STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 18.07.2016

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein
ameizindua rasmin Kamati ya Rais ya Kukusanya fedha kwa ajili ya ununuzi wa
madawati kwa skuli za Msingi na Sekondari za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
huku akiahidi kuwa Serikali itakuwa bega kwa bega na Kamati hiyo katika kuhakikisha
lengo hilo linafikiwa.
Dk. Shein aliyasema hayo leo huko Ikulu
ndogo Kibweni katika hafla fupi ya kuizindua Kamati hiyo ambayo itafanya kazi
kwa lengo la kulitafutia ufumbuzi tatizo la uhaba wa madawati katika skuli za
Sekondari na Msingi za Unguja na Pemba.
Katika maelezo yake Dk. Shein alisema
kuwa anamatumaini makubwa kuwa Kamati hiyo chini ya Mwenyekiti wake Waziri wa Nchi
Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora Haroun Ali
Suleiman itapata mafanikio na kufikia lengo lililokusudiwa kutokana na uzoefu
na uhodari wa wajumbe wake.
Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar itakuwa bega kwa bega katika kushirikiana na Kamati hiyo
ili lengo lililokusudiwa liweze kufikiwa kwani tatizo hilo ni la Jamii nzima ya
Zanzibar.
Kutokana na hali hiyo, Dk. Shein
alisisitiza kuwa Serikali itachukua juhudi za makusudi kwa mashirikiano na
Kamati hiyo katika kuhakikisha lengo hilo linafikiwa kama ilivyofanya katika
kulitafutia ufumbuzi suala la usafiri wa baharini na hatimae Serikali ikanunua
meli yake mpya ya MV Mapinduzi II.
Aidha, Dk. Shein alieleza kuwa anaelewa
kuwa kazi hiyo ni ngumu lakini anaamini kutokana na uzoefu, weledi na uhodari
wa Wajumbe wa Kamati hiyo kwa mashirikiano ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
mafanikio yatapatikana kwani tayari Serikali imeshawasilisha rasimu ya
uchangiaji na upatikanaji wa madawati katika skuli za Serikali za Unguja na Pemba.
Pamoja na hayo, Dk. Shein alitumia fursa
hiyo kutoa shukurani kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi ambapo mara tu baada ya uwasilishaji wa
rasimu hiyo Katika Kikao cha Baraza la Wawakilishi baadhi ya wajumbe walianza
kutoa michango yao kwa ajili ya ununuzi wa madawati hayo.
Nae Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Mohammed
Raza ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati hiyo
kwa niaba ya Wanakamati wenziwe alieleza azma na nia sambamba na lengo la
Kamati hiyo ni kuhakikikisha tatizo la uhaba wa madawati katika skuli za
Zanzibar linapatiwa ufumbuzi.
Katika maelezo yake Raza alitoa shukurani
za dhati kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali
Mohamed Shein kwa juhudi zake na maarifa katika kuwatumikia wananchi wa
Zanzibar wakiwemo wanafunzi katika kuhakikisha wanapatiwa madawati ili sekta ya
elimu izidi kuimarika hapa nchini.
Raza alisema kuwa nia na malengo ya
Kamati hiyo ni kulitafutia ufumbuzi tatizo hilo kwa mashirikiano ya pamoja
ikiwa pia ni miongoni mwa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM katika
kuimarisha sekta ya elimu hapa nchini.
Pamoja na hayo, Raza alisisitiza suala la uangalifu katika
manunuzi sambamba na umazubuti wa madawati hayo ili yaweze kudumu kwa muda
mrefu na kujenga heshima kwa kufahamika kwa matumizi ya fedha zote
zilizochangwa.
Nae Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia
ni Mwakilishi wa Jimbo la Makunduzi Haroun Ali Suleiman alimueleza Rais Dk.
Shein hatua za awali zilizoanza kuchukuliwa na Kamati hiyo ikiwa ni pamoja na
kukutana na uongozi wa Wizara husika ya Elimu katika kulipangia mikakati suala
hilo.
Aidha, Waziri Haroun aliahidi kuwa nia na
malengo ya Kamati hiyo itafikiwa katika kulitafutia ufumbuzi suala hilo kwa
mashirikiano ya pamoja.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment