Habari za Punde

Dk Shein apongeza ushirikiano wa taasisi za elimu za Zanzibar na China


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akisalimiana na Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi kutoka China (ZHEJING UNIVESITY  OF MEDIA&COMMUNICATIONS) Rrof.Dk.Peng Shaojian wakati alipofika Ikulu mjini Zanzibar akiwa na ujumbe aliofuatana nao leo,[Picha na Ikulu.]

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akizungumza na Ujumbe kutoka nchini China katika Chuo cha (ZHEJING UNIVESITY  OF MEDIA&COMMUNICATIONS) chini ya kiongozi wake Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi  Rrof.Dk.Peng Shaojian (katikati) wakati alipofika Ikulu mjini Zanzibar akiwa na ujumbe aliofuatana nao leo,[Picha na Ikulu.] 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akiagana na mgeni wake Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi  Rrof.Dk.Peng Shaojian kutoka Chuo cha (ZHEJING UNIVESITY  OF MEDIA&COMMUNICATIONS) nchini China baada ya mazungumzo na Ujumbe  aliofuatana nao walipofika  Ikulu mjini Zanzibar leo,[Picha na Ikulu.]

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                  16 Oktoba, 2015
---
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema ushirikiano kati ya Chuo Kikuu cha Zhejiang cha China na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali ni mwanzo mzuri wa kujenga misingi imara ya ushirikiano madhubuti kati Taasisi za elimu ya juu humu nchini na zile za Jamhuri ya Watu wa China.

Akizungumza na ujumbe wa Chuo Kikuu cha Zhejiang leo, Dk. Shein ameupongeza uongozi wa chuo hicho kwa kuwapatia vijana wa Zanzibar nafasi za masomo ya shahada za kwanza katika masomo ya Habari na Utangazaji.

Aliuambia ujumbe huo ulioongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi wa chuo hicho Prof. Peng Shaojian kuwa masomo ya Habari na Utangazaji yana nafasi ya pekee katika ulimwengu wa sasa kwa vile masomo hayo yamekuwa nyenzo muhimu katika kusukuma maendeleo.

“katika ulimwengu wa leo habari na utangazaji ni nyenzo muhimu na ya pekee katika kufanikisha shughuli za binadamu ikiwemo maendeleo ya uchumi na kisiasa” Dk. Shein alieleza.

Alielezea kuvutiwa na azma ya Chuo Kikuu hicho kuanzisha ushirikiano wa karibu na Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) hatua aliyoielezea kuwa inadhihirisha urafiki na udugu uliopo kati ya watu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wa Jamhuri ya Watu wa China.

“Uhusiano kati ya nchi zetu ulianzishwa na viongozi wetu ambao walipigania Uhuru wa nchi zetu Marehemu Mao Zedong na Cho En Lai kwa upande wa China na kwa upande wa Tanzania ni Mwalimu Julius Nyerere na Mzee Abeid Amani Karume” Dk. Shein alisema.

Kwa hivyo mbali ya kuupongeza na kuushukuru uongozi wa Chuo cha Zhejiang, Dk. Shein aliunga mkono mpango wa pamoja kati ya SUZA na chuo hicho wa kuanzisha masomo ya habari na utangazaji katika chuo Kikuu cha SUZA ambayo yanalenga kuvutia pia wanafunzi kutoka nchi nyingine za ukanda huu.

“Ningependa kuona ushirikiano imara na endelevu kati ya Chuo chenu na SUZA na mpango huu nauona kuwa ni mwanzo mzuri wa kujenga ushirikiano huo” Dk. Shein alisema.

Dk. Shein alieleza kufurahishwa na taarifa kuwa wanafunzi wanaosoma chuoni hapo wote 21 wanafanya vizuri katika masomo yao ikiwemo lugha ya kichina ambayo ndio lugha ya kufundishia.

Akitoa maelezo kwa Mheshimiwa Rais, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amani Ali Juma Shamuhuna alisema chuo hicho kinatoa fursa za masomo ya habari na utangazaji kiwango cha shahada ya kwanza kwa wanafunzi wa Zanzibar tangu mwaka 2014.

Hivi sasa alisema kuna vijana 21 waliojiunga na masomo hayo ya miaka 4 tangu waanze kujiunga ambapo mwaka 2014 walijiunga wanafunzi 11 na kufuatia kufanya vizuri kwa wanafunzi hao chuo hicho kilitoa nafasi nyingine 10 ambapo Septemba 2015 wanafunzi hao walijiunga na kufanya idadi hiyo.  

Alibainisha kuwa ujumbe wa Wizara yake ulifanya ziara kutembelea chuo hicho mwaka jana kuangalia maeneo mapya ya ushirikiano na chuo hicho.Katika ziara hiyo aliongeza kuwa walitembelea skuli za awali, msingi na Sekondari na kujifunza namna ya kuendesha skuli na hatimae waliweza kuanzisha ushirikiano kati ya skuli hiyo ya sekondari na skuli ya Kiembesamaki ya hapa Zanzibar.  

Katika mazungumzo hayo walikuwepo pia viongozi wengine wa Wizara ya Elimu pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu na Utawala Bora Dk. Mwinyihaji Makame na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee.  
Kwa upande wake, Profesa Peng alimueleza Mhe Rais kuwa chuo chake kina dhamira ya kweli ya kujenga ushirikiano wa muda mrefu na SUZA na kwamba ushirikiano huo mbali ya kuanzisha programu za pamoja lakini pia chuo chake kitasaidia kujenga uwezo wa SUZA katika eneo la masomo ya Habari na Utangazaji.

Alisema chini ya ushirikiano huo, Chuo hicho kitatoa nafasi za masomo kwa wakufunzi wa SUZA katika fani ya habari na utangazaji katika ngazi ya shahada za uzamili na uzamivu ili kujenga uwezo wao wa kitaaluma.


Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.