Habari za Punde

Wakulima wa Karafuu waelezea kuridhishwa na huduma kutoka ZSTC

 Mkurugenzi Fedha wa ZSTC akitoa ufafanuzi kwa Wandishi wa Habari juu ya hali ya manunuzi ya karafuu.
  Mkulima wa karafuu Wilaya Mkoani Salum Suleiman Said akizungumza na Wandishi wa Habari juu ya namna Shirika la ZSTC linavyowahudumia Wakulima katika vituo vya manunuzi.

Wakulima na Mpasishaji wakiangalia karafuu kwa ajili ya kupasishwa  katika kituo cha ununuzi cha Wete.Ø Wafurahishwa na Malipo kwa wakati

Na Majid Omar Najim

Wakulima wa zao la karafuu visiwani Zanzibar wameelezea  kuridhishwa na huduma wanazozipata kutoka Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC) katika vituo vya ununuzi wa karafuu, ikiwemo kulipwa fedha taslimu pale wanapouza karafuu zao.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Watendaji Wakuu wa Shirika hilo waliofanya ziara maalum kuangalia namna zoezi la ununuzi wa karafuu linavyoendelea katika msimu wa 2015/2016, Wakulima hao wamesema wamekuwa wakilipwa fedha zao taslimu bila kukopwa.

Salum Sleiman Said ambae ni Mkulima maarufu wa zao hilo Wilaya ya Mkoani- Mkoa wa Kusini Pemba alisema tangu aanze kuuza karafuu katika Shirika hilo amekuwa akilipwa fedha zake zote hapo hapo na hajawahi kukopwa jambo ambalo linamuwezesha kuifanya vyema biashara hiyo.

 “Leo hapa nimeleta gunia 80, nimelipwa fedha zangu taslimu, wiki mbili nyuma nilileta gunia 70, pia nililipwa fedha zangu zote,” Alisema Mkulima huyo huku akionyesha risiti ya malipo yake.


Nae Mkulima kutoka Finya, Wilaya ya Wete, Ramadhan Hamad Yussuf alisema hakufikiria kama Shirika lingeweza kununua karafuu zote za msimu kwa fedha taslim kutoka kwa Wakulima kutokana na msimu kuwa mkubwa.

“Leo nimeleta gunia 40 hapa, nimelipwa fedha zangu zote, nashukuru sana, naona Shirika lilijiandaa vizuri kunua karafuu zetu. Alifahamisha Mkuliama huyo wa Wete.

Nadhani kuna watu wana malengo yao wenyewe. Hivyo kufikia malengo yao huamua kulipaka matope shirika”,alibainisha.

Alisema katika kituo chao cha Wete wanachouza karafuu hajawahi kumsikia mkulima yoyote akilalamika kuhusu malipo ama karafuu zake kukopwa na Shirika la ZSTC.

Akizungumzia huduma nyengine wanazopata kutoka Shirika la ZSTC Zuhura Ali Nassor Mkulima kutoka Wilaya ya Chake Chake alisema wamekuwa wakipata ushirikiano mzuri kutoka kwa Watendaji wa Shirika jambo ambalo limepelekea Wakulima kuuza karafuu nyingi msimu huu.

“Sio tu kutulipa kwa wakati, lakini pia tumekuwa tukipatiwa huduma za mikopo, usafiri na ulinzi. Shirika pia limetukatia bima kwa wanaopata ajali wakati wa uchumaji wa karafuu.” Alibainisha Bi. Zuhura.

 Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la ZSTC, Afisa Mdhamini wa Shirika hilo Abdalla Ali Ussi amewashukuru na kuwapongeza wakulima wa karafuu kwa namna wanavyoshirikiana na Shirika katika kuuza karafuu zao.

“Serikali inafahamu kazi mnayofanya ya kuimarisha zao la karafuu na kuuza Serikalini, inawathamini sana ndio maana ipo karibu sana na nyinyi, niinawaomba musiwe na wasi wasi wowote Serikali kupitia Shirika la ZSTC ipo pamoja na nyinyi.” Alifahamisha Afisa Mdhamin.

Alisema kuwa suala la Shirika kuwakopa Wakulima halipo na wala halitokuwepo na wala halina mpango wa kushusha bei ya karafuu katika katika ya msimu.

Mdhamin aliwahakikishia Wakulima na wafanyabiashara wa zao la karafuu kuwa Shirika lina uwezo na nguvu za kutosha za kununua karafuu zote kwa fedha taslim.

Ameongeza kuwa kutokana na mazingira mazuri yaliyowekwa na shirika kwa wakulima, suala la magendo limepungua kwa kiasi kikubwa ambapo ni gunia 47 tu za magendo ndizo zilizokamatwa mpaka sasa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Fedha wa Shirika hilo, Ismail Omar Bai alisema Shirika lina fedha za kutosha kununulia karafuu zote pamoja na kutoa huduma nyengine kwa wakulima, hivyo amewataka wakulima kupeleka karafuu zao katika vituo bila ya wasi wasi wowote.

 Alisema hadi tarehe 26/01/2016 Shirika  limenunua jumla ya tani 5,100.3500 kwa fedha taslim 71, 482,010,500.00, Pemba tani 4,841,810.00 kwa fedha taslim 67,878,290,500.00 na Unguja tani 258,540.00 kwa fedha taslim 3,603, 720,000.00 na hakuna mtu aliyokopwa au kucheleweshewa malipo.

“Hakuna Mkulima anaelidai Shirika na wala aliyepewa risiti akaambiwa aje baada ya wiki mbili kama yupo ajitokeze. Tunajua biashara ya karafuu inahitaji fedha za uchumishaji na huduma nyengine hivyo hatuwezi kumkopa mkulima kwani kumkopa ni kumrudisha nyuma”. Alisema Mkurugenzi Fedha wa ZSTC.

Ameongeza kuwa ili kuwawezesha wakulima kufikia malengo yao Shirika limekuwa likitoa mikopo  isiyo na riba kwa wakulima wa zao hilo la karafuu muhimu awe ametimiza masharti ya mkopo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.