Habari za Punde

Mawakili Zingatieni Maadili ya Taaluma ya Sheria – Jaji Mkuu Mhe.Othman Chande..


Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Othman Chande akiongoza maandamano ya Majaji na Watendaji wa Mahakama wakati wa hafla ya 53 ya kuwapokea na kuwaapisha Mawakili wapya 104 iliyofanyika katika viwanja vya Karimjee leo jijini Dar es salaam.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. George Masaju (kulia) akiwasili katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es salaam leo wakati wa hafla ya 53 ya kuwapokea na kuwaapisha Mawakili wapya 104.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Othman Chande akizungumza na Mawakili 104 walioapishwa leo jijini Dar es salaam. Mhe. Chande amewataka Mawakili hao kufanya kazi zao kwa kuzingatia weledi na maadili ya taaluma yao.
 Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Othman Chande (katikati) akiongoza akiwa na Majaji na Watendaji wa Mahakama wakiendelea na zoezi zoezi la kuwaapisha Mawakili wapya 104 katika viwanja vya Karimjee leo jijini Dar es salaam.
Mawakili wakiwa wamesimama mbele ya Jaji Mkuu kabla ya kuapishwa.
 Mawakili wakiwa wamesimama mbele ya Jaji Mkuu kabla ya kuapishwa.
Mawakili walioapishwa wakiwa katika picha ya pamoja na Jaji Mkuu Mhe. Othman Chande na Watendaji wa Mahakama ya Tanzania.
Na. Aron Msigwa Maelezo.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Othman Chande amewataka Mawakili kote nchini kufanya kazi zao kwa kuzingatia weledi na maadili ya taaluma ya Sheria na kwamba wasisite kuwaeleza ukweli wateja wao wanaopeleka mashauri Mahakamani ili kuepuka kupoteza muda na gharama katika masuala yanayoweza kupatiwa ufumbuzi nje ya Mahakama.

Akizungumza na Mawakili wapya 104 waliohitimu Shule ya Sheria  kwa mwaka 2015 wakati wa hafla ya 53 ya kuwapokea na kuwaapisha iliyofanyika katika viwanja vya Karimjee leo jijini Dar es salaam amesema kuwa msingi mkubwa wa kazi yao umejengwa katika uzingatiaji wa maadili ya taaluma ya sheria.

Amewataka Mawakili hao kubadilika kifikra kwa kuwa Mawakili Bora ili kujenga imani na uaminifu kwa jamii wanayoihudumia na kuongeza kuwa sasa wameingia kwenye utaratibu wa kutambuliwa rasmi na Mahakama ya Tanzania kwa kuwezeshwa kufanya shughuli za uwakili kwenye mahakama ya Tanzania maeneo mbalimbali nchini.


Naomba mtambue kuwa kila Wakili ni Ofisa wa Mahakama hivyo mnao wajibu na jukumu la kusoma, kufuatilia mashauri mbalimbali ili kuwa na uhakika wa kesi mnazosimamia kuliko kuzitegemea Mahakama

Aidha, ameeleza kuwa yapo mambo ambayo yamekua yakifanywa na baadhi ya Mawakili wasio waaminifu yanayochafua sura ya Taaluma ya Sheria ikiwemo kutumia nyaraka za kughushi, kuvunja Kanuni na Maadili ya Taaluma huku baadhi yao wakijikuta wakiingia katika mgogoro na Mamlaka zinazosimamia kitaaluma taaluma hiyo.


Nawataka mzingatie sheria, kanuni na Maadili ya Uwakili, hata hivyo tuna chombo kinachosimamia maadili yenu, wapo takribani 176 waliokiuka maadili na hawa wanashughulikiwa kwa mujibu wa Sheria ili kulinda maadili na utendaji wa taluma yenu Amesisitiza Mhe. Othman.

Amewataka  watimize wajibu wao kwanza kwa wananchi watakaouhudumia pamoja na Mahakama ya Tanzania ambayo inawataka kufanya kazi zao kwa kuzingatia Sheria,  kanuni na taratibu zilizowekwa.

Mhe.Othman amefafanua kuwa Mahakama ya Tanzania inaendelea na Mkakati wa kupunguza mrundikano wa Kesi Mahakamani kwa kuhakikisha kuwa kesi zote zinazofikishwa Mahakamani zinamalizika katika kipindi cha chini ya mwaka 1

Ameeleza kuwa silimia 47 ya kesi zaidi ya 200 zilizokuwepo Mahakama Kuu katika kipindi cha miaka 4 iliyopita zimeendelea kusisikilizwa kwa ubora na sasa zimebaki asilimia 17 ya kesi hizo jambo linaonyesha kuongezeka kwa ufanisi wa Mahakama.

Kwa upande wake Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. George Masaju akiwakaribisha Mawakili hao katika familia ya sheria Tanzania amesema kuwa katika jamii wanao mchango mkubwa katika kuhakikisha Haki na Usawa vinadumishwa nchini.

Amesema mawakili hao kabla ya kuapishwa na kuingizwa kwenye utaratibu wa kutambuliwa kuwa Mawakili wamepitia na kufauru vigezo vya kitaaluma vilivyowekwa ili kulinda heshima ya Taaluma ya sheria nchini.

Amewaeleza kuwa mara baada ya kupokea viapo vyao wameingia kwenye utumishi wa umma kutekeleza majukumu yao ya kikatiba na kuongeza kwamba wao kama wanasheria wanatakiwa kuzingatia weledi wa taaluma yao.

Amewataka kuwa makini katika utendaji wao kwa kuepuka kuwa sehemu ya migogoro na kuepuka kuegemea upande wowote watakapokuwa wakitimiza majukumu yao ili kuendelea kujenga jamii ya kistaarabu na ya kidemokrasia.

"Naomba mkumbuke kuwa mna wajibu mkubwa kwa watu mtakaokuwa mnawahudumia, zingatieni maadili maana ninyi sasa ni sehemu ya Mahakama ya Tanzania, fanyeni kazi kwa weledi na umakini mkubwa" Amesisitiza.

Amesema utekelezaji wa majuku yao ya kila siku ni sehemu ya utumishi wao katika umma hivyo wasiruhusu aina yoyote ya ukiukwaji wa maadili yakitika kutimiza majukumu yao na kuwasaidia wananchi wasiokuwa na kipato/ wananchi masikini watakakao omba msaada wao wa kisheria. 

Aidha amewataka wawe wabunifu, kufanya kazi kwa bidii na kujiendeleza pale inapowezekana ili waweze kuwa msaada kwa wananchi walio na kiu ya kupata huduma kutoka kwao.

Kwa upande wake Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Charles Rwechungura akizungumza wakati wa wa kuwakaribisha mawakili hao 134 amesema kuwa wao kama Chama cha Wanasheria wanayofuraha ya kuwakaribisha wanachama wapya kwenye uwanja wa Sheria nchini.

Amesema mawakili hao wameingia katika wakati muafaka kuongeza nguvu katika kuwahudumia wananchi huku akieleza kuwa shule ya Wanasheria Tanzania itaendelea kutoa mafunzo na kusimamia viwango vya taaluma ya sheria nchini na kuwataka mawakili hao kulinda heshima ya taaluma ya sheria kwa kutoa huduma bora kwa umma.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.