Habari za Punde

Kiwanda cha Sukari Mahonda chahitaji eneo zaidi la ardhi kufanikisha uzalishaji

Na Mwashungi Tahir                Maelezo 

Meneja wa Biashara wa Kiwanda cha sukari  Mahonda Bw Pronav Shah amekumbushia ombi lao kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar la kukipatia Kiwanda maeneo zaidi ya ardhi  ili kuimarisha uzalishaji wa sukari katika kiwanda hicho.

Amesema kiwanda  hulazimika kusitisha uzalishaji wa sukari kutokana na upungufu wa miwa na huku ikwalipa mishahara wafanyakazi bila ya kuzalisha na kukipelekea kiwanda kuingia katika hasara.

 Ameeleza hayo  Ofisini kwake Mahonda wakati   Kamati ya Fedha, Biashara na Kilimo ya Baraza la Wawakilishi ilipofanya ziara  ya kutembelea  kiwanda  hicho  kuangalia mafanikio na  changamoto zinazowakabili . 

Bw Pronav Shah ameieleza Kamati hiyo ya Baraza la Wawakilishi kuwa sehemu kubwa ya mashamba ya kiwanda imevamiwa na wananchi wa kawaida  kwa shughuli zao ikiwemo ujenzi wa nyumba huku wakijua kuwa ni sehemu ya kiwanda na kupunguza ukubwa wa  shamba hilo. 

“Sehemu kubwa ya shamba la miwa hivi sasa limevamiwa na watu wa kawaida na inasemekana wanaungwa mkono na baadhi ya viongozi wa shehia,” amelalamika Meneja huyo.

 Katika hatua nyengine Meneja huyo wa Biashara ameiomba serikali   kuwapatia  bima  ili inapotokea ajali waweze kufidiwa gharama za ajali hiyo. 
Amesema  iwapo serikali itawapatia bima itawasaidia hasa kwa vile mara kwa mara mashamba ya miwa hushambuliwa na moto ambao haujulikani chanzo chake licha ya juhudi za uchunguzi zinazofanwa na jeshi la Polisi. 

Bw. Pronav  Shah ameshauri kuruhusiwa kupanua soko la kuuza sukari katika soko la Tanzania Bara ambalo hivi sasa bei ni tafauti na Zanzibar ama kuuza sukari yao Zanzibar kwa bei ya soko la Tanzania Bara.

 Nae mwenyekiti wa Kamati ya Fedha , Biashara na Kilimo Yussuf Hassan ameutaka uongozi wa Kiwanda hicho kuendeleza  uzalishaji  wa sukari ili kuwasaidia vijana kupata  ajira na kufikia lengo la kujitosheleza kwa bidhaa hiyo.

Ameuhakikishia uongozi wa kiwanda hicho kuwa ombi lao la kupata ardhi zaidi kwa ajili ya kuongeza mashamba ya miwa watalifikisha katika ngazi za juu ili liweze kupatiwa ufumbuzi.

Amesema Serikali inafahamu kuwa kufanikiwa kwa Kiwanda cha sukari cha Mahonda  itakuwa ni kivutio kwa wawekezaji wengine  kuja kuwekeza Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.