Habari za Punde

Uchunguzi wanaodaiwa kuharibu uchaguzi Zanzibar wakamilika



Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar (DPP) Ibrahim Mzee

Uchunguzi wa vigogo na watendaji wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec) wanaotuhumiwa kuharibu uchaguzi mkuu visiwani humo ambao matokeo yake yamefutwa umekamilika na majalada kuwasilishwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar (DPP), Ibrahim Mzee.


Hayo yalisemwa na Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai Zanzibar (DDCI), Salum Msangi, alipokuwa akizungumzia maendeleo ya uchunguzi huo.



Alisema kazi ya kuwahoji watuhumiwa mbalimbali wakiwamo baadhi ya makamishna wa tume hiyo, watendaji na askari polisi na usalama waliokuwa na dhamana ya kusimamia uchaguzi huo uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu imefanyika kwa umakini mkubwa kabla ya majalada yao kufikishwa kwa DPP.



“Majalada ya uchunguzi tayari tumekabidhi katika mamlaka za kusimamia mashtaka ikiwamo Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar,” alisema.



Masangi alisema uchunguzi huo ulianza kufanyika baada ya uchaguzi kuharibika na kusababisha Tume ya Uchaguzi Zanzibar kufuta matokeo yake Oktoba 28, mwaka huu.



“Mbali na watendaji waliohojiwa pia wananchi wa kawaida, wagombea wa nafasi mbalimbali pamoja na mawakala na wasimamizi wa vituo wamehusishwa katika uchunguzi huo.”



“Kinachoendelea huko zitafuteni mamlaka zinazohusika na ufunguaji wa mashtaka watakuambieni wamefikia hatua gani za kisheria. Sisi kwa upande wetu kazi ya uchunguzi tumekamilisha,” alisema.



Msangi alifafanua kuwa, kwa mujibu wa mgawanyo wa majukumu, Jeshi la Polisi kazi yake ni kufanya uchunguzi na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka kazi yake ni kufungua mash taka mahakamani pamoja na kutetea kesi.



Hata hivyo, juhudi za kumpata Mkurugenzi wa Mashitaka Zanzibar (DPP), Ibrahim Mzee, hazikufanikiwa jana kutokana na simu yake kutokupokelewa mara kadhaa alipopigiwa.



Matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar yalifutwa na Mwenyekiti wa Zec, Jecha Salim Jecha, akisema kulibainika kasoro tisa katika uchaguzi huo, ikiwamo masanduku ya kura kuchukuliwa na kuhesabiwa nje ya vituo kinyume na sheria na mawakala wa baadhi ya vyama kupigwa na kufukuzwa katika maeneo yao ya kazi.



Alisema sababu nyingine ni kufanyika udanganyifu ikiwamo kura kuongezwa katika masanduku tofauti na idadi ya watu waliosajiliwa katika Daftari la Kudumu la Wapigakura Zanzibar na namba za fomu za idadi ya wapiga kura kufutwa na kuwekwa za kughushi tofauti na idadi ya watu waliosajiliwa katika kila kituo cha kupigia kura.



Alisema kutokana na hali hiyo Tume imeamua kufanya uchaguzi wa marudio na kuwataka wananchi wasubiri kutangazwa tarehe ya kufanyika kwa uchaguzi huo.
CHANZO: NIPASHE

2 comments:

  1. Eee hakuna uchaguzi ulioharibika wezi wakubwa hawa hawataki kushindwa wanahiari waitie nchi katika matatizo na kuwaongezea raia umaskini lakini yupo alie miliki mbingu na ardhi na vilivyomo atawatia mkononi tu hapo ndio mutajuwa nani muongo nani mkweli

    ReplyDelete
  2. Ni aibu na fedheha kubwa sana. Mungu BABA atusitiri na aibu ya kujitakia

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.