Habari za Punde

Wanafunzi 22 wa Zanzibar Kushiriki Mashindano ya Wanasayansi Wachanga Dar es Salaam.

Na Ramadhani Ali /Maelezo.                  
Wanafunzi 22 kutoka Skuli 11 za Zanzibar wataungana na wanafunzi wenzo kutoka Skuli 140 za Tanzania Bara katika mashindano ya Mradi wa wanasayansi wachanga Tanzania (YST) yanayoanza kesho katika Ukumbi wa Mwalimu Nyerere Dar es salaam.

Mratibu wa Mradi wa YST Zanzibar Maalim Ame Haji Vuai amesema wanafunzi wa skuli saba za Zanzibar wakiwa na walimu wao wameondoka leo mchana na wanafunzi wa skuli nne za Pemba wameshawasili Dar e s salaam.

Maalim Ame amesema lengo la Mradi wa wanasayansi wachanga ulioanza mwaka 2012 ni kuwapa fursa vijana kutumia elimu waliyoipata madarasani kutatua changamoto zinazoikabili jamii na kuwafanya kupenda masomo ya sayansi.

Ameongeza kuwa washindi wa tatu wa mwanzo kwa Tanzania hupata zawadi ya fedha taslim na mshindi wa kwanza hupewa fursa ya kutembelea nchi ya Ireland na kupewa udhamini wa masomo ya juu nchi za nje.

Mafanikio makubwa kwa Zanzibar tokea kuanzishwa mradi huo ni wanafunzi wa skuli ya Sekondari ya Lumumba kushinda nafasi ya kwanza mwaka 2014 na mwaka jana Skuli ya sekondari ya Kiembesamaki ilishinda nafasi ya tatu.

Akiwaaga wanafunzi hao katika Skuli ya Sekondari ya Kiembesamaki, baada ya kuangalia kazi watakazoziwasiliisha kwenye mashidnao hayo, Naibu Makamu Mkuu wa chuo cha SUZA (Taaluma) Dkt. Haji Mwemvura Haji amewapongeza wanafunzi hao na kuwataka kujiamini zaidi ili waweze kushinda.

Amewahakikishia wanafunzi na walimu wao kuwa kazi zote zilizoonyeshwa na wanafuzi kutoka  Unguja ni nzuri na zinanafasi ya kushinda katika mashindano hayo licha ya kuwa watakabiliana na ushindani mkubwa kutoka skuli za Bara ambao ni nyingi zaidi.

Amesema chuo Kikuu cha SUZA hivi karibuni kitazindua kituo cha uvumbuzi chenye lengo la kuwasaidia vijana wanaojishughulisha na uvumbuzi wa kisayansi ili kuwaendeleza na kuwasaidia katika tafiti zao.

“Nimevutiwa sana na namna vijana wanavyoonyesha vipaji vyao na ninaamini kuwa watakuwa wa kwanza kupata msaada wa kituo chetu mara tu baada ya kuzinduliwa,” alisisitiza Dkt. Mwemvura.

Aliahidi kuwa tafiti zote zinazofanywa na wanasayansi wachanga kwa ajili ya mashindano hayo SUZA itazikusanya kwa ajili ya kuziendeleza ili ziweze kuchangia katika maendeleo ya Taifa.
Hata hivyo amewataka walimu wakuu wa skuli za sekondari  ambao hazijawihi kutowa washiriki katika  maswhindano hayo kufanya juhudi za makusudi ili waweze kushiriki.

Skuli zinazoshiriki mashindano ya wanasayansi wachanga kutoka Zanzibar mwaka huu ni Lumumba, S.O.S, Bembella, Hailesellassie, Mwanakwerekwe ‘A’, Mpendae na Kiembesamaki zote kutoka Mkoa wa Mjini Magharibi.

Skuli kutoka Pemba ni Maendeleo ya Wilaya ya Mkoani, Shamiani na Fidelcastro Wilaya ya Chake Chake na skuli ya sekondari ya Utaani Wilaya ya Wete. 

IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.