Habari za Punde

Kitumieni ZLSC kupata ushauri wa kisheria

Na Haji Nassor, Pemba
Viongozi na wanachama wa Jumuiya za kiraia Kisiwani Pemba, wametakiwa kukitumia Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ZLSC Tawi la Pemba, ili kupata ufafanuzi wa mambo kadhaa ya kisheria, kabla ya kufanya maamuzi ya kisheria ndani ya Asasi zao.
Ushauri huyo umetolewa kwa nyakati tofauti na Afisa Mdhamini Wizara ya Katiba na Sheria Pemba , Ndg.Omar Khamis Juma alipokuwa akifungua mafunzo ya elimu ya uraia kwa viongozi hao yalifanyika Chakechake.
Alisema lazima kila jambo wanalolifanya liwe kwa mujibu wa sheria na hilo kama hawalifahamu ufumbuzi wake, basi wazitumie taasisi kadhaa zilizopo kisiwani Pemba ikiwa ni pamoja na Kituo hicho.
Mdhamini huyo alisema, kazi zinazofanywa na kituo hicho kwa taasisi nyenginez zinahitaji gharama kubwa ya fedha, ambapo ZLSC hutoa bila ya malipo msaada wa kisheria kwa makundi yote ndani ya jamii.
Hivyo amewataka viongozi wa asasi za kiraia kuwa karibu na kituo hicho ambacho kipo kisheria, ili kuyapatia ufumbuzi mambo kadhaa wanayoyafanyia kazi ili kuyapatia uwelewa ikiwa ni pamoja na katiba na sheria za vyama vya ushirika.

“Jamani kama mtakuwa makini kukitumia Kituo cha Huduma za Sheria, basi hata mtakayofanya kwa mujibu wa kazi zenu hamtakuwa na ugomvi na mtu, maana sheria mnazifahamu’’,alifafanua.
Katika hatua nyengine Afisa Mdhamini huyo wa Wizara ya katiba na Sheria Omar Khamis Juma, alisisitiza haja kwa washiriki wa mafunzo hayo kuitumia nafasi hiyo, ili kujifunza mambo kadhaa.
Mapema Mratibu wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ZLSC tawi la Pemba Fatma Khamis Hemed, alisema asasi za kirais zinayonafasi kubwa ya kuishawishi serikali juu ya kufanya au kuwacha kufa jambo.
Akiwasilisha mada ya mgawanyo wa madaraka mratibu wa mafunzo hayo Mohamed Hassan Ali, alisema suala hilo hailiihusu serikali kuu pekee, hata ndani ya asasi za kiraia.
Kwa upande wake afisa mipango wa Kituo cha Huduma za sheria Pemba, Khalfan Amour Mohamed, kwenye mada ya utawala bora, utawala wa sheria na demokrasia, alisema dhana hiyo lengo ni kuona mamlaka yote yako kwa wananchi.
“Lakini hata ndani ya asasi zenu, suala la demokrasia linahitajika, maana ili jumuia ihesabike kuwa inaendeshwa kisheria, mamlaka yawe kwa wanachama’’,alifafanua.

Katika mafunzo hayo ya siku mbili, mada kadhaa zilijadiliwa ikiwa ni pamoja na uraia, katiba ya Zanzibar, mgawanyo wa madaraka ambapo ni mfululizo wa Kiuto cha Huduma za Sheria Zanzibar ZLSC kuipatia elimu ya sheria na haki jamii.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.