Habari za Punde

Wawakilishi, Wabunge msisahau kurudi Pemba kutelekeza ahadi zenu


Na Haji Nassor, Pemba
UCHAGUZI umeshamalizika na viongozi walioingia kwenye kinyang’anyiro wameshapatikana, na wanakumbuka vyema kwamba walitoa ahadi kwa korja kwa wananchi wao.
Na ndio utaratibu wa kuingia kwenye uchaguzi na kisha wananchi kupiga kura na kuwasaka viongozi wawatakao, kwa ajili ya kuwaongoza katika kipindi cha kusubiri uchgauzi mwengine.
Si haba kabla ya kuingia kwenye mchakato huo, viongozi hao walitamba na kujinapa kwenye majukwaa, wakizieleza ahadi ambazo watawatekelezea wananchi wao bila ya kujali vyama vyao.
Kwa wale wawakilishi wao hulazima kwenda kisiwani Unguja kuingia kwenye mjengo wa baraza hilo, ili kuwawakilishi wananchi wao, huku wabunge wakijitupa Dodoma kwa kazi kama hiyo.
Sasa basi wawakilishi, wabunge lazima misasahu kurudi kisiwani Pemba kutelekeza ahadi zenu kwa wananchi, maana waliwachagua kwa kuwaamini kwamba mnaweza.
Hili lazima nilikokomoke, maana uzoefu unaonyesha kuwa baadhi ya wabunge na wawakilishi wanaotokea kisiwani Pemba, wamekuwa wakijisahau kurudi majimboni, kutekeleza ahadi zao.
Maana wapo baadhi ya wananchi majimboni, wamekuwa wakiwaona tunu viongozi wao, kutokana na kujiweka Unguja au Dodoma hata baada ya kumalizika vikao, jambo ambalo huwaudhi.
Iweje wabunge na wawakilishi hawa, wayaone majimbo yao kama kuti kavu, kwa kujichimbia kwenye majimbo ya wenzao, wakati wao wakisakwa kwa udi na uvumba.
Jamani viongozi nyinyi, mnasahau fadhili za wananchi wenu kwamba ndio wao waliowavalisha suti na mitandio ya bei kubwa, sasa iweje hata baada ya kumalizia vikao kushindwa kurudi Pemba.
Wakati mwengine hata waandishi wa habari, asasi za kirai au vikundi vya ushirika huwahitaji viongozi hawa na kushindwa kuonekana majimboni na kuwaacha wahusika njia panda.
Haipendezi na wala haingii akili, kwamba eti mbunge au mwakilishi amalize miezi ista hajaonekana jimboni, sasa huku ni kuwatendea haki wananchi na wapiga kura?
Wapo wengine wabunge na wawakilishi hao wamekuwa mstari mbele kujimwanga majimboni mwao na hata kushirikia mazikoni, kuangalia na kutoa michango yao kwa wagonjwa, sasa lazima wengine waige mifano hii.
Chonde chonde, viongozi wetu jiwekeeni utaratibu wa kutembelea maeneo kadhaa ya majimbo yenu, kwa staili ile ile mlioitumia ya kuomba kura, na sio vibaya hata zile ofisi za majimbo nao wawakilishi kujipachika.
Kama hivyo ndivyo lazima wananchi majimboni mjiwekee utataribu na mikakati ya kuwasema viongozi wa majimbo ambao wamekuwa watoro kuonekana kwenye maeneo yao.
Lakini na nyinyi wabunge na wawakilishi, iweje hasa ifikie pahala mpaka wananchi wenu wawatamani, pahala penyewe ni Unguja na Pemba au Dodoma na Pemba, hebu kuweni wastaarabu.
Hata viongozi wa vyama, msisite kuwaamsha viongozi kuwapitia wananchi majimboni na sio kujitia kwenye misafara ya viongozi wakuu wanapofika kwa shughuli zao za maendeleo.

Mimi naamini kila jambo linawezekana, iwapo kila mmoja atafanya kazi zake kwa kufuata kanuni na sheria zilizopo, tukiamini kuwa mjenga nchi ni mwananchi

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.