Na Salum
Vuai, Maelezo.
Jamii visiwani Zanzibar imeombwa kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wawekezaji
wanaoonesha nia ya kuwekeza miradi ya maendeleo yenye mwelekeo wa kubadilisha
maisha ya wananchi na kuwatoa kwenye umasikini.
Akizungumza
na waandishi wa habari wakati wa ziara ya kutembelea eneo la Matemwe ambako
kampuni ya Penny Royal inajenga kijiji cha utalii, mwanaharakati Rashid Yussuf
Mchenga, amesema Zanzibar haiwezi kujitenga na dunia, hivyo hapana budi
kuwapokea kwa mikono miwili wawekezaji wenye nia njema.
Alitaka
dhamira ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuwafungulia milango wawekezaji wa
nje iungwe mkono na kila mpenda maendeleo, kwani uchumi wa visiwa hivi
unahitaji ushirikiano wa kila hali na taasisi zenye mitaji mikubwa ya kuwekeza
miradi yao hapa nchini zikiwemo za kigeni.
Mchenga
ambae pia ni Katibu Mwenezi Taifa wa chama cha ADA-TADEA, amesema mradi huo
utakaokuwa wa aina yake, ni neema ya kushukuriwa na wananchi wa Matemwe, mkoa
wote wa Kaskazini na Wazanzibari kwa jumla.
“Kama
tunavyosikia kwamba mradi huu utaajiri zaidi ya wananchi 1,500 katika hatua za
awali, hii ni fursa muhimu ya kuwasaidia vijana wetu kuondokana na tatizo la
ajira,” alifahamisha.
Hata hivyo,
alisema kustawi kwa miradi ya maendeleo katika nchi yoyote lazima kuende
sambamba na kuimarika kwa hali ya amani na usalama, kwani bila vitu hivyo,
hakuna jambo la maendeleo linaloweza kufanyika.
Meneja wa Penny
Royal Brian Thompson, amesema miongoni mwa mipango yao katika kuufanikisha mradi
huo, ni kushirikiana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, kuandaa utaratibu
wa mafunzo ya lugha ya Kiingereza kwa vijana, pamoja na elimu ya kazi
zinazohusiana na utalii ili kuwaandaa kwa ajili ya ajira zitakazopatikana.
Alisema
ujenzi wa kijiji hicho utakaogharimu zaidi ya dola bilioni moja, unatarajiwa
kukamilika kabisa baada ya miaka minane, ukifanyika kwa awamu mbili, ambapo
kila moja itachukua miaka mine.
Mradi huo mkubwa na wa kwanza wa aina yake hapa nchini,
utajumuisha ujenzi wa skuli, hospitali, kituo cha polisi, kituo cha jamii
kwa wajasiriamali, uwanja wa ndege,
kiwanja cha Golf na ujenzi wa visiwa vidogo vidogo pamoja na mkahawa maalum
utakaojengwa chini ya bahari.
No comments:
Post a Comment