Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Ali Mohamed Shein akitoa Risala ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhan kwa Wananchi na Waislamu wote nchini katika Risala hiyo amewataka Wananchi kuwa Amani na Utulivu na kuwaombea kwa Mola wetu kuwajaalia Rehma na baraka za Mwezi Mtukufu wa Ramadhan pia amewataka kufanya ibada kwa wingi katika kipindi chote cha mwezi huu,(Picha na Ikulu.)06/06/2016
STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 6.6.2016
SERIKALI ya Mapinduzi ya
Zanzibar itaongeza juhudi za kuwafuatilia wafanyabiashara wenye tabia ya
kupandisha bei za bidhaa bila ya sababu za msingi, jambo ambalo linaathiri
hatua ya Serikali kutoa unafuu wa ushuru wa bidhaa muhimu kwa wafanyabiashara hao
hapa nchini.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed
Shein aliyasema hayo, Ikulu mjini Zanzibar katika risala aliyoitoa kwa wananchi
kupitia vyombo vya habari katika kuukaribisha Mwezi mtukufu wa Ramadhani mwaka
huu.
Katika risala hiyo, Alhaj Dk. Shein alisema kuwa inasikitisha kuona kuwa,
licha ya kuwa Uislamu unahimiza kuoneana huruma, lakini wapo wafanyabiashara
ambao huchukua fursa ya kupandisha bei bidhaa zao katika mwezi wa Ramadhani,
hasa zile bidhaa za chakula muhimu ambazo Serikali hupunguza ushuru ili kuwapa
nafuu wananchi.
“Nafahamu malalamiko yaliopo hivi sasa, ambapo wafanyabiashara walipandisha
bei za bidhaa kwa kisingizo cha uchaguzi na hadi hii leo bei za bidhaa hizo
bado ziko juu”,alisema Alhaj Dk. Shein.
Aidha, Alhaj Dk. Shein alisema kuwa upandishaji wa bei usio na msingi
unakwenda kinyume na malengo ya Serikali ya kuanzishwa kwa biashara huru yenye
ushindani.
Hata hiyo, Alhaj Dk. Shein alisisitiza kuwa Serikali itaendelea
kushirikiana na wafanyabiashara na itahakikisha kuwa bidhaa zote muhimu
zinazohitajika na kutumika zaidi katika mwezi wa Ramadhani zinapatikana wakati
wote na bila ya usumbufu wowote.
Kwa vile mwezi wa Ramadhani ndio Qur-ani iliteremshwa kwa Mtume Muhammad
(SAW), Alhaj Dk. Shein alieleza kuwa bidii inahitajika katika kuisoma na
kuifahamu Qur-an sambamba na kuhimizana katika kuzitekeleza Sala za Fardhi na
Sala za Sunna mbali mbali hasa nyakati za usiku.
Alhaj Dk. Shein alisisitiza wajibu wa kuishi kwa kumfanya Mtume Muhammad
(S.A.W) kuwa mfano katika kutekeleza ibada mbali mbali katika mwezi wa
Ramadhani ikiwemo kutoa sadaka, bidii ya kumtaja Allah, kufanya istighfari,
kukaa Itikafu, kuharakisha kufungua wakati unapofika pamoja na kutekeleza sunna
ya kula daku.
Pamoja na hayo, Alhaj Dk. Shein alieleza kuwa ni muhimu ikafahamika kwamba
hivi sasa teknolojia imevisogeza vishawishi vingi vinavyoweza kuibatilisha
saumu karibu na nafsi ambapo miongoni mwa vishawishi hivyo ni pamoja na mitandao
ya simu na intaneti.
Alisema kuwa bila ya kujijua, mtu anaweza kujikuta anafanya makosa pale
anapoangalia mitandao yenye mambo yasiopendeza, hasa katika Mwezi Mtukufu wa
Ramadhani.
Hivyo, Alhaj Dk. Shein alitoa wito kwa Mashekhe kuendelea kutoa taaluma juu
ya umuhimu wa matumizi bora ya mitandao na kwa pamoja kuhimizana juu ya umuhimu
wa kuunga mkono juhudi za Serikali za kushajihisha matumizi bora ya mitandao ya
simu na kompyuta kwa matumizi ya mitandao ya intaneti.
Alisema Serikali itaendelea kuchukua tahadhari na hatua mbali mbali kama
ilivyotangazwa na Wizara ya Afya katika
kujikinga na maradhi ya miripiko licha ya kuwa uamuzi huo unaweza kuathiri
utamaduni wa kufutarishana unaoandaliwa na wananchi, taasisi za Serikali na
binafsi katika kipindi cha Ramadhani.
Katika risala hiyo, Alhaj Dk. Shein aliiagiza Wizara ya Ardhi, Maji,
Nishati na Mazingira pamoja na Mamlaka ya Maji ya Zanzibar (ZAWA) zifanye kila
jitihada ili iwapatie wananchi maji safi na salama, kwa kutumia magari katika
sehemu zote ambazo zina upungufu wa maji
safi na salama.
Alhaj Dk. Shein alimtaka Mkurugenzi Mkuu wa ZAWA kuhakikisha kwamba kazi
hiyo ya kuwapatia wananchi maji inafanyika kwa mafanikio makubwa na kutoa wito
kwa wananchi kushirikiana na Mamlaka hiyo ili kufanikisha shughuli hiyo.
Sambamba na hayo, Alhaj Dk. Shein aliwataka
wananchi kufuata mafundisho ya Qur-an na Hadithi za Mtume Muhammad (S.A.W)
katika kuhakikisha kuwa wanafanya vitendo vyema, wanaimarisha mapenzi na wanaepuka
chuki na hasama miongoni mwao.
“Ni wajibu wetu kumshukuru Mwenyezi Mungu muweza kwa kuiweka nchi yetu
katika hali ya amani na salama na sote tunafahamu kuwa sisi ni wamoja na kwa
hivyo, chuki na husda hazina tija wala hazina nafasi katika kuijenga Zanzibar
ya leo”,alisisitiza Alhaj Dk. Shein.
Alhaj Dk. Shein aliwahakikishia wananchi kuwa Serikali zote mbili Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,
zitaendelea kuhakikisha kuwa nchi inaendelea kuwa ya amani na salama.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment