Habari za Punde

Dk Shein akutana na Balozi wa Afrika Kusini Ikulu

 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Ali Mohamed Shein akisalimiana na Balozi wa Afrika ya  Kusini katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Thamsanga Dennis Msekelu leo alipofika Ikulu Mjini Zanzibar,[Picha na Ikulu.] 21/06/2016.
 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Ali Mohamed Shein akizungumza na Balozi wa Afrika ya  Kusini katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Thamsanga Dennis Msekelu leo alipofika Ikulu Mjini Zanzibar,[Picha na Ikulu.] 21/06/2016.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Ali Mohamed Shein akifuatana na Balozi wa Afrika ya  Kusini katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Thamsanga Dennis Msekelu baada ya mazunguzo yao leo alipofika Ikulu Mjini Zanzibar,[Picha na Ikulu.] 21/06/2016.
STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                     21  Juni, 2016

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema msingi madhubuti wa uhusiano kati ya Tanzania na Afrika Kusini unawapa fursa zaidi wananchi wa nchi mbili hizo kuimarisha na kupanua maeneo mengi ya uhusiano na ushirikiano kati yao.

Akizungumza na Balozi wa Afrika Kusini nchini Tanzania Mheshimiwa Thamsanqa Dennis Msekelu ofisini kwake Ikulu leo, Dk. Shein alisema uhusiano huo ambao umejengwa na waasisi wa vyama vya ukombozi vya nchi hizo umewezesha Serikali na wananchi wa Tanzania na Afrika Kusini kushirikiana na kuzidi kuwa karibu siku hadi siku.

“Sisi ni ndugu tulioshirikiana bega kwa bega katika kipindi cha miaka mingi ya mapambano dhidi ya ukoloni na ubaguzi ili kuleta ustawi wa watu wetu. Tuna kila sababu ya kuimarisha udugu na urafiki wetu” Dk. Shein alieleza.

Aliongeza kuwa kuimarisha uhusiano kati ya nchi hizo ni sehemu ya kuendeleza utamaduni wa uhusiano mwema miongoni mwa watu wa bara la Afrika.

Alibainisha kuwa chini ya uhusiano na ushirikiano huo nchi hizo zimekuwa zikishirikiana katika nyanja mbalimbali ikiwemo uchumi na uwekezaji ambapo Afrika Kusini imekuwa mmoja ya wawekezaji wa muda mrefu nchini Tanzania.


“Wafanyabiashara wa Afrika Kusini wamekuwa miongoni mwa wawekezaji wanaoshiriki katika kuendeleza uchumi wetu ambapo hapa Zanzibar kuna zaidi ya hoteli 12 za kitalii” Dk. Shein alieleza.

Hata hivyo pamoja na kutambua uwekezaji huo katika sekta ya utalii, Dk. Shein alimueleza balozi huyo kuwa kuna haja ya wawekezaji kutoka nchi hiyo kutumia fursa nyingine za uwekezaji zilizopo ikiwemo sekta ya uvuvi wa bahari kuu ambao haijavutia uwekezaji mkubwa hadi sasa.

Dk. Shein alitumia fursa hiyo kupitia kwa Balozi Msekelu kumpelekea salamu za heri Rais wa Afrika Kusini Mheshimiwa Jacob Zuma na kumtakia mafanikio zaidi katika uongozi wake.

Katika mazungumzo hayo, Balozi wa Afrika Kusini Mheshimiwa Msekelu alimueleza Dk. Shein kuwa Afrika Kusini inathamini sana uhusiano wake na Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na nchi hiyo itatumia kila fursa iliyopo kuona kuwa uhusiano huo unaimarika zaidi na zaidi kwa faida ya pande zote.

“Tuna kila sababu ya kuwa karibu na ndugu zetu wa Tanzania na tunatarajia kuwa hata wawekezaji kutoka nchini kwetu wanakuwa mabalozi wazuri nchini Tanzania kuonesha udugu na urafiki wetu” alieleza Balozi Msekelu.

Alikubaliana na rai ya Mheshimiwa Rais ya kuangalia uwezekano wa kupata wawekezaji katika uvuvi wa bahari kuu ambapo alisema itakuwa ni muendelezo wa ushirikiano uliopo sasa kati ya nchi yake na Tanzania katika sekta ya bahari.

Balozi Msekelu alishauri kuwepo na ushirikiano kati ya mamlaka za viwanja vya ndege vya Afrika Kusini na Zanzibar ambao utaweza kusaidia jitihada za kuendeleza sekta ya utalii kwa pande zote mbili.  

Mheshimiwa Rais alieleza kuwa ni jambo zuri kwani nchi hiyo ina utaalamu na uzoefu wa kutosha ambao utaweza kuisaidia Zanzibar katika eneo hilo.

Mazungumzo hayo yalihudhuriwa pia na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshmiwa Issa Haji Ussi.  

Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.