STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 22.11.2016

MKE wa Rais wa Zanzibar
Mama Mwanamwema Shein amesema kuwa miongoni mwa mambo muhimu ambayo jamii inapaswa
kuyatekeleza kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuyalinda
Mapinduzi ya Januari 12, mwaka 1964 sambamba na kusimamia kwa nguvu zote amani
iliyopo.
Mama Shein aliyasema
hayo leo kwa nyakati tofauti wakati akizungumza na akinamama, viongozi na
wanachama wa Jumuiya ya Wanawake Tanzania (UWT) wa Wilaya ya Kaskazini A na
Wilaya ya Kaskazini B Unguja kwa lengo la kuwasalimia na kuwashukuru kwa
kuendelea kuiunga mkono CCM, na kupelekea kupata ushindi wa kishindo katika uchaguzi
uliopita.
Akiwa katika ukumbi wa
Korea, huko Kibokwa Wilaya ya Kaskazini A, Mama Shein alieleza kuwa kila mtu
kwa nafasi yake ailinde amani na kuinukuu kauli ya Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein anayoitoa mara kwa mara
isemayo “hakuna mbadala wa amani”.
Alisema kuwa mara
nyingi kinamama na watoto huwa ndiyo wanaoathirika zaidi wakati amani
inapotoweka.
Mama Shein ambaye
katika ziara yake hiyo amefuatana na viongozi mbali mbali wakiwemo wake wa
Wabunge na Wawakilishi wa Zanzibar, alisema kuwa tayari Serikali iliyochaguliwa
na wananchi yenye nia ya kweli ya kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar,
imeshaundwa na inaendelea na kazi ya kuwatumikia wananchi kwa ufanisi mkubwa.
Alieleza kuwa Serikali
chini ya uongozi wa Dk. Shein inafanyakazi kwa umakini mkubwa kwa lengo la
kutimiza matumaini na matarajio waliyonayo wananchi wakati walipoichagua.
Hivyo, Mama Shein
alisema kuwa ni wajibu wa viongozi na wananchi wote kutoa ushirikiano katika
kuhakikisha kwamba malengo ya Serikali katika kuinua uchumi na kuimarisha
huduma za jamii yanafanikiwa.
Mapema Mama Asha
Balozi, Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza haja ya wanawake kuendelea
kupendana huku akisisitiza suala zima la uadilifu katika mchakato mzima wa
uchaguzi ujao wa Chama hicho hapo mwakani.
Aliwataka akinamama
kujipunguzia majukumu na badala yake wawe na utaratibu wa kujua nyendo za
watoto wao hasa kutokana na kukithuri vitendo vya ubakaji ambavyo vimeendelea
kushika kasi katika Mkoa huo.
Nae Mama Fatma Karume
kwa upande wake aliwataka akina mama kuwaelimisha na kuwafunza watoto wao
pamoja na kuwasaidia waume zao katika harakati zote za kisiasa na kimaendeleo.
Alieleza furaha yake
kwa kona wanawake waliowengi hivi sasa wamepata uongozi na wamo madarani jambo
ambalo ilikuwa nadra kabla ya Mapnduzi ya Januari 12, 1964 na kuwataka
waliopana fursa hiyo kuitumia vyema na kuishi na watu vizuri.
Katika risala yao
wanachama wa Jumuiya ya UWT walieleza kufarajika kwao na ujio wa Mama Shein
katika Wilaya yao ya Kaskazini A na kumuhakikishia kuwa wataendelea kuiunga
mkono CCM ili iendelee kushika hatamu.
Akiwa katika ukumbi wa Hoteli ya Sea Cliff huko Kama, Wilaya ya
Kaskazini B, Unguja Mama Shein alitoa wito kwa jamii kuchukua juhudi za
makusudi katika kuhifadhi mazingira na kuielimisha jamii juu ya utunzaji wa
mazingira hayo.
Alisema kuwa maeneo
ambayo kwa miaka mingi yamekuwa yakitegemewa kuwa na vianzio vikubwa vya maji,
yameathiriwa kutokana na ukataji wa miti, na ujenzi wa nyumba bila ya
kuzingatia mipango mizuri sambamba na shughuli za uchimbaji wa mchanga na
udongo ambazo zimeathiri sana ndani ya Mikoa hapa nchini.
Pia, Mama Shein ambaye
alipata mapokezi makubwa katika mkoa huo, alisisitiza suala zima la
kushirikiana na Serikali katika kupambana na ukatili na udhalilishaji wa
wanawake na watoto kwani katika jamii kumeendelea kusikika vitendo vya aina hiyo
ambavyo ni aibu, na ni kinyume cha maadili na mafundisho ya Dini.
Nae Mama Fatma Karume aliwataka
akinamama wa Jumuiya hiyo kutojali maneno na kasumba mbali mbali zinazosambazwa
na wapinzani ambazo hazina manufaa wala nafasi kwa CCM.
Nae Mama Asha Balozi aliendelea
kutoa wito kwa wananchi wa Mkoa huo kupiga vita suala zima la udhalilishaji wa
wanawake na kusisitisha mashirikiano ndani ya Jumuiya ya UWT.
Nao wanajumuiya ya UWT
Wilaya ya Kaskazini B, walieleza kuwa haja ya kuongezewa mitaji na mikopo katika
vikundi vyao ili kipato wanachokipata kiweze kukidhi haja ya malengo yao.
Wakieleza suala zima
la udhalilishaji wa wanawake na watoto na kueleza kuwa suala zima la
mashirikiano katika kesi za ubakaji sambamba na changamoto zilizopo katika mtiririko
mzima wa hukumu za kesi za aina hiyo.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment