Habari za Punde

Dk Shein, Azindua Uwekaji Taa Uwanja wa Ndege Pemba na Kutoa Huduma Masaa 24 Uwanjani Hapo.

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                                                         07 Januari, 2016
---
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kukamilika kwa mradi wa uwekaji taa za kuongozea ndege zitakazowesha ndege kutua wakati wote katika kiwanja cha ndege cha Pemba ni kielelezo kingine cha hatua madhubuti zinazochukuliwa na Serikali kuimarisha miundombinu ya kiuchumi nchini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo jana huko katika kiwanja cha Ndege cha Pemba nje kidogo ya Mji wa Chake Chake, Dk. Shein aliwaeleza mamia ya wananchi waliohudhuria hafla hiyo kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejidhatiti kukiimarisha kiwanja hicho hadi kufikia kiwango cha kimataifa.

Dk. Shein alifafanua kuwa baada ya uwekaji wa taa kinachofuata ni hatua nyingine za kujenga jengo jipya la abiria na kuongeza urefu wa njia ya kurukia na kutua ndege kutoka kilomoita 1.5 sasa hadi kilomita 2.5.
Alibainisha kuwa utekelezaji wa kazi hizo utaanza si muda mrefu kwa kuwa Serikali imo katika hatua nzuri ya mazungumzo na Benki ya Maendeleo Afrika (ADB) kugharimia kazi hizo.

Dk. Shein alisema uwepo wa taa hizo sasa kutawezesha uwanja huo kutumika kwa saa 24 ambapo ndege zitaweza kutua na kuruka wakati wowote hivyo wasafiri hasa watalii wataweza kupanga safari zao wapendavyo.

Kwa hivyo aliwaeleza wananchi hao na wageni waliohudhuria hafla hiyo ambayo ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 52 ya Mapinduzi kuwa hatua za uimarishaji viwanja vya ndege Unguja na Pemba kunakwenda sambamba na juhudi za serikali za kuimarisha sekta ya Utalii.

Hivi sasa, Dk. Shein alieleza, kuwa idadi ya watalii wanaotembelea kisiwa cha Pemba inazidi kuongezeka siku hadi siku na miongoni mwa vivutio vyake ni ekolojia na hali ya jiografia yake.
“watalii wengi wanaokuja Pemba wanavutiwa na mazingira ya msitu wa Ngezi na fukwe ya Vumawimbi pamoja na ardhi ya vilima na mabonde na urahisi wa kuoina bahari kila baada ya kilomita chache” Dk. Shein alibainisha.

Alifafanua kuwa Utalii unaozingatia mazingira (eco-tourism) ndio unaoshika kasi ulimwanguni hivi sasa hivyo ametoa wito kwa wananchi wa Pemba kuhakikisha wanatunza mazingira ya kisiwa hicho ili kiendelee kubaki katika uhalisia wake.

Dk. Shein alisema mwenendo wa safari za kitalii Zanzibar unaonesha kuwa lengo la mpango wa serikali wa kuimarisha sekta ya Utalii kwa kufikisha idadi watalii 500,000 wanaotembelea Zanzibar ifikapo mwaka 2020 linaweza kuvukwa hadi kufikia watalii 700,000 mwaka huo.

Alifafanua kuwa idadi ya watalii waliotembelea Zanzibar mwaka 2010 walikuwa 132,836 na mwaka 2014 walitembelea watalii 311,801 ikiwa ni ongezeko la asilimia 134 katika kipindi cha miaka 4 wakati kati ya Januari na Novemba mwaka 2015 watalii 254,699 walitemebelea Zanzibar.

Akimkaribisha mgeni Rasmi, Naibu Waziri Miundombinu na Mawasiliano Issa Haji Gavu alitoa wito kwa wananchi kuthamini jitihada hizo za serikali kwa kulinda miundombinu ya uwanja huo.
Waziri huyo alisema serikali inauimarisha uwanja huo ili huduma zote muhimu ziweze kupatikana kwa ajili ya kuleta maendeleo. 

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano Dk. Juma Akil, akitoa maelezo ya kitaalamu kuhusu mradi huo alisema kukamilika kwa mradi huo kunadhihirisha kipimo cha ufinisi wa Mamlaka wa Viwanja vya Ndege Zanzibar ambayo ilianzishwa miaka mitano iliyopita.

Dk. Akil alibainisha kuwa mamlaka hiyo imeanza “kukua na kujijengea uwezo kuelekea kujitegemea yenyewe katika kutafuta na kukusanya rasilimali fedha, ubunifu na usimamizi wa miradi mikubwa”

Alitoa mfano kwa kueleza kuwa mafundi wa mamlaka hiyo kwa kushirikiana na wizara yake wamesimamia na kutekeleza mradi huo ambao umegharimu shilingi bilioni 1.4 kwa asilimia 98.

Dk. Akil alifafanua kuwa mradi huo wa uwekaji wa taa za kuongozea ndege ni mmoja kati ya miradi miwili iliyopangwa na Serikali ya kukiimarisha kiwanja cha ndege cha Pemba.

Aliutaja mradi mwingine kuwa ni kufanya Upembuzi Yakinifu na Usanifu wa Uendelezaji wa Jumla wa Uwanja huo ambao unatarajiwa kuanza mwaka huu.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu huyo kandarasi ya kuweka taa ilifanywa na kampuni ya Safegate kutoka Ujerumani wakati kazi za ujenzi (civil works) zikiwemo za uchimbaji mashimo ya nyaya za umeme na uwekaji wa uzio zimefanywa na kampuni ya SKARS Building Company Ltd ya Zanzibar. 

Sherehe hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali na Taasisi zake wakiwemo wafanyakazi wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano pamoja na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar.

Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.