STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 6.09.2016
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein ameeleza haja kwa uongozi wa Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati
na Mazingira kuwafuata wananchi katika maeneo yao wanayoishi ili kutambua
mahitaji yao katika upatikanaji wa huduma muhimu zilizopo katika Wizara hiyo.
Dk. Shein alieleza
kuwa iwapo viongozi wa Wizara hiyo watakwenda katika maeneo wanayoishi wananchi
wataweza kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi na kuwataka kutokaa maofisini na
badala yake wawafuate wananchi katika maeneo yao kwani Serikali imo katika
kutekeleza jukumu lake la kuwahudumia wananchi wote wa Zanzibar popote pale
walipo.
Dk. Shein aliyasema
hayo wakati alipokutana na uongozi wa
Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira wakati ukitoa taarifa ya
Utekelezaji wa Programu ya Utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi pamoja
na ahadi za Rais kwa muda wa miaka mitano (2015-2020) huko Ikulu mjini Zanzibar.
Katika maelezo yake
Dk. Shein alisisitiza juu ya uwajibikaji kwa viongozi hao katika kutekeleza
majukumu yao ili kuwahudumia wananchi ipasavyo sambamba na kutambua vyema
majukumu yao katika maeneno yao ya kazi.
Dk. Shein alitumia
fursa hiyo kutoa pongezi kwa viongozi na watendaji wa Wizara hiyo katika
kutekeleza ipasavyo majukumu yao katika kutoa huduma kwa wananchi hali ambayo
imepelekea huduma hizo kuimarika zaidi Unguja na Pemba.
Aidha, Dk. Shein aliwataka
viongozi hao kutotumia muda wao mwingi kukaa maofisini na badala yake waende
kwa wananchi ili kutafuta changamoto zinazowakabili katika kupata huduma
zitokanazo na Wizara hiyo.
Nao uongozi huo kwa
upande wake ulieleza juhudi inazozichukua katika kutekeleza majukumu yake ikiwa
ni pamoja na mafanikio makubwa iliyoyapata katika kuwapelekea huduma bora na
muhimu wananchi zikiwemo huduma za maji na umeme.
Katika maelezo yao
viongozi hao walieleza kuwa tayari Shehia zote za Unguja na Pemba
zimeshafikishiwa huduma za umeme na hivi sasa zimebaki Shehia mbili tu ambazo
ni Fundo na Minazini zilizopo Kiswani Pemba ambazo nazo hivi sasa zimo katika
mchakatoya kupelekewa huduma hiyo.
Aidha, uongozi huo
ulieleza kuwa kwa upande wa visiwa vidogo vidogo tayari vyote vimeshapelekewa
huduma ya umeme na kisiwa kilichobaki ni kiswa cha Fundo na visiwa vidogo vya
Uvinje, Okota na Njao ambavyo navyo vitapata huduma hiyo katika kipindi kifupi
kijacho.
Katika programu hiyo
ya Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020 uongozi huo
ulieleza kuwa umo katika jitihasda za kupunguza migogogro ya ardhi kwa
kuimarisha huduma za mahakama za ardhi katika mikoa yote ya Unguja na Pemba.
Pamoja na hayo,
uongozi huo ulieleza juhudi zinazoendelea kuchukuliwa katikan kuandaa Sera na
Sheria ya Mafuta na Gesi Asilia ikiwa ni pamoja na jitihada za kuwajengea uwezo
watendaji pamoja na kuhamasisha vijana kujiunga na masomo ya fani ya Mafuta na
Gesi Asilia.
Kwa upande wa suala
zima la mazingira uongozi huo ulieleza kuwa hatua inazozichukua katika
kusimamia Sera na Sheria ya Mazingira pamoja na ushirikishwaji wa jamii katuika
utunzaji wa Uhifadhi wa Mazingira kwenye maeneo yao ikiwa ni pamoja na
kusimamia mabadiliko ya tabianchi na elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa
utunzaji wa mazingira.
Wakati huo huo, Dk. Shein alikutana
na uongozi wa Wizara ya Biashara, Wiwanda na Masoko hapo Ikulu mjini Zanzibar
kwa lengo hilo hilo la kutoa taarifa ya Utekelezaji wa Programu ya Utekelezaji
wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020 iliyotolewa na Wizara hiyo.
Katika taarifa yake
Wizara hiyo ilieleza kuwa majukumu yake makubwa ni kusimamia na kuendeleza
sekta ya biashara na sekta ya viwanda hapa Zanzibar.
Aidha, uongozi huo
ulieleza kuwa Wizara hiyo inatekeleza malengo hayo ambayo kwa ujumla
yanajielekeza katika malengo makuu ya Mkakati wa Kukuza Uchumi Zanzibar pamoja
na kuweza Mazingira ya Ukuaji Uchumi, Kujenga Uchumi Endelevu na mpana ili
kuondoa umasikini pamoja na kujenga sekta binafsi iliyo imara kwa lengo hilo la
kukuza uchumi.
Nae Dk. Shein kwa
upande wake aliwataka viongozi na watendaji wa Wizara hiyo kufanya kazi kwa
mashirikiano zaidi katika kuhakikisha malengo yaliokusudiwa yanafikiwa huku
akipongeza juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Wizara hiyo katika kuimarisha
sekta zake.
Sambamba na hayo, Dk.
Shein aliendelea kusisitiza suala zima la uwajibikaji kwa viongozi na watendaji
wa Wizara hiyo sambamba na kuzitafutia ufunmbuzi changamoto zilizopo kwa lengo
la kuendelea kupata mafanikio zaidi katika sekta za biashara, viwanda na masoko
ili kuendelea kukuza na kuimarisha uchumi wa Zanzibar.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address:
2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail:
rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment