Habari za Punde

Zantel yatoa msaada wa kompyuta 21 na huduma ya intaneti bure kwa vyuo vya Ualimu Zanzibar.


Zanzibar, 19, Aprili-2016: Kampuni ya simu inayoongoza visiwani Zanzibar, Zantel imetoa msaada wa kompyuta  21 na huduma ya intaneti bure kwa vyuo saba vya walimu pamoja na shule ili kuboresha na kukuza  mfumo wa elimu kupitia  mafunzo ya  habari na teknolojia ya maswasiliano .
Msaada huo wenye thamani ya shilingi milioni 34 umetolewa wiki moja tu baada ya kampuni hiyo kuzindua mtandao wa kasi wa 4G pamoja na kutanua upatikanaji wa mtandao upande wa bara.
Kompyuta hizo ambazo zimeunganishwa na mtandao wa inteneti kwa muda wa miezi mitatu zitasaidia kukabiliana na uhaba wa walimu wenye ujuzi  katika teknolojia ya mawasiliano visiwani Zanzibar.
Vyuo na shule  zitakazo pokea msaada huo ni pamoja na chuo cha biashara cha Zanzibar (Unguja), shule ya Chasasa (Pemba), chuo cha taifa cha Ualimu (Unguja),Chuo cha Ualimu  Kiembe Samaki (Unguja),chuo cha ualimu cha  Michakaeni (Pemba), chuo ch Ualimu ( Unguja) na chuo cha  Ualimu Kitogani (Unguja).
Akizungumza wakati wa  makabidhiano hayo,  Afsa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya simu ya Zantel, Bwana Benoit Janin alisema lengo la Zantel ni kushirikiana na serikali kwa lengo la kukuza na kuboresha elimu ya teknolojia na mawasiliano na  kusaidia vyuo vya ualimu vinayotoa mafunzo hayo ili kuongeza ufanisi katika ufundishaji wao.
'Ni matumaini yetu mchango huu utasaidia kuendeleza elimu ya teknolojia na mawasiliano na kuwanufaisha walengwa kwa kuwawezesha kutekeleza majukumu yao na kuongeza  wataalamu kwenye taifa' alisema Janin.
Akizungumza wakati wa tukio hilo,  Mkurugenzi wa bodi wa Zantel na Afsa Mtendaji wa Millicom Africa, Bi Cynthia Gordon alisema walimu ndio msingi wa maendeleo kwenye taifa na ndio maana Zantel imewapa kipaumbele katika miradi yake ya kijamii.
'Daima Zantel tumekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha tunaboresha sekta ya elimu kwa wazanzibari na kama tunavyojua elimu ya teknolojia na mawasiliano ni muhimu kwa dunia ya sasa ' alisema Bi Gordon.
Katika hotuba yake, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mheshiwa Riziki Pembe Juma, ameipongeza kampuni ya  Zantel kwa jitihada  zake inayofanya kwa kushirikiana na serikali katika kukuza na kuboresha elimu visiwani Zanzibar.
'Ili kutoa elimu bora kwa walimu wa teknolojia ya mawasiliano wa ngazi zote ni muhimu kuhakikisha mafunzo ya komputa yanajumuishwa kwenye mtaala wa vyuo vya elimu ili kuwajengea uwezo walimu katika kufundisha wanafunzi' alisema Mheshimiwa Riziki Pembe Juma.

Zantel imekuwa ikitoa michango mbalimbali kwenye sekta ya elimu visiwani Zanzibar ikiwemo kusaidia ununuzi wa vitabu kwa maktaba kuu ya Zanzibar  na pia kutoa msaada kwenye  shule za msingi kama vile Kisiwandui na pia ukarabati wa madarasa katika shule ya Mikanyageni mkoani Pemba.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.