STATE HOUSE
ZANZIBAR
OFFICE OF THE
PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 10.12.2016
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewataka
viongozi wa Serikali kutoa taarifa kwa wananchi kwa mujibu wa sheria na
miongozo iliyopo kwani suala hilo ni la kikatiba na msingi muhimu wa kuimarisha
maadili na kukuza utawala bora.
Dk. Shein aliyasema hayo leo huko katika viwanja vya Victoria Garden mjini
Zanzibar, katika maadhimisho ya siku ya Maadili na Haki za Binaadamu, hafla
ambayo ilihudhuria na viongozi mbali mbali wa Serikali na weatendaji wake,
vyama vya siasa, wake na wananchi.
Katika maelezo yake Dk. Shein alisema
kuwa kuna baadhi ya viongozi wanadhani
kwamba anapowahimiza kuwa watoe taarifa kwa wananchi wanadhani kwamba jukumu
hilo si lao badala yake ni la vyombo vya habari au ni kazi ya watu maalum.
Alisema kuwa dhana hiyo si sahihi kwani
kazi hiyo ni ya viongozi wote kwa mujibu wa Katiba Ibara ya 18, kifungu cha (2)
na kusisitiza kuwa licha ya Serikali kuweka utaratibu maalum unaowataka
viongozi wa Serikali watoe taarifa kwa wananchi, bado wapo ambao hawatekelezi
vyema agizo hilo.
“Katika kuimarisha utawala bora, tunapaswa
tuhakikishe kuwa tunatoa taarifa sahihi na za kuaminika kwa wanaostahiki,
wanawananchi na watu waliochuni ya dhamana zetu”,alisema Dk. Shein.
Akieleza kuhusiana na suala la rushwa Dk.
Shein alisema kuwa serikali zote mbili hapa nchini zinaendelea kuchukua juhudi
katika kupambana na rushwa, uhujumu wa mali za umma na kuimarisha uwajibikaji,
imeanza kuza matunda.
Aidha Dk. Shein alisema kuwa, viongozi
wamechaguliwa na wameteuliwa ili waongoze Wizara na Idara zao kwa mujibu wa
taaluma, uzoefu na sifa maalum walizonazo, hivyo wawe mstari wa mbele kutoa rai
mbali mbali za maendeleo na kusimamia utekelezaji wake badala ya kusubiri
maagizo kutoka ngazi za juu.
Alisema kuwa kila kiongozi aliyepewa jukumu
la kuongoza wananchi au kusimamia taasisi ya Serikali ni lazima atekeleze
jukumu hilo kama inavyostahiki kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo hasa
kwa wale viongozi waliokula viapo.
Dk. Shein alisema kuwa Tume ya Maadili ya
Viongozi wa Umma tayari imeshaanza kutoa elimu juu ya umuhimu wa madili ambapo
aliwahimiza viongozi wote waliohusika wahakikishe
wanarejesha fomu ya tamko la rasilimali na madeni zilizotolewa hivi karibuni
kwa viongozi wote waliotajwa kwenye sheria Na.4 ya mwaka 2015 kwa wakati
uliopangwa.
Sambamba na hayo, Dk. Shein alisisitiza
kuwa kila mmoja ahakikishe anatoa taarifa kama ilivyoelezwa na taarifa zote
zinazotolewa ziwe sahihi kwani utoaji wa taarifa za uongo ni kosa kwa mujibu wa
sheria hiyo ya maadili.
Dk. Shein alilitilia mkazo suala zima la
kushikamana katika kupiga vita unyanyasaji wa watoto na akina mama huku
akisisitiza matumizi mazuri ya mitandao sambamba na kupiga vita matumizi ya
dawa za kulevya.
Mapema Waziri wa Katiba, Sheria, Utumishi
wa Umma na Utawala Bora alieleza kuwa juhudi zitaendelea kuchukuliwa katika
suala zima la utawala bora, kusimamia maadili pamoja na rushwa ili kuhakikisha
lengo lililokusudiwa linafikiwa.
Nae Mwenyekiti wa Tume ya Maadili, Asaa Ahmada
Rashid alisema kuwa kauli mbiu ya siku hiyo inayosema ‘Imarisha utawala bora
kwa kukuza uadilifu, uwajibikaji, haki za binaadamu na mapambano dhidi ya
rushwa” imebeba ujumbe muwafaka kwa taasisi za utawala bora.
Aidha, Mwenyekiti huyo alitumia fursa
hiyo kueleza juhudi za Serikali katika kuimarisha utawala bora ikiwa ni pamoja
na kuunda taasisi mbali mbali ikiwemo Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma
ambayo imepewa jukumu la kusimamia Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma,
Sheria Na 4 ya mwaka 2015.
Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania
Bi Anna Liboro Senga kwa upande wake alisisitiza umuhimu wa utawala bora,
maadili na wajibikaji ambapo pia alitoa ujumbe wa UN katika kuadhimisha siku ya
Maadili duniani.
Bi Senga, alitumia fursa hiyo kueleza
kuwa bila ya kuwepo kwa maadili amani na utulivu haitokuwepo huku akitoa
pongezi kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Dk. Shein kwa
kusimamia amani na utawala bora.
Mapema Dk. Shein alipokea maandamano
kutoka kwa Wafanyakazi wa Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee. Vijana, Wanawake
na Watoto.
Sherehe hizo zilipambwa na vionjo mbali
mbali vikiwemo ngoma ya kibati kutoka kikundi cha Vijana Ngoma Group, Mchezo wa
Kuigiza kutoka kundi la Black Root Investment chini ya Makombara pamoja na
utenzi mwanana.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024
2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment