STATE HOUSE
ZANZIBAR
OFFICE OF THE
PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Pemba
6.1.2016
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amekagua
maendeleo ya mradi wa huduma za mazingira na usafi wa miji Zanzibar (ZUSP)
iliyopo Pemba na kueleza kuwa hatua hizo ni miongoni mwa utekelezaji wa ahadi
alizowaahidi wananchi mwaka 2010 za kuimarisha miji mikuu ya Unguja na Pemba.
Dk. Shein alisema kuwa hatua za
utekelezaji wa mradi huo ni miongoni mwa juhudi za kuimarisha miji hiyo kwa
lengo la kuifanya kuwa ya kisasa hasa ikizingatiwa kuwa Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar imekopa fedha nyingi kutoka Benki ya dunia kwa ajili ya mradi huo.
Dk. Shein alisema kuwa Serikali ilikopa
kutoka Benki ya Dunia jumla ya Dola milioni 38 sawa na Tsh. Bilioni 56 kwa
hesabu za fedha za mwaka 2011 kutekeleza mradi huo ambapo kwa upande wa Pemba
utafanyika katika miji ya Wete, Chake na Mkoani.
Akizungumza na wananchi kwa nyakati
tofauti mara baada ya kutembelea maeneo ya miradi hiyo huko Mkoani na Chake
Chake Pemba, Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
anayoiongoza yeye itaendelea kufanya kazi zake za kuwapelekea wananchi huduma muhimu
za maendeleo.
Dk. Shein aliwaeleza wananchi kuwa mradi
huo kwa upande wa Unguja unahusisha uimarishaji wa Mji Mkongwe pamoja na Ngambo
kwa kuweka taa za jua za barabarani kuelekea uwanja wa ndege, Amani na sehemu
nyengine za mji hatua ambayo itauweka mji katika mazingira mazuri pamoja na kuupamba.
Ujenzi huko pia, utahusisha ujenzi wa
ukuta wa Forodhani pamoja na ujenzi wa barabara mbili katika eneo hilo ambapo
tayari ukuta wa bahari umeanza kujengwa.
Katika maelezo yake, Dk. Shein aliwaeleza
wananchi kuwa mkopo huo si ruzuku wala msaada na fedha hizo ni nyingi hivyo
wananchi wanatakiwa kushirikiana na serikali yao kwa kuhakikisha kuwa inatunzwa
na inaendelezwa huku wakitambua kuwa kila mmoja anachangia kwa njia tofauti
katika mkopo huo.
Aidha, Dk. Shein alisema kuwa mradi huo
pia, unahusisha kuyatoa maji ya mvua na bahari katika maeneo ya viwanja vya
Mnazi Mmoja, ujenzi wa misingi mikubwa ya kutoa maji katika maeneo ya Mpendae
kwa Biti Amrani na Sebleni.
Mapema Mkurugenzi wa Baraza la Mji wa
Mkoani Issa Juma Othman alimueleza Dk. Shein kuwa kwa upande wa Mji wa Mkoani,
mradi huo unahusisha maeneo makubwa matatu ambayo yanajumuisha ukarabati mkubwa
wa Ofisi ya Baraza la Mji Mkoani, Ujenzi wa njia za vidaraja katika eneo la mji
wa Mkoani pamoja na ujenzi wa mitaro ya maji katika maeneo ya Mji wa Mkoani.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa miradi hiyo
mitatu inatarajiwa kugharimu jumla ya Tshs. Milioni 755 huku akieleza kuwa miradi
hiyo inatekelezwa kwa kipindi cha mwaka mmoja kutoka tarehe 01 April,2015 na kutarajiwa
kukamilika mwezi April mwaka huu.
Alieleza kuwa mradi wa ujenzi wa vidaraja katika Mji wa
Mkoani unahusisha ujenzi na ukarabati wa njia za vidaraja 17 ambapo tano kati
ya hizo ni ukababati na 12 ni ujenzi mpya.
Nae mwakilishi wa Kampuni ya ZECCON
COMPANY LTD Ali Mbarouk alieleza kuwa gharama za miradi hiyo kwa upande wa mji
wa Mkoani imeongezeka kutoka Tshs 755 hadi Tshs. Bilioni 1 kutokana na marekebisho
mbalimbali ya lazima yaliyofanywa kqtika miradi hiyo..
Akiwa katika mji wa Chake Chake, Dk.
Shein alitemebela ujenzi wa vidaraja huko Chachani-Minazini pamoja na kuangalia
ujenzi wa jengo la Ofisi ya Baraza la Mji Chake ambalo ni la ghorofa mbili huku
akisisitiza ujenzi wa ofisi hizo uzingatie watu wenye ulemavu wa miguu pamoja
na wazee.
Wakati huo huo, mara baada ya kuzungumza
na wananchi Dk. Shein alielekea huko Kisiwani Wesha kwa ajili ya kuangalia
ujenzi wa chinjio jipya la Ng’ombe la Baraza la Mji Chake na kupata maelezo juu
ya chinjio hilo ambalo hadi kumalizika ujenzi wake litagharimu Tshs milioni
166.
Chinjio hilo linalojengwa na Kampuni ya
NOWE INVESTMENT LMT ya Dar-es-Salaam ambapo hadi sasa ujenzi wake umeshafikia
asilimi 90 linatarajiwa kukamilika mwezi April mwaka huu.
Dk. Shein yuko kisiwani Pemba kwa ziara
ya kiserikali ikiwemo kuangalia miradi ya maendeleo pamoja na kuzindua miradi
mbali mbali iliyomo katika ratiba ya shamrashamra za sherehe za miaka 52 ya
Mapinduzi ya Zanzibar.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024
2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment