Habari za Punde

Iweje watoto wakoseshwe matunzo, huduma kwa ndoa kuvunjika?

Na Haji Nassor, Pemba
NI jambo la faraja lililochanganyika na furaha kubwa,kwa mwanamme kuchagua mke ampendae, huku akiamini kwamba ndie ambae atamzalia watoto, kama yeye alivyozaliwa na kulelewa.
Wahenga walishanena kwamba furaha ya ndoa, ni siku moja ingawa mikiki yake huwa daima, na naamini hayo yanafahamika, lakini hakuna mwanamme anegopa kuchagua ampendae kwa kuliogopa hilo.
Baada ya ndoa, wengine hubahatika kupata watoto si haba, kama malengo yao yalivyokuwa kabla na baada ya kufungwa kwa ndoa, ingawa nazo takala mara hujiri bila ya wengine kutarajia.
Kwa waliokwenda darasani, wanafahamu kuwa talaka ni moja ya halali ambayo Allah ameichukia, hili linamantiki sana maana wapo wanaowaacha watalaka wao na kisha kuwakosesha huduma sambamba na watoto.
Lakini linalonipa wasi wasi na kunikosesha usingizi na hata kujiuliza suali bila ya kupata jawabu, iweje watoto wakoseshwe matunzo na huduma nyengine za lazima, mara tu ndoa inapovunjika?
Hapa mimi niwaulize wenye kuzitoa talaka kama njugu, hawa watoto wanakosa gani, ndoa tu zinapovunjika hadi kufikia kukoseshwa matunzo na huduma za kibinaadamu?
Kama mmegombana na kukosana, mbona naona ni wewe na mama yao tu, wala watoto hasa waliochini ya umri, hawafahamu kwamba penzi lenu sasa limemaliza muda (love expire), wanahusika je kukoseshwa na matunzo .
Wakati mnafunga ndoa, mliifuata kikamilifu misingi, matamko, maelekezo na sharia za kiislamu na hata ulipoamua kumuacha mama watoto wako, pia uliangalia hilo, sasa iweje watoto uwakoseshwe matunzo kwa talaka yako?
Mbona hapa mimi sipati picha, au hawa waachaji wanatumia misingi na kanuni za kitabu gani, maana hata katiba ya nchi iliotungwa na wanaadamu, haielekezi kwamba ni sahihi kuwakosesha watoto matunzo na huduma kwa ndo kuvunjika.
Yapo mashauri zaidi ya 500 kwenye mahakama za kadhi kisiwani Pemba kuanzia mwaka 2011 hadi mwaka jana, ambayo wanawake walifika kulalamika, wakielezea kwamba watoto wamekoseshwa huduma baada ya ndoa kuvunjika.
Kwenye hayo wilaya ya Wete, ilijukusanyia matukeo 131 sasa jiulize ndani ya matukio hayo 500 mna watoto wangapi ambao wanaishi kama vifaranga vilivyokosa mama, kwa akinababa kutotoa matunzo na huduma baada ya wao kutoa talaka?
Pengine hawa wanaume wenye tabia ya kukimbia matunzo kwa watoto wao, hawaamini kwamba na wao walilelewa kwa salama na amani, hadi wakafikia pahala wakatafuta wapendwa wao, sasa iweje leo wasahau wanakotoka?
Ijapokuwa wapo baadhi ya akinamama wachache huzikataa huduma za aliekuwa mume wake, pengine kwa uchungu au iblisi amentanda, lakini mbona huyu baba anawajibu wa kubuni njia ili watoto wapate huduma.
Mbona unapokwenda kuposa pahala na ukikataliwa, unabuni njia, maneno mengine, mavazi na hata kuwalisha kijio maini wakwezako watarajiwa ili kumtia mkononi mtoto wao, sasa iweje kweye hutunzo hapa ushindwe na ulegee.
Kama hivyo ndivyo, lazima wanaume wanaocha wajitahidi kuhakikisha huduma na matunzo kwa watoto wao, hawakatishwi maana kinyume chake ni kujikusanyia tani za dhambi zilizoendelevu.
Lakini hata wewe mama ulioachika lugha na tabia yako kwa baba watoto wako anaetaka kuleta huduma, basi acha ndaro kinyume chake ni kujibebesha mazigo usiokuwa wako.
Taasisi za serikali na za dini nazo zisifumbie macho wakati wanapopokea malalamiko kutoka kwa watoto au akina mama juu ya kukoseshwa matunzo.
Mimi naamini kila jambo linawezekana ikiwa kila mmoja atatimiza wajibu wake bila ya kusimamiwa na akiamini kwamba, anachokifanya ni kwa mujibu wa maelekezo ya imani yake.

                                hajinassor1978@gmail.com

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.