Habari za Punde

Zoezi la Uwekaji wa Nyasi Bandia na Tatan Uwanja wa Gombani Pemba Wakamilika kwa Hatua Kubwa.

Baada ya Kukamilika kwa kazi ya Uwekaji wa Raba ya kukimbilia katika uwanja wa michezo Gombani Kisiwani Pemba, pichani ni muonekano wa mpya wa uwanja huo baada ya wataalamu kutoka kampuni ya Guangzhou Jrage Athletic Facilities Co.LTD ya nchini China, kukamilisha kazi hiyo.
Wataalamukutoka kampuni ya Guangzhou Jrage Athletic Facilities Co.LTD ya nchini China, wakiwa katika hatua za mwisho kukamilisha kazi ya Uwekaji wa Tatani katika uwanja wa gombani, pichani wataalamu hao wakiweka alama katika njia kwa wanariadha ndani ya uwanja huo.
(Picha na Abdi Suleiman.Pemba)


Na Abdi Suleiman, Pemba.

KAZI ya Uwekaji wa Mpira wa kukimbilia (Tatani) katika uwanja wa michezo Gombani, iiliyokuwa ikifanywa na wataalamu kutoka kampuni ya Guangzhou Jrage Athletic Facilities Co.LTD ya nchini China, imeshakamilika kwa asilimia 99.9.

Kazi hiyo iliyokadiriwa kuchukuwa muda wa siku 40 hadi kukamilika kwake, lakini wataalamu hao kutoka China wamelazimika kuifanya kazi hiyo kwa ufanisi zaidi.

Wataalamu hao waliwasili kisiwani Pemba katikati ya Mwezi wa Juni mwaka huu, huku kazi hiyo ya uwekaji wa tatani wakianza Juni 25, kwa kuweka sawa vifaa vyao, huku hatua ya awali ya uwekaji wa raba hiyo ikianza Juni 29.

Mwandishi wa habari hizi alifika katika uwanja huo wa michezo na kushuhudia wataalamu hao, wakiwa katika hatua za mwisho katika uwekaji wa nambari kwenye njia za kukimbilia wanariadha.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Afisa Mdhamini wa Wizara ya Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo Pemba, Khatib Juma Mjaja alisema kwa sasa kazi zilizobalia ni ndogo ndogo lakini kwa asilimia 99.9 kazi hiyo imeshakamilika.

Alisema wataalamu hao wamejitahidi kufanya kazi kwa umakini zaidi, ili kuhakikisha kazi hiyo inakamilika kwa wakati, licha ya kukumbana na changamoto ya Mvua iliyokuwa ikisitisha ufanyaji wao wa kazi.

Aliwataka mashabiki wa mpira wa miguu kisiwani Pemba, kuendelea kuwa wastahamilivu katika kipindi hicho ambacho uwanja uko katika hatua za matengenezo.

“Wanamichezo endeleeni kuwa na uvimilivu mambo mazuri hayahitaji haraka, matumaini yenu yamefikia na endeleeni kuwa wavumilivu mutarudi katika uwanja wenu”alisema.

Nao wapenzi wa mipira wa miguu Kisiwani Pemba, waliokuwa wakifuatilia kazi hiyo ya uwekaji wa tatani hiyo, waliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuufanya uwanja huo kuwa wa kisasa zaidi.

Walisema kukamilika kwa kazi hiyo basi ni moja ya hatua kubwa ya kuutangaza zaidi Uwanja huo, kitaifa na kimataifa kwani vilabu mbali mbali vikubwa vitajitokeza kuhitaji kufanya mazoezi kiwanjani hapo.

Omara Ali Khamis aliyomba Serikali baada ya kumaliza kazi ya Uwekaji wa Tatan, kuuangalia katika sehemu za majukwani, skoobodi na pamoja na paa la uwanja huo.

Alisema pindi sehemu hizo pindi zikifanyiwa marekebisho basi uwanja huo utaweza kuwa uwanja wa kisasa zaid, kwani baada ya uwekaji wa tatani umeweza kubadilika pia.

“Tunapaswa kuishukuru Serikali yetu katika hatua kubwa iliyopitia, hili ni jambo la kuwapongeza viongozi wa Serikali na Wizara ya Habari kwa kazi kubwa waliyofikia ya uwekaji war aba hiyo”alisema.

Amini Yussuf Khalfani alisema sasa matumaini ya wanamichezo wa kisiwa Cha Pemba, yamerudi upya baada ya kazi ya uwekaji wa tatani kukamilikwa kwa asilimia kubwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.