STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 29.11.2016

SHIRIKA la Umoja wa Mataifa linalowahudumia Watoto Duniani
(UNICEF) limepongeza juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar katika suala zima la kuwahudumia watoto na kuahidi kuendelea kuunga
mkono juhudi hizo ili Zanzibar ifikie malengo iliyoyakusudia.
Mwakilishi wa UNICEF
katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Bi Maniza Zaman aliyasema hayo leo Ikulu
mjini Zanzibar wakati alipokuwa na mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti
wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.
Mwakilishi huyo wa
UNICEF hapa nchini alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweza
kupata mafanikio makubwa katika kuwahudumia watoto sambamba na kuhakikisha
wanapata haki zao za msingi ikiwemo kupata elimu na afya bora.
Alieleza kuwa Shirika hilo
linathamini juhudi hizo na limeweza kushuhudia mafanikio na mabadiliko makubwa katika
sekta za maendeleo hatua ambazo zimewawezesha watoto wa Zanzibar na wao kuweza
kupata haki zao za msingi pamoja na mahitaji yao muhimu ya kimaisha.
Bi Zaman alizipongeza
hatua za Serikali ya Mapinduzi za kujenga majengo mapya yatakayowahudumia
wanawake na watoto katika hospitali ya Manzi Mmoja na ujenzi wa hospitali mpya ya
Abdalla Mazee ni miongoni mwa mafanikio katika sekta ya afya ambayo watoto nao
watafaidika.
Vilevile, Mwakilishi
huyo alimpongeza Dk. Shein kwa juhudi zake kubwa anazozichukua katika kupiga
vita vitendo Ukatili na udhalilishaji wa wanawake na watoto kupitia Kampeni
aliyoianza mnamo mwaka 2014, kwa ajili ya kukomesha vitendo hivyo.
Alieleza kuwa hatua za
Serikali katika kuhakikisha vifo vya akinamama na watoto vinapungua hapa Zanzibar
sambamba na kukabiliana na tatizo la mtapiamlo kwa watoto navyo vimepata
mafanikio ambapo UNICEF pia, imeahidi kuendelea kuziunga mkono juhudi hizo.
Mwakilishi huyo
alieleza kuwa UNICEF tayari imeshaanzisha programu mbali mbali mpya pamoja na
kuziendeleza zile za zamani katika suala zima la kuwahudumia watoto na kueleza
azma yake ya kwenda ngazi za chini zaidi katika jamii kwa kushirikiana na serikali
katika kutatua changamoto zinazowakabili watoto.
Nae Rais wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein kwa upande wake
amelipongeza Shirika la UNICEF kwa juhudi zake za kuendelea kuiunga mkono
Zanzibar na kuahidi kuimarisha uhusiano na mashirikiano yaliopo.
Katika maelezo yake
Dk. Shein alisema kuwa Shirika la UNICEF lina historia kubwa na mashirikiano
kati yake na Zanzibar ikiwa ni pamoja na kuimarisha sekta za maendeleo zikiwemo
sekta ya afya, elimu sambamba na kuimarisha ustawi wa akinamama na watoto.
Dk. Shein alisema kuwa
Shirika hilo limeweza kutoa misaada yake mbalimbali na kuweza kuiunga mkono
Zanzibar katika sekta ya afya kwa kushirikiana na Shrika la Afya Duniani (WHO).
Aidha, Dk. Shein
amesema kuwa licha ya changamoto kadhaa zinazowakabili watoto katika Bara la
Afrika lakini bado Shirika hilo limeendelea kutoa ushirikiano wake na misaada
mbali mbali kwa watoto walio ndani ya nchi za bara hilo.
Pamoja na hayo, Dk.
Shein alieleza juhudi zilizochukuliwa katika kupambana na vifo vya akinamama na
watoto, ambapo Zanzibar imepiga hatua kubwa hasa pale ilipoanzisha mapambano
dhidi ya Malaria jambo ambalo limefanikiwa.
Dk. Shein alitumia
fursa hiyo, kutoa pongezi kwa Shirika hilo kwa kuungana na Mashirika mengine ya
Umoja wa Mataifa (UN) yenye Ofisi zake hapa Zanzibar kuunda ‘One UN’ iliozipelekea
ofisi hizo kukaa katika jengo moja na kuweza kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.
Dk. Shein alieleza
kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuzisimamia vyema, Sera,
Kanuni na Sheria zinazowahusu watoto katika kupata haki zao za msingi na huduma
za kijamii.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment