Habari za Punde

Upotevu wa mashuka hosital ya Wete, Afisa Mdhamini atoa wiki mbili yapatikane

Na Salmin Juma , Pemba

AFISA Mdhamini Wizara ya Afya Pemba Bakar Ali Bakar amebaini kuwepo na  upotevu wa mashuka 36 na mito 20 katika Hospitali ya Wete  na kuuagiza uongozi wa hospitali hiyo kuhakikisha vifaa hivyo vinapatikana ndani ya kipindi cha wiki mbili .

Amesema upotevu wa mashuka na mito hiyo ameubaini kufuatia ziara yake ya kukagua  utoaji wa huduma kwa wagonjwa katika hospitali hiyo ambapo alipokea malalamiko kutoka kwa wagonjwa juu ya ubovu wa mashuka katika vitanda vya wodi ya watoto.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana Ofisini kwake ,Bakar amesema  ziara hiyo aliyoifanya akiwa ameambatana na maafisa wa Wizara hiyo Pemba , alishuhudia  vitanda vikiwa na mashuka machakavu .

Ameeleza kwamba hali hiyo ilimfanya ahoji sababu zinazowafanya kuendelea kutumia mashuka yaliyochakaa  licha ya Serikali kuandaa mazingira mazuri ya upatikanaji huduma bora kwa wagonjwa ikiwemo suala la malazi .

“Tumekuwa tukipokea malalamiko kutoka kwa wagonjwa kwamba huduma katika wodi ya watoto sio mzuri , na nimebaini kwamba hali inachangiwa na watendaji ambao sio waaminifu ambao wameficha mashuka hayo , hivyo nimewataka kuyarejesha ndani ya wiki mbili ”alieleza.

Afisa Mdhamini alizidi kufahamisha kwamba , uchunguzi wa awali unaonyesha kwamba mashuka na mito hiyo imechukuliwa na watendaji kwani hakukuwa na kitendo cha kuvunjwa ghala la Hospitali hiyo .
Aidha alifahamisha kuwa mtendaji ambaye atabainika kujihusisha na upotevu huo atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani kwanin atakuwa ameenda kinyume na maadili ya utumishi wa umma .

“Hata kama watarejesha au wasirejeshe hatua za kisheria zitachukuliwa , hatuwezi kukaa mkimiya huku mali za serikali zinawanufaisha wahache kwa maslahi yao binafsi hii hatuwezi kuivumilia na tutaonyesha mafano kisheria ”alisisitiza.

Awali wakizungunza na mwandishi wa habari baadhi ya akinamama ambao watoto wao wamelazwa kwenye wodi hiyo wamelalamikia uchakavu  wa mashuka kwenye vitanda vya wagonjwa na kusema kwamba kwa sasa wanatumia mashuka wanayokuja nayo kutoka nyumbani kwao .

 Wamesema mashuka  hayo yaliyotandikwa kwenye vitanda ni machakavu  na  hayana ubora kwa ajili ya kulaza mgonjwa .

“Mashuka yaliyotandikwa kwenye vitanda vya hospitali wodi ya watoto hayana ubora na kwa sasa mgonjwa analazimika kutandaika mashuka waliyokuja nayo kwani yaliyopo yamechakaa ”alieleza  Fatma Juma.

Hata hivyo wameiomba serikali kuandaa utaratibu wa kukagua vitanda hivyo mara kwa mara kuangalia usafi wa mashuka kwani kila mgonjwa anamaradhi yake .

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.