Alhamdulillaah, nilibahatika kuwa miongoni mwa waliojaaliwa kuitekeleza Ibada ya Hajj mwaka
1435 - 2014
Nilikuwa
kwenye mafunzo ya kivitendo ya siku sita kuanzia tarehe 8 Dhulhijjah - mfunguo tatu mpaka tarehe 13
Dhulhijjah 1435.
Kwa
wale watakaombatana na safari yangu hii ni kwamba Hijja ni ibada ambayo
hufanyika katika mji wa Makkah, Saudi Arabia ni matendo maalum, yanayofanyika
katika wakati maalum, sehemu maalum na kwa ajili ya watu maalum. Ni nguzo ya
tano katika nguzo za kiislamu ambayo humuwajibikia kila Muislamu mwenye uwezo
mara moja katika maisha yake.
Naam
ni siku sita tu lakini nimeweza kujifahamu na kujitambua katika kipindi cha
siku sita ambazo zitabakia katika kumbukumbu ya maisha yangu. Kwani mafunzo
yake ya kinadharia, kivitendo na kiroho ni mafundisho nadra unayoweza kuweza
kuyapata kwa kipindi kifupi na yakaweza kuleta athari kubwa katika maisha ya
Muislamu.
Nikikumbuka
kwa mara ya pili nilipoivaa Ihraam siku ya Tarwiyah, tarehe 8 Dhulhijjah na
kutia nia ya Hajj na kuanza Talbiyah “Labbayka Allaahumma Labbayka Labbayka Laa
shariyka laka Labbayka Innal hamda Wanni’imata laka walmulk Laa shariyka laka”.
Sikujikuta peke yangu, kila ninaemkuta njiani anatamka Talbiyah kama mimi. Kila
ninaemkuta njiani amevaa Ihraam kama mimi shuka mbili tu nyeupe miongoni mwa
wanaume hana kitu chochote ndani kwani ni haramu kuvaa nguo yoyote iliyoshonwa
wakati upo katika Ihraamu. Sote tumevaa viatu vya kawaida tu mithili ya kanda
mbili au viatu visivyofunika mguu wote na hakuna hata mwanamme mmoja aliyevaa
kofia, ukishahirimia hutakiwi kuvaa kofia kichwani kwa mwanamme au kupaka
manukato ya aina yoyote.
Kila
ninamkuta njiani simjui jina lake wala wapi anapotoka, simjui kama ni Daktari
au ni Mwalimu, Mpagazi au Mchuuzi, ni mheshimiwa au mtu wa kawaida, mweupe,
mweusi mkubwa, mdogo lakini namjua kama
ni ndugu yangu Muislamu na sote
tumetamka Laa Ilaaha Illa Llaah Muhammadun Rasuulu Llaah. Kalima au neno
hili ndilo lilitukutanisha katika ardhi ya Haram, Kalima hili ndilo
litakalokutanisha peponi, Kalima hili ndilo litakalotuepusha na adhabu kali ya
moto wa Allaah ‘Azza wa Jall ikiwa tutakamilisha masharti yake saba.
Tulipofika
Mina huku tukiendeleza Talbiyah na kuomba dua kwa Allaah ‘Azza wa Jall, kila
nikiirudia Talbiyah basi nafsi yangu inanikumbusha ujumbe mzito uliopo kwenye
talbiyah nao ni wa Tauhiyd kumpwekesha Allaah ‘Azza wa Jall kwa ibada na kila
kwa kila kitu. Tunamhakikishia Allaah
‘Azza wa Jall kwamba hana mshirika huku tumemwitikia, tunamthibitishia Allaah
‘Azza wa Jall kwamba hakika himidi na shukrani, neema na ufalme vyote ni vyake
pekee na hana mshirika.
Nikaikumbuka
aya katika Qur’aan inayosema: “hakika Sala zangu, vichinjwa vyangu, uhai wangu
na mauti yangu vyote ni vya Allaah Mola wa viumbe vyote, hana mshirika na hivyo
nimeamrishwa kuwa Muislamu wa awali”. Naam Hijja ni darsa muhimu
inayotufundisha somo la Tawhiyd kwani Mtume Muhammad Swalla Allaahu ‘alayhi
wasallam alihama Makkah kwenda Madina (kwa sababu ya kuisimamisha Tawhiyd) na
aliporudi kuikomboa Makkah aliikomboa bila ya kumwaga damu na kuisimamisha
Tawhiyd.
Itaendelea...
No comments:
Post a Comment