STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar
21.12.2016

RAIS wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amezipongeza juhudi zinazochukuliwa
na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika
kuimarisha sekta za maendeleo.
Dk. Shein aliyasema
hayo leo, Ikulu mjini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na aliyekuwa Mwakilishi Mkaazi wa Benki ya Maendeleo
ya Afrika (AfDB) Dk. Tonia Kandiero, aliyefika Ikulu kwa ajili ya kumuaga baada
ya kupewa majukumu mengine ya kuwa Mkurugenzi
Mkuu wa Benki ya (AfDB) Kuisini mwa Afrika.
Dk. Shein alitumia
fursa hiyo kutoa shukurani zake binafsi
kwa kiongozi huyo pamoja na Benki ya (AfDB)
kwa namna inavyotoa ushirikiano wake kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
katika kuimarisha miradi ya maendeleo hapa nchini.
Katika mazungumzo
hayo, Dk. Shein alieleza kuwa Benki ya (AfDB) imekuwa ikichukua juhudi za
makusudi katika kuhakikisha miradi mbali mbali ya maendeleo hapa Zanzibar inaimarika
na kuendelea kuwasaidia wananchi wote wa Unguja na Pemba.
Alisema kuwa (AfBD)
siku zote imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha Zanzibar inapata mafanikio
katika kuendeleza miradi yake mbali mbali ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii
hivyo, Dk. Shein alizipongeza juhudi hizo ambazo zimekuwa chachu katika
maendeleo ya Zanzibar.
Kwa upande wa
uimarishaji wa sekta ya maji katika Mkoa wa Mjini Magharibi, Dk. Shein alieleza
kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefaidika kwa kupata mkopo wenye
masharti nafuu kutoka Benki hiyo ambao utasaidia katika kutatua changamoto ya
uhaba wa maji katika Mkoa huo na si muda
mrefu changamoto hiyo itakuwa historia.
Alieleza kuwa uhaba wa
maji umekuwa ni changamoto kwa baadhi ya
wakaazi wa mji wa Zanzibar kwani hiyo ni kutokana na kuongezeka kwa idadi ya
watu hapa nchini sambamba na tatizo la tabianchi ambalo linapelekea maji kupungua
kwa kiasi kikubwa katika vyanzo vyake.
Pamoja na hayo, Dk.
Shein alipongeza hatua za Benki hiyo katika kuiunga mkono Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar kwenye sekta ya Mawasiliano ya barabara kwa Unguja na Pemba ambazo zipo zilikuwa
zimemalizika pamoja na zile ambazo zinatarajiwa ujenzi wake kuanza na nyengine
kuendelezwa.
Alieleza kuwa miradi ya barabara kisiwani Pemba itasaidia katika kuendeleza
sekta za maendeleo ikiwemo sekta ya utalii sambamba na juhudi nyengine
zinazoendelelea kuchukuliwa na serikali kisiwani humo ikiwemo uimarishaji wa
uwanja wa ndege ambayo nayo itachangia kukua kwa sekta hiyo ya utalii kisiwani
humo.
Aidha, Dk. Shein
alisema kuwa mbali ya Benki hiyo kutoa ushirikiano wake katika kuimarisha sekta
mbali mbali za maendeleo hapa nchini zikiwemo
maji, barabara, kilimo, nishati, afya, elimu na utawala bora pia, imeweza kutoa
mashirikiano katika nyanja nyengine za kijamii, kiuchumi na kimaendeleo.
Nae aliyekuwa Mwakilishi Mkaazi huyo wa Benki ya Maendeleo ya Afrika
(AfDB) Dk. Tonia Kandiero alimueleza Dk. Shein kuwa Benki yake itaendelea
kuiunga mkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kutambua na kuthamini
juhudi inazozichukua katika kuleta maendeleo endelevu hapa nchini.
Dk. Kandiero
alipongeza na kusifu mashirkiano mazuri yaliopo kati ya Benki hiyo na Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Rais Dk. Shein na kueleza kuwa
hatua hiyo imesaidia sana katika kuleta maendeleo zaidi hapa Zanzibar.
Kiongozi huyo alimuhakikishia
Dk. Shein kuwa miradi yote inayosimamiwa na Benki hiyo itakamishwa ikiwemo
miradi ya ujenzi wa barabara zikiwemo barabara ya Mahonda -Mkokotoni yenye urefu wa km 31, Fuoni
-Kombeni km 8.6, Pale- Kiongele km 4.6 na Matemwe -Muyuni yenye urefu wa km
7.6.
Pamoja na hayo, Dk.
Kandiero ambaye amefanya kazi zake hapa Tanzania kwa takriban miaka sita, alimueleza
Dk. Shein kuwa (AfDB) itaimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano wake na
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kutoa
pongezi za pekee kwa Dk. Shein na serikali anayoiongoza kwa kusimamia
vyema miradi ya maendeleo.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment