Habari za Punde

Dk Shein:Tuzo ya Dhahabu kwa Sheria ya Watoto Zanzibar ni Kielelezo Dhamira ya Kweli ya Kuwapatia Watoto Wetu Ulinzi na Kuhakikisha Ustawi Wao.

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                                                     26 Novemba, 2015
---
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein amesema ushindi wa tuzo ya dhahabu iliyopewa Sheria ya Watoto ya Zanzibar ni kielezo cha matokeo ya kazi nzuri iliyofanywa na wengi kwa maslahi mapana ya watu wote wa Zanzibar.

“Ni umoja na mshikamano wetu uliotuwezesha kushirikiana wakati wote wa kutayarisha sheria hii pamoja na mkakati wake wa utekelezaji ndio uliotupatia zawadi hii adhimu kwa nchi yetu” Dk. Shein amesema.

Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo na Waziri wa Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana na Watoto Bibi Zainab Omar Mohamed Ofisini kwake Ikulu leo, Dk. Shein alieleza kuwa tuzo hiyo kuwa ni fahari kubwa kwa wananchi wa Zanzibar  na inadhihirisha azma ya serikali uhakikisha ulinzi na ustawi wa watoto nchini unakuwa wa kiwango kinachokubalika kitaifa na kimataifa.

Zanzibar ilitunukiwa tuzo hiyo ya Gold Future Policy Award kwa mwaka 2015 na kukabidhiwa mjini Geneva Uswizi tarehe 20 Oktoba, 2015 baada ya Sheria ya Watoto ya Mwaka 2011 kuzishinda sheria za nchi nyingine zaidi ya 20 kwa kukidhi vigezo vinavyoshindaniwa.

“Tuzo hii ni mwanzo wa kazi kubwa iliyo mbele yetu ya kuitekeleza sheria hii kikiamilifu na kuendelea kuonesha kwa vitendo utayari wetu wa kuwatia watoto wetu ulinzi unaowahakikishia maisha bora yenye kuwawezesha kukua katika mazingira bora na salama” Dk. Shein aliongeza.

Alibainisha kuwa wako wanaoiunga mkono sheria hiyo lakini akatahadharisha pia kuwa wako wanaoipinga sheria hiyo kwa dhahiri na wengine kwa kujificha lakini kitu muhimu ni kufanya kazi kwa bidii na ushirikiano ili sheria hiyo iweze kutekelezwa na kufikia malengo ya kupitishwa kwake.

“Tuitekeleze kwa bidii kwani kwa kupata tuzo hii wako watakaotayarisha sheria zao kwa kuchukua baadhi ya yaliyomo katika sheria yetu na wakaweza kutekeleza vizuri zaidi na kujipatia sifa zaidi ya sisi kama hatukuwa makini katika kutekeleza sheria yetu hii kwa sifa kulingana na malengo yaliyowekwa” Dk. Shein alitahadharisha.

Alibainisha kuwa kutokana na sifa iliyopata sheria hiyo mapema mwezi ujao Balozi wa Tanzania katika Shirikisho la Ujerumani Balozi Philip Marmo atawasilisha mada kuhusu sheria hiyo katika kongamano litakalofanyika huko katika mji wa Humburg nchini Ujerumani.

Akitoa maelezo ya Tuzo hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bibi Asha Ali Abdalla alieleza kuwa  hiyo ilitolewa na Taasisi ya Kimataifa ya World Future Council inayojishughulisha na kushajiisha uandaaji na utekelezaji wa sera zinazolenga katika kuimarisha ustawi, haki na hali za maisha kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Alifafanua kuwa kwa mwaka 2015 tuzo ilielekezwa katika sera na sheria zenye kulenga ustawi wa watoto na kwamba jumla ya sera na sheria za nchi 20 zilishindanishwa.

“Tumeshinda tuzo hii kwa kuwa imekidhi vigezo vinavyokubalika kimataifa pamoja na namna mchakato wetu wa kutengeneza sheria hii hadi kupitishwa kwake kuwa shirikishi” alibainisha Katibu Mkuu huyo.

Aliongeza kuwa hatua mbali mbali zilizochukuliwa hadi sasa na serikali kutekeleza sheria hiyo zimesaidia Zanzibar kushinda tuzo hiyo.

Alizitaja hatua hizo kuwa ni pamoja na uanzishwaji wa mahkama za watoto, vituo vya mkono kwa mkono vinavyosaidia wahanga wa vitendo vya udhalilishaji watoto na kuanzisha madawati ya jinsia katika vituo vya Polisi kushughulikia masuala ya udhalilishaji wa watoto na wanawake.

Katibu Mkuu aliongeza kuwa kampeni kubwa iliyoanzishwa na Mheshimiwa Rais ya kupiga vita unyanyasaji na udhalilishaji watoto  imesaidia sana Zanzibar kupata tuzo hiyo pamoja na kukamilika kwa Mkakati wa Miaka Mitano wa Mapitio na Marekebisho ya Sheria ya Watoto (Child Justice Reform: A five year Strategy 2013-2018).

“Tuzo hii imesaidia sio tu kuitangaza Zanzibar bali pia imedhihirisha utashi na dhamira ya kisiasa ya viongozi wa Zanzibar katika kusimamia sheria kupanga mikakati inayolenga kuhakikisha haki na ustawi watoto nchini” alisema Katibu Mkuu huyo.
Katika hafla hiyo mbali ya kukabidhiwa tuzo hiyo, Dk. Shein alikabidhiwa pia nakala za Sheria ya Watoto ya mwaka 2011 na Mkakati wa Miaka Mitano ya Mapitio na Marekebisho ya Sheria za Watoto.

Hafla hiyo ilihudhuria pia na Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee na manaibu Makatibu wakuu wa wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto.   

Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 
                                               

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.