STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 18.10.2016

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,
Dk. Ali Mohamed Shein amesisitiza haja ya kujitegemea kwa kuwatumia wataalamu waliopo nchini
sambamba na kutumia nyenzo na rasilimali zilizopo ili kupunguza gharama zisizo
za lazima na hatimae kuweza kuisaidia Serikali.
Dk. Shein aliyasema
hayo leo, Ikulu mjini Zanzibar katika kikao maalum kati
yake na uongozi wa Wizara ya Elimu mara baada ya kuwasilishwa kwa Ripoti ya
Utekelezaji wa Kazi za Wizara hiyo kwa
kipindi cha Julai hadi Septemba mwaka 2016.
Katika maelezo yake,
Dk. Shein alisema kuwa kuna faida kubwa iwapo wataalamu waliopo Mawizarani
watatumiwa vizuri badala ya wataalamu kutoka nje ya nchi.
Alisema kuwa kwa
upande wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, imejaaliwa kuwa na wataalamu wa
fani mbali mbali ambao wanaweza kuisaidia Wizara hiyo katika kufanya mambo yake
mbali mbali katika kuimarisha sekta ya elimu.
Aidha, Dk. Shein
alieleza juhudi za makususdi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar katika ukusanyaji wa mapato huku akisisitiza azma ya Serikali ya
kukata maposho yasiyoyalazima ili fedha
hizo ziweze kusaidia katika kuendeleza majukumu na mipango ya Serikali.
Dk. Shein alitumia
fursa hiyo kutoa pongezi kwa Wizara hiyo kwa kuwasilisha vyema Mpango wake wa
kazi na kuwataka viongozi na watendaji wa Wizara hiyo kuendelea kushirikiana na
kufanya kazi kwa pamoja ili waendelee kupata mafanikio.
Pamoja na hayo, Dk. Shein alisisitiza umuhimu wa uzalendo katika utekelezaji wa majukumu na
kueleza kuwa suala zima la uzalendo litapewa kipaumbele mafanikio makubwa
yanaweza kupatikana.
Nae Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar aliipongeza Wizara hiyo na kusisitiza haja ya kuendelezwa
vuguvugu la mashindano katika skuli mbali mbali hapa nchini ili kuweza kupata
wanamichezo wazuri sambamba na kuongeza vipaji vya vijana katika sekta ya
michezo.
Balozi Idd nae
alitumia fursa hiyo kuihakikishia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kuwa
ataendelea kushirikiana na kuisaidia Wizara hiyo ili kuweza kupatikana elimu
iliyo bora hapa nchini.
Nae Katibu Mkuu
Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Abdulhamid Yahya Mzee alisisitiza umuhimu wa usimamizi katika skuli hapa nchini na kuwataka walimu
wakuu na wasaidizi wao kushirikiana kwa pamoja katika kulifanyia kazi suala
hilo ili elimu bora iliyokusudiwa iweze kupatikana.
Mapema Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Riziki Pembe
Juma alieleza kuwa katika mwaka wa fedha wa 2016/2017, Wizara
yake inaendelea na malengo ya kupanua upatikanaji wa huduma za elimu na
kuimarisha ubora wa elimu inayotolewa.
Alisema kuwa Wizara
imeweka vipaumbele katika kufikia dhamira ya utoaji wa elimu bora kwa wote na
kuweza kupanga mipango mbali mbali ikiwemo kuimarisha elimu ya Maandalizi,
kutayarisha na kuchapisha miongozo ya walimu, kuimarisha elimu na Msingi,
kuimarisha Elimu ya Sekondari, Kuimarisha Elimu Mbadala na Watu wazima na
kuimarisha elimu ya juu.
Aidha, Waziri Pembe
alisema kuwa katika kipindi cha miezi mitatu Julai hadi Septemba 2016, Wizara
hiyo imeweza kutekeleza malengo mabli mbali yakiwemo matayarisho ya Mpango Mkuu
wa Maendeleo ya Elimu kwa kipindi cha miaka mitano (2016-2021) yameanza.
Pamoja na hayo,
alieleza kuwa ujenzi wa vituo viwili vya Mafunzo ya Amali huko Makunduchi na
Daya nao umeanza pamoja na ujenzi wa Kituo cha Utamaduni wa Kiislamu Mazizini
umekamilika.
Alieleza kuwa Wizara
hiyo imepokea jumla ya madawati 5,150, Viti 1630 na meza 600, samani ambazo
zimepokelewa kutoka kwa Wabunge, Wawakilishi na Diaspora.
Vile vile alieleza
kuwa ujenzi wa jengo jipya la Taasisi ya Utalii Maruhubi unaendelea na umefikia
asilimia 20 na ujenzi wa jengo jipya la Taasisi ya Karume nao unaendelea na umefikia
asilimia 30 ambapo pia, ujenzi wa Kituo cha Mafunzo ya Amali Wingwi Mtemani nao
unaendelea na umefikia asilimia 90.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment