Habari za Punde

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) hatutambui kujitoa kwa mgombea Ubunge wa CUF Jimbo la Kijitoupele Zanzibar

Tume  ya Taifa ya Uchaguzi (NEC),imesema haitambui  kujitoa kwa Chama cha Wananchi (CUF),katika uchaguzi wa Mbunge  Jimbo la Kijitoupele hapa Zanzibar unaotarajiwa kufanyika Jumapili licha ya kuwa  Tume imepokea barua rasmi toka kwa uongozi wa Chama hicho.
Mkurugenzi wa uchaguzi wa Tume ya Taifa Bw Kailima Ramadhani amesema Tume imefikia maamuzi hayo kutokana na ukweli kuwa barua hiyo ya CUF imechelewa huku maandalizi ya uchaguzi huo yakiwa yamekamilika na ni Wananchi tu kwa sasa Wanasubiriwa kwenda kupiga kura.
Aidha Bw Kailima ameeleza kuwa,kwa kuwa karatasi za kupigia kura zilishachapishwa na kuwasili hapa nchini tayari kwa uchaguzi huo,zitaendelea kuwa na picha za Wagombea wa CUF hata kama wamejitoa katika uchaguzi huo.
Awali,wajumbe wa Tume ya Taifa ya uchaguzi  wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Tume Jaji mstaafu Hamid Mahamood Hamid walitembelea katika vituo mbalimbali  vya kupigia kura katika Jimbo la Kijitoupele ili kujiridhisha na maandalizi ya uchaguzi huo kabla ya uchaguzi kufanyika jumapili.
Tume ilibaini kuwepo kwa baadhi ya kasoro ndogondogo katika baadhi ya vituo vya kupigia kura ikiwa ni pamoja na kubanduliwa kwa karatasi zenye majina ya wapiga kura,mfano katika kituo cha Skuli ya sekondari Kinuni.
Jimbo la Kijitoupele lina jumla ya Wapiga kura wapatao 17,274 na vituo vipatavyo 53 vitatumiwa na wapiga kura ili kumchagua mbunge wa Jimbo la Kijitoupele siku ya Jumapili.
Sambamba na Uchaguzi wa ubunge katika Jimbo la Kijitoupele, marudio ya uchaguzi mkuu wa Zanzibar Oktoba 25,2015 ambayo matokeo yake yalifutwa uatafanyika Jumapili hiyo pia.
Uchaguzi katika jimbo la Kijitoupele uliahirishwa mwaka jana kutokana na hitilafu ndogondogo zilizojitokeza katika karatasi za kupigia kura,kabla ya kufutwa kwa matokeo ya Uchaguzi mkuu wa Zanzibar uliofanyika Oktoba 25,2015.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.