Habari za Punde

Rais wa Zanzibar Dk Shein Azungumza na Uongozi wa Wizara ya Habari Utalii Utamaduni na Michezo Zanzibar.

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                 21 Oktoba, 2016

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameipongeza Wizara ya Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo kwa kutekeleza vyema majukumu yake katika Kipindi cha Robo ya Kwanza ya Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Akihitimisha mjadala wa taarifa ya utekelezaji wa kazi za wizara hiyo kwa kipindi cha Julai-Septemba 2016,Ikulu jana, Dk. Shein alieleza kuwa ametiwa moyo na kasi ya utekelezaji wa maelekezo yote yaliyotolewa wakati wa ziara yake ya kutembelea vyombo vya habari vya serikali aliyoifanya mwezi uliopita.

Dk. Shein alibainisha kuwa kasi ya utekelezaji wa maelekezo hayo inadhihirisha umakini wa uongozi wa wizara hiyo na ni kielelezo kuwa dhamira ya serikali ya kuleta mabadiliko katika vyombo vya habari vya serikali ifikapo mwezi Disemba mwaka huu itatimizwa.

“Tumedhamiria kufanya kazi na ndio maana niliahidi kuwa lazima kuwe na mabadiliko ifikapo Disemba mwaka huu na tayari tumeanza kuona mabadiliko hayo hivyo tujitahidi tufikie lengo letu” Dk. Shein alieleza na kuutaka uongozi wa wizara hiyo kufanyakazi kwa kujiamini.

Dk. Shein alibainisha kuwa uongozi wa wizara hiyo ni “timu mpya yenye uwezo” na anaamini kuwa ikifanya kazi kwa ushirikiano itafikia malengo yaliyokusudiwa na kuongeza kuwa tayari ameona “mwanga wa mafanikio tofauti na tulipotoka”

Katika taarifa ya utekelezaji wa Wizara hiyo iliyosomwa na Katibu Mkuu wake Omar Hassan Omar ilionesha  kuwa hatua mbali mbali zimeshachukuliwa na zinaendelea kuchukuliwa kuimarisha vyombo vya habari vya Serikali kama  serikali  ilivyoagiza  na yatakamilika kwa mujibu wa ratiba ya utekelezaji.

Dk. Shein alisisitiza kuwa wizara hiyo ina umuhimu wa kipekee kwa kuwa inashughulika na masuala ya wananchi moja kwa moja hivyo ni lazima utendaji wake uende sambamba na matarajio ya wananchi.

“Wizara hii ni ya watu kwani Utalii ni watu kwa faida ya watu, habari ni watu, utamaduni ni watu na michezo ni watu” Dk. Shein alieleza.
Katika hatua nyingine Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ameagiza suala la madeni ya Shirika la Magazeti ya Serikali ambalo linazidai wizara na taasisi za serikali kiasi cha shilingi zipatazo 537 huku lenyewe kudaiwa kiasi cha shilingi 570 liwe limeshughulikiwa na kumalizwa ifikapo mwezi Machi mwakani.

“Ifikapo mwezi Machi mwakani taarifa za kuwa Shirika hilo linadai rundo la madeni kutoka wizara na taasisi za serikali lisiwepo tena na wao shirika walipe madei yao yote ili waanze upya” Dk. Shein alisema kwa msisitizo.

Kwa upande mwingine Dk. Shein ameitaka Kamisheni ya Utalii kufanya jitihada za ziada za kuhimiza Utalii wa ndani kwa kushirikiana na Umoja wa Makampuni ya Kutembeza Watalii Zanzibar- ZATO ili kuimarisha eneo hilo muhimu katika biashara ya Utalii.

“Tuna maeneo mengi na mazuri ya kitalii kuliko nchi nyingi kama zetu ambazo zimepiga hatua kubwa hatika utalii wa ndani ambayo wananchi wetu wakihamasishwa wanaweza kutembelea” Dk. Shein alisisitiza.

Alifafanua kuwa baadhi ya maeneo hayo ni visiwa vingi vidogo vidogo na maeneo ya kihistoria yaliyotapakaa Unguja na Pemba ambayo wananchi wakitembelea yatawasaidia kuongeza ufahamu wa historia yao na ya nchi yao.

Akisisitiza umuhimu wa vikao hivyo, Dk. Shein alieleza kuwa mpango huo ambao aliuanzisha miaka sita iliyopita ni msingi bora wa kuleta ufanisi na kuongeza kasi ya utekelezaji wa majukumu ya wizara na taasisi zake na ndio maana kumekuwepo na mabadiliko na mafanikio makubwa katika utendaji na utekelezaji wa shughuli za serikali tangu kuanza kwa mpango huo.

“Ni utaratibu unaotumiwa sasa ulimwenguni kote. Unatupa fursa ya kuwa pamoja na kutupa nafasi ya kutatua matatizo yanayojitokeza kwa pamoja, tunapeana maelekezo na kuandaa utaratibu wa kuleta mafanikio zaidi katika kutekeleza majukumu yetu” Dk. Shein alisema.

Katika kikao hicho ambacho ni cha tano katika mfululizo wa vikao hivyo, Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi pamoja na kuipongeza wizara hiyo lakini aliitaka kuchukua tahadhari zaidi katika kushughulikia sekta ya Utalii hasa suala la vitendo vya udhalilishaji wanawake na watoto.
 “Lazima tuwe makini kwa watalii wanaoingia nchini kwa kuhakikisha kuwa ni watu safi na ambao wataheshimu mila na utamaduni wetu na wizara lazima iwe makini katika hili” alisema Balozi Seif.

Akitoa utangulizi wa Wizara yake, Waziri wa Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo Mheshimiwa Rashid Ali Juma alieleza majukumu ya wizara yake na kueleza wa mwelekeo wa utekelezaji wa majukumu ya wizara katika kipindi husika ni mzuri.   

Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 
                                                

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.