu ya mafunzo na nilipomaliza funzo la Tawaaf nikaanza funzo la Sa’iy.

 Sa’iy ni kwenda matiti kati ya Jabal Swafaa na Jabal Marwah. Milima hii imo ndani ya Msikiti ambako kumetengenezwa eneo maalum la kjufanya ibada hii. Fundisho hili ni muhimu kwa ni mojawapo katika mambo ambayo lazima niyafanye ili Hijja yangu ikamilike ni mojawapo ya nguzo za Hijja.

Fundisho hili lina mazingatio makubwa kwani linatukumbusha kisa cha mke wa Nabii Ibrahiym ‘alayhis salaam alipomwacha mkewe bi Hajrah na mtoto mchanga Nabii Ismaail ‘alayhis salaam kwenye jangwa lisilokuwa na chochote wakati huo. Na Bi Hajrah alimuuliza Nabii Ibrahiym ‘alayhis salaam: “kwanini unatuacha hapa?” Nabii Ibrahiym ‘alayhis salaam hakumjibu kitu mpaka alipomuuliza: “hivi ndivyo alivyokuamrisha Mola wako?” Akajibu: “naam” basi Bi Hajra akasema: “Mola wetu hatotuacha mkono”.

Ni kisa kirefu ila fundisho muhimu ni pale Bi Hajrah alipoishiwa na maji na akawa anatafuta kila upande akihaha huku na kule akienda katika ya Jabal Swafaa na Marwah. Na kila akipita sehemu alipomwacha Ismaaiyl na kumsikia akilia alizidisha mwendo kutafuta maji.

Naam tunafanya Sa’iy kwa kumkumbuka mke wa Nabii Ibrahiym ‘alayhis salaam alipokuwa akihangaika kutafuta, maji kwa ajili ya mwanawe.

Nikafika Jabal Swafaa ambapo hutakiwa kuanzia na kumalizia Marwah. Nilipoweka mguu wangu kwenye mlima Swafaa nikasoma aya Inna Swafaa walmarwata min sha’aairi Llaah, faman hajjal bayta awi’itamara falaa junaah ‘alayhi an yatawwafa bihimaa, wamna tattawa’a khayran, Fainna Llaah Shaakirun ‘aliym. (Suuratul Baqarah 158)

Nilipomaliza nikasema kama alivyosema Mtume Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam – abdau bimaa bada-a Llaahu bihi ( Ninaanza kwa kile ambacho Allaah alianzia)

Kisha nikapanda Jabal Swafaa (ukitaka kulipata Jabal Swafaa itakubidi ufanye Sa’iy chini na si kwenye ghorofa ya kwanza au ya pili) mpaka kufikia sehemu ambayo ninaweza kuliona Al Ka’abah, nikaelekea qiblah na kisha nikaomba dua’a aliyotufundisha Mtume Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam

Kisha nikaanza kutembea kutoka Jabal Swafaa nikielekea Marwah ili kukamilisha mzunguko mmoja.

Nilipofika kwenye alama za taa za kijani (karibu na Jabal Swafaah) nikaongeza mwendo na kwenda mwendo wa haraka (ni Sunnah kwa wanaume tu jambao ambalo pia hushangaza kwani alietuletea utaratibu huu ni mwanamke , mke wa nabi Ibarhiym ‘alayhis salaam) na zilipomalizika alama nikaendelea na mwendo wa kawaida hadi nilipopanda Jabal Marwah nikasoma kama nilivyosoma nilipanza Jabal Swafaa na kuendelea na sa’iy.

Nilikithirisha kuomba du’aa na kumkumbuka Allaah ‘Azza wa Jall muda wote wa Sa’iy mpaka nnamaliza.

Kila nikijaribu kupata mazingatio katika Sa’iy naona tuna mengi ya kujifunza kwani chimbuko la maji ya zamzam ni kutokana na Sa’iy aliyoifanya Bi Hajrah. Tukio hili ambalo mamilioni ya waislamu duniani hulifanya kila mwaka ni limeanzia na Bi Hajrah wakati alipokuwa akihangaika kwa ajili ya mwanaye mchanga. Kwanini Nabii Ibrahiym ‘alayhis Salaam amuwache mkewe kwenye jangwa ambalo halina kitu wala watu wala maji? Majibu ya masuala haya ndiyo hii nyumba ya mwanzo iliyoasisiwa kwa Ibada. Allaahu Akbar. 
 
Alhamdulillaah nimemaliza fundisho muhimu la Hijja ambalo limehitaji kutumia mwendo wa miguu kama ilivyokuwa Tawaaful Ifaadhah, kama ilivyokuwa safari yangu kutoka Mina hadi Jamaraat, Jamaraat hadi Aziziyah, Aziziyah hadi Haram.

Naam mwili sasa niliusikia kama umechoka na kipande cha kurudi Aziziyah nilipofikia kilikuwa si kidogo kutembea kwa miguu na bado nitatakiwa kutembea tena usiku kurudi Mina.

Niliamua kuchukua Taxi na kurudi Aziziyah ambapo nilipofika kabla ya kupumzika nilitekeleza fundisho jengine la Hijja la kunyoa nywele zote.  Naam mara nyingi huwa sinyoi kipara, hupunguza tu nywele zangu lakini ili Hijja yangu iwe na ubora niliamua kunyoa kwani Mtume Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam aliwaombea du’aa mara tatu walionyoa na mara moja waliopunguza.

Baada ya kumaliza kunyoa sasa nimetahallal kikamilifu yaani yale mambo yote niliyokatazwa wakati nipo katika Ihraam sasa nimeruhusiwa mpaka kustarehe na mke .

Natumai uliebahatika kusoma waraka huu utaweza kufaidika japo kidogo hasa kwa kuzingatia ibra – mazingatio yanayopatikana katika Ibada ya Hijja na Umrah na Allaah atuwafikishe katika kila lililokuwa na kheri kwetu.

Aamiyn


1 comment:

  1. Allah amlipe katika mizani ya kheri kwa simulizi hii ambayo ina manufaa si kwake tu, bali pia kwa wale wote wataojaaliwa kuusoma, kuuzingatia na kuchambua yale aliyoyaainisha kuwa ni mafundisho.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.