Habari za Punde

China Kuiunga Mkono Zanzibar Uthibitisho wa Muendeleo wa Uhusiano.

Jaji wa Mahakama Kuu ya China Mheshimiwa Zhang Giannan akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipofika nyumbani kwake kwa mazuungumzo ya kuimarisha uhusiano akiuongoza Ujumbe wa Majaji sita wa Mahakama Kuu ya China.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akibadilishana mawazo na Jaji wa Mahakama Kuu ya China Mheshimiwa Zhang Giannan nyumbani kwake Kama nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Baadhi ya Majaji wa Mahakama Kuu ya Jamuhuri ya Watu wa China wakifuatilia mazungumzo kati ya Kiongozi wao Jaji  Zhang Giannan na Balozi Seif huko kama.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi  akipokea zawadi maalum kutoka kwa Jaji wa Mahakama Kuu ya China Mheshimiwa Zhang Giannan mara baada ya kumaliza mazungumzo yao.
Balozi Seif Kati kati aliyevaa suti nyeuzi akiwa katika picha ya pamoja na Ujumbe wa Majaji wa Mahakama Kuu ya Jamuhuri ya Wat wa china uliopo nchini kwa ziara ya kutathmini uhusiano wa kihistoria kati ya Tanzania na China.Kulia ya Balozi Seif ni Kiongozi wa Ujumbe huo Jaji wa Mahakama Kuu ya China Mheshimiwa Zhang Giannan na kushoto ya Balozi Seif ni Balozi Mdogo wa China aliyepo hapa Zanzibar Bwana Xie Yun Liang.
                                       Picha na – OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kitendo cha Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China kuonyesha muelekeo wa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar ni uthibitisho wake wa muendelezo wa uhusiano iliyokuwa nao kati yake na Zanzibar.

Balozi Seif alisema hayo nyumbani kwake Kama nje kidogo ya Mji wa Zanzibar wakati akizungumza na Jaji wa Mahakama Kuu ya China Mheshimiwa Zhang Giannan aliyeuongoza ujumbe wa Viongozi sita wa Mahakamu Kuu ya China.

Balozi Seif alisema China ni nchi ya kwanza iliyoamua kuiunga mkono Zanzibar mara tu baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa marejeo uliofanyika Tarehe 20 Machi mwaka huu katika hali ya amani na utulivu.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliipongeza Nchi hiyo kubwa ya Bara la Asia kwa jitihada zake ilizochukuwa katika kuweka mfumo maalum wa utoaji wa mafunzo kwa watendaji wa Taasisi za Umma kwa nchi zinazoendelea kiuchumi ikiwemo Tanzania.

Balozi Seif alisema utaratibu huo kwa kustawisha uwajibikaji na uchumi umesaidia zaidi watumishi wanaopata mafunzo nchini China kuwa na uwezo wa utekelezaji wa majukumu yao kitaaluma zaidi.

“Tumefarajika sana jinsi ya watendaji wa Baraza la Wawakilishi, Waheshimiwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wanavyoitumia fursa hiyo ya mafunzo kwa kuwajibika kitaaluma wakati wa kuwatumikia wananchi ”. Alisema Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimuhakikishia Jaji Mkuu huyo wa Mahakama Kuu ya China na Ujumbe wake kwamba uhusiano uliopo wa kihistoria katika ya pande hizo mbili utadumishwa zaidi kwa faida ya wananchi wake.

Mapema Jaji wa Mahakama Kuu ya Jamuhuri ya Watu wa Chima Mheshimiwa Zhang Giannan akiambatana pia na Balozi Mdogo wa China aliyepo hapa Zanzibar Bwana Xie Yun Liang alisema wananchi wa taifa hilo la Bara la Asia wanafurahia kuona uhusiano wa Nchi hiyo na Zanzibar bado unaendelea kudumu.

Jaji Giannan alieleza kwamba Mikakati ya China katika hatua yake ya baadaye imepanga kuimarisha zaidi uhusiano wake na Tanzania na Zanzibar kwa ujumla katika Sekta za Utamaduni, sanaa pamoja na Michezo.

Alisema eneo hilo kwa sasa ni muhimu katika dhana ya kuwaunganisha Vijana ambao ndio kundi kubwa katika jamii kuelekeza nguvu zao katika sekta hizo zenye nafasi pana ya kutoa fursa za kujitegemea badala ya kusubiri Serikali ambazo tayari zimekuwa na ufinyu wa nafasi za ajira.

Ujumbe huo wa Mahkama Kuu ya Jamuhuri ya Watu wa China upo Nchini kufanya ziara ya kutathmini maendeleo ya ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya nchi hiyo na Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo pia Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.