Habari za Punde

Balozi Seif aahirisha Mkutano wa Nne wa BLW

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  akitoa Hoja ya kuahirisha Mkutano wa Nne wa Baraza la Tisa la Wawakilishi lililokuwa likiendelea kwenye Ukumbi wa Majengo yake yaliyopo Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.(Picha na Hassan Issa OMPR) 

Na Othman Khamis OMPR. 

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekusudia kulifanyia marekebisho makubwa ya Miundombinu eneo la Kijangwani ili liweze kutumika kama Kituo Kikuu cha magari ya Abiria katika azma yake ya kuendeleza uboreshaji wa haiba ya Mji wa Zanzibar Kibiashara.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akitoa Hoja ya kuahirisha Mkutano wa Nne wa Baraza la Tisa la Wawakilishi lililokuwa likiendelea kwenye Ukumbi wa Majengo yake yaliyopo Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Alisema Serikali haijawa na nia mbaya kama baadhi ya watu wanvyofikiria ya kuwahamisha Wafanyabiashara wanaouza mbao katika eneo hilo la Kijangwani na kuwatengea sehemu maalum iliyotengwa kwa ajili yao katika Mtaa wa Daraja Bovu.

Balozi Seif aliwakumbusha  Wananchi kwamba  zoezi hilo la kudumu litaendelea kutekelezwa katika maeneo mengine ya  Mji na Vitongoji vyake  ambayo baadhi ya wafanyabiashara waliamua kuyavamia kwa kufanya biashara zao bila ya utaratibu na mpango maalum.

“ Kama nilivyoeleza katika Hotuba yangu ya kuahirisha Mkutano wa Tatu, Serikali itaendelea na mkakati wake wa kuufanya Mji wa Zanzibart kuwa na haiba inayostahiki. Tunawaomba Wananchi waendelee kuyaunga mkono mazoezi ya aina hiyo ”. Alisema Balozi Seif.

Akizungumzia  kelele za Wananchi dhidi ya vilabu vya pombe vinavyoonekana kuzidi kufunguliwa katika maeneo ya makaazi ya Watu Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  alisema taratibu za ufunguzi wa nyumba za biashara hizo lazima uzingatie sheria  zilizopo.

Alisema Serikali haikatazi watu au Mtu kufurahi baada ya saa za majukumu ya kazi, lakini  kinachokusudiwa kuzingatiwa zaidi kwa wahudumu wa nyumba hizo ni kuheshimu mila, utamaduni wa kutoudhi wakaazi wa maeneo husika ili kuendelea kuimarisha heshima ya Nchi.

Balozi Seif  aliwaagiza wamiliki wa nyumba hizo kudhibiti upigaji ovyo wa muziki katika maeneo ya makaazi ya wananchi kwani baadhi ya nyumba hizo zimekuwa zikiendeleza kelele kubwa wakati wa usiku.

Kuhusu suala la Amani ambalo limekumbwa na tabia iliyochipuka ya baadhi ya watu hasa vijana kuharibu mali, mimea na mali za Wananchi na Taasisi za Umma Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alivitaka vyombo vya dola kuwachukulia hatua kali wale wote watakaopatikana na hatia ya kuhatarisha amani na utulivu uliopo Nchini.

Balozi Seif  aliwapa pole Wananchi wa Kijiji cha Pwani Mchangani Kisiwani Unguja na Kikosi cha Vyuo vya Mafunzo Tungamaa Kisiwani Pemba kwa kuharibiwa mazao na vipando vyao.

Aliwaasa wazee na wazazi katika maeneo mbali mbali Nchini kuendelea kuwasihi watoto kutojiingiza katika vitendo vya uvunjifu wa amani vikiwemo vile vya ufisadi wa kuharibu mali na mazao ya watu.

Balozi Seif  aliwahakikishia wananchi kwamba Serikali itaendelea kusimamia amani na utulivu uliopo nchini na wale watakaojitokeza  kuvuruga hali hiyo vyombo vya dola havitasita kuwashughulikia kwa mujibu wa sheria na taratibu za Nchi.

Wajumbe wa Mkutano huo wa Nne wa Baraza la Tisa la Wawakilishi Zanzibar walijadili na kupitisha Miswaada Minne ya Sheria ambayo ni pamoja na Mswaada wa Sheria ya kufuta na kutunga upya Sheria ya Ushahidi Sura ya Tano na masuala yanayohusiana na nayo.

Mswaada mengine ni Mswaada wa Sheria ya kurekebisha Sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Nambari 2 ya Mwaka 2005 kuweka masharti bora zaidi kwa ajili ya ufanisi na usimamizi imara wa Mfuko na mambo yanayohusiana nayo.

Uliofuata ni Mswaada wa Sheria wa kufuta sheria ya manunuzi na uuzaji wa mali za Serikali nambari 9 ya mwaka 2005 na kutunga sheria inayoanzishwa  mamlaka ya manunuzi na uuzaji wa mali za Umma na kuweka masharti mengine yanayohusiana nayo.

Ukamalizia mswaada wa sheria wa kutunga sheria ya usimamizi wa fedha za Umma kwa kuweka masharti bora ya udhibiti na kusimamia fedha za umma na kuweka mambo mengine yanayohusiana na hayo na kufuta sheria ya usimamizi wa fedha za Serikali nambari 12 ya mwaka 2005.

Baraza la Wawakilishi Zanzibar limeahirishwa hadi Jumatano ya Tarehe 15 Febuari Mwaka 2017 mnamo saa 3.00 za Asubuhi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.