Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwa katika picha ya pamoja na Uongozi wa Jumuiya ya Wide Zanzibar uliofika Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar kujitambulisha rasmi.
Kulia ya Balozi Seif ni Mkurugenzi na muanzilishi wa Wide Zanzibar Bibi Rehema Mwinyi, Mjumbe wa Jumuiya hiyo Issa Salum Ali na kushoto ya Balozi Seif ni Mshauri wa Wide Zanzibar Bwana Said Alawy.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Mkurugenzi na muasisi wa Jumuiya iliyojikita kuelimisha jamii katika masuala ya maendeleo na ustawi wa Jamii Zanzibar { Wide } Bibi Rehema Mwinyi alisema wakati umefika kwa vijana kujitambua na kuacha kuchezewa kiakili kunakopelekea kujiingiza katika wimbi la matatizo ya kimaisha.
Alisema kutokana na mabadiliko ya mfumo wa kimaisha uliopo hivi sasa Ulimwenguni Vijana hasa wale wanaopata elimu wanapaswa kutumia taaluma yao katika kutafuta maisha kupitia mfumo wa ujasiri amali badala ya kusubiri ajira chache zilizopo Serikalini.
Bibi Rehema Mwinyi alieleza hayo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiuongoza Ujumbe wa Viongozi Watatu wa Jumuiya hiyo walipofika kujitambulisha rasmi Ofisini Vuga Mjini Zanzibar.
Alisema mradi wa kuleta shukrani kwa jamii kufuatia wanajumuiya hiyo kufaidika na misaada ya Serikali katika kuwaandaa Kitaaluma umelenga kuyajengea uwezo wa kiujasiri amali makundi ya Wanawake na Vijana hapa Zanzibar.
Alisema wapo Vijana na akina mama wengi mitaani waliobarikiwa kuwa na vipaji vya kujiendesha kimaisha lakini wanashindwa kuvitumia ipasavyo kutokana na ufinyu wa Taaluma pamoja na mitaji ya kuanzia miradi wanayoamua kuianzisha.
Mkurugenzi huyo wa Wide Zanzibar Bibi Rehema alieleza kwamba mradi huo umelenga kuanzisha matamasha kwa ajili ya kuibua vipaji hivyo katika Nyanja mbali mbali ili kuwatengeneza kwa faida yao ya baadae.
Naye Mshauri wa Jumuiya ya Wide Zanzibar Bwana Said Alawi alisema ipo mipango ya muda mrefu ya Jumuiya hiyo iliyoandaliwa katika muundo wa kutoa elimu ya kuliendeleza bonde la Uwanja wa Farasi liliopo Kwahani Mjini Zanzibar badala ya kuwa eneo hatarishi.
Bwana Alawi alisema Vikundi vya wajasiri amali vitapatiwa taaluma katika kuona vinashiriki kwenye usafishaji pamoja na upandaji miti kwenye Bonde hilo lengo likiwa kulirejeshea hadhi yake ya asili ya kuwa sehemu za Burdani.
“ Eneo hilo lilipata umaarufu wa kuitwa uwanja wa Farasi kutokana na watu wengi kulitumia kwa burdani ya michezo ya Farasi miaka mingi iliyopita ”. Alisema Mshauri huyo wa Jumuiya ya Wide Zanzibar.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Jumuiya ya Wide inapaswa kuendelea kupiga kelele katika kuwaongoza Vijana njia yenye muelekeo sahihi wa maisha yao.
Balozi Seif alisema kazi zinazotekelezwa na Jumuiya hiyo ikiwemo taaluma ya kuwajengea uwezo wa Ujasiri amali Vijana na Wanawake itaisaidia Serikali katika mapambano yake kwenye sekta ya ajira.
Akigusia suala la mazingira ambalo limo ndani ya mpango kazi wa Jumuiya hiyo Balozi Seif alisema kwamba mazingira yaliyopo nchini hivi sasa yamechafuka katika maeneo mengi kutokana na usimamizi mbovu wa watendaji wa Halmashauri za Wilaya pamoja na Serikali za Mitaa.
Alisema ipo tabia ya baadhi ya watu kutafuta nafasi ndogo zilizomo ndani ya mitaa na kuzitumia katika kuanzisha miradi inayochafua mazingira na hatimae kusumbua jamii.
No comments:
Post a Comment