Habari za Punde

Vijana Nchini Watakiwa Kuwa Wazalendo na Waadilifu Kuenzi Mchango wa Baba Taifa

Na Beatrice Lyimo. Maelezo.
VIJANA nchini wametakiwa kuwa wazalendo, waadilifu, kufanya kazi kwa bidii na kufuata maadili ili kuenzi mchango wa waasisi walioleta uhuru wa Tanzania.
Wito huo umetolewa leo na Katibu Tawala Mkoa wa Arusha Bw. Richard Kwitega alipokuwa akizungumza kuhusu mafanikio ya miaka 55 ya uhuru tangu nchi ilipopata Uhuru mwaka 1961.
Alisema kuwa katika kipindi cha uongozi wa Mwalimu Nyerere, watumishi walikuwa wawajibikaji, hivyo watendaji vijana hawana budi katika kufuata mienendo hiyo ili kuweza kusonga mbele katika maendeleo ya nchi.
“Vijana kwa ujumla tunatakiwa kujenga uzalendo wa nchi, nchi itajengwa na sisi, uhuru tulionao tuutumie katika uzalishaji ili kuweza kusonga mbele” alifafanua Katibu Tawala huyo.
Kwitega alisema Serikali ya Awamu ya Tano kupitia kauli mbiu yake ya Hapa Kazi tu imejikita katika kuhamasisha wananchi kufanya kazi kwa bidii ambapo Mwalimu Nyerere alihamasisha Uhuru na Kazi akimaanisha uhuru ni kufanya kazi kwa bidii
Alisema Watanzania tunapaswa kujivunia kupata Uhuru kutoka katika makucha ya ukoloni, hivyo ni wajibu wa jamii kudumisha utamaduni wa kitanzania, mahusiano tuliyonayo na mataifa mengine ili kuiletea nchi maendeleo ya haraka. 


Aidha aliwaasa wananchi kwa ujumla kufanya kazi kwa bidii na  kutunza amani iliyopo ili kuzidi kuwaenzi waasisi waliopigania uhuru kwa hali na mali na kuliletea taifa maendeleo ya haraka.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.