Habari za Punde

UNESCO Kutumia Bilioni 3 Kusaidia wa Watoto wa Kike Kurudi Shuleni.

 Mkuu wa Ofisi na Mwakilishi wa UNESCO nchini, Bi. Zulmira Rodriguez akizungumza kuhusu mradi ambao una malengo ya kurejesha watoto wa kike shuleni. Kushoto ni Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Wanawake (UNWOMEN), Hashina Begum na kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Bi. Maimuna Tarishi.
 Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Bi. Maimuna Tarishi akizungumza kuhusu mipango ya serikali kukabiliana na tatizo la watoto wa kike kukatishwa masomo.
Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Wanawake (UNWOMEN), Hashina Begum akizungumzia sababu ya watoto wa kike kutokuwepo shuleni na jinsi ambavyo UNWOMEN watashiriki katika mradi wa kusaidia watoto wa kike kurudi shuleni.
Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Watu Duniani (UNFPA), Maria Karadenizli akielezea takwimu za watoto wa kike ambao hawapo shuleni. 
 Mkuu wa Ofisi wa Shirika hilo la Maendeleo la (KOICA), Joosung Park akielezea ushiriki wa KOICA katika kusaidia mradi huo kukamilika sawa na mipango iliyowekwa.


Na Mwandishi wetu

Katika kuhakikisha watoto wa kike wanakuwa shuleni na hatimaye kumaliza masomo yao, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) limetenga Dola 1,605,000 ambazo ni zaidi ya Bilioni 3 za Kitanzania ambayo zitatumika kuwasaidia watoto wa kike nchini kurejea katika shuleni kwa ajili ya kuendelea na masomo.

Akizungumzia mradi huo, Mkuu wa Ofisi na Mwakilishi wa UNESCO nchini, Bi. Zulmira Rodriguez alisema kuwa Tanzania bado inaonekana kuwa na tatizo la watoto wa kike kuachishwa masomo yao kutokana na sababu mbalimbali ikiwepo kupata mimba za utoto na ndoa za utotoni hivyo kupitia mradi huo wataweza kuwasaidia watoto hao kuendelea na masomo.

Bi. Rodriguez alisema UNESCO imeamua kushirikiana na serikali ili kuwasaidia watoto wa kike kurejea masomoni na utafanyika kwa uhakika bila kumwacha mtoto yoyote na wana matumaini utaweza kusaidia watoto wa kike ambao wamekatishwa ndoto zao kimaisha kutokana na kukatishwa masomo.

“Tanzania kuna tatizo la watoto wa kike kusahaulika katika elimu na UNESCO imejitoa kushirikiana na serikali ya Tanzania ili kusaidia kukuza elimu ya watoto wa kike, “Baadhi ya mambo ambayo yanaonekana kuchangia ni pamoja na mambo ya asili, wamekuwa wakiwaozesha ndoa za utotoni na na watoto wengine wamekuwa wakipata mimba za utoto na hivyo kuacha masomo … mradi huu ni wa uhakika na utasaidia kukuza elimu,” alisema Bi. Rodriguez.

Kwa upande wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Bi. Maimuna Tarishi alisema serikali inafahamu kuwepo kwa changamoto hizo na imekuwa ikifanya jitihada ili kuhakikisha kuwa matatizo ya watoto wa kike kukatishwa masomo yakimalizika.

Alisema kuwa makabila mengi ya Tanzania yamekuwa yakiwaona watoto wa kike kama watu wa kukaa nyumbani na kulea watoto lakini kama jamii ikiwa na mtizamo tofauti na kuwawezesha watoto wa kike basi wanaweza kusaidia nchi kukuza uchumi.

“Tumeona kazi ambayo wameifanya UNESCO hata machifu huko Ngorongoro wameanza kuelewa umuhimu wa watoto wa kike kuwa shuleni na kwa mpango huu matarajio ya serikali ni kumaliza changamoto iliyokuwepo awali,

“Serikali inafahamu kuna changamoto nyingi ambazo zinawakuta watoto wa kike na sio katika elimu pekee bali ni maeneo mengi … serikali inataka kukuza thamani ya elimu kwa watoto wa kike ambao wengi wao wanakatishwa kwa sababu ya mimba na ndoa za utotoni,” alisema Bi. Tarishi.

Nae Afisa Mradi wa Maswala ya Afya ya Uzazi kwa Vijana (UNFPA), Fatina Kiruviya alisema mradi una malengo ya kuhakikisha watoto wa kike wanakuwa shuleni na kwa kuanza wanataraji kufanya mradi Ngorongoro, Pemba, Geita na Sengerema.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.