Na Frank Mvungi. Maelezo Dar es Salaam
SERIKALI kupitia Wizara ya
Kilimo, Mifugo na Uvuvi imetoa kiasi cha Tsh. Milioni 440 katika mwaka 2015/16
kwa vikundi 73 vya uvuvi ili kuiwezesha sekta ya uvuvi kuongeza tija na
kuchangia kikamiliu katika ujenzi wa uchumi wa Viwanda nchini.
Hayo yamesemwa jana Jijini Dar es
salaam na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Yohana
Budeba wakati wa mahojiana maalum katika Kipindi cha “TUNATEKELEZA” kinachoratibiwa
na Idara ya Habari (MAELEZO) kurushwa hewani kupitia Kituo cha Televisheni ya
Taifa (TBC).
Dkt. Budeba alisema Serikali
imekusudia kuinua mchango wa sekta ya uvuvi kwa kuviwezesha vikundi vya
wafugaji kuendesha shughuli zao kwa ufanisi mkubwa kwa kuvipatia ruzuku na
mikopo kutoka katika taasisi mbalimbali za kifedha ikiwemo mabenki na mifuko ya
hifadhi za jamii.
“Wizara inashirikiana na
Halmashauri za Wilaya nchini katika kuwapatia fedha vikundi vyote vya wafugaji
samaki waliopo katika ushirika, ambapo asilimia 40 hutolewa na Serikali
ikihusisha ruzuku ya zana bora za uvuvi ikiwemo injini, nyavu na chakula cha
samaki” alisema Dkt. Budeba.
Kwa mujibu wa Budeba alisema
katika kuhamasisha ujenzi wa uchumi wa viwanda nchini kupitia mchango wa sekta
hadi kufikia sasa Serikali imeanisha jumla ya viwanda 48 vya usindikaji samaki
nchini, ikiwemo viwanda vidogo 36 vilivyopo katika ukandwa wa pwani wa bahari
ya hindi, viwanda 11 vilivyopo kanda ya ziwa na kiwanda kimoja kilichopo katika
ukanda wa ziwa Tanganyika.
Aidha Dkt. Budeba alifafanua kuwa
katika kuwajengea uwezo vikundi hivyo, Serikali imekusudia kuajiri Maafisa
Ugani katika kila kata nchini, hatua inayolenga kuongeza thamani ya mazao ya
uvuvi na kuweza kutumika kama pato na lishe kwa wananchi.
Akizungumzia kuhusu maendeleo ya
sekta hiyo, Dkt. Budeba alisema mpaka sasa Tanzania ina jumla ya mabwawa 22,000
yenye uwezo wa kuzalisha tani 10,000 za samaki, ambapo katika kipindi cha miaka
mitano ijayo Serikali imekusudia kuvuna tani 50,000 za samaki, hatua inayolenga
kuiwezesha nchi kujitosholeza na akiba ya samaki.
Akifafanua zaidi, Dkt. Budeba
aliongeza kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa wananchi wanafuga
kitaalamu zaidi, ambapo Serikali inaendelea kutoa mafunzo kwa wataalamu wake
katika vituo vya kutotoleshea vifaranga vya samaki vilivyopo Mbegani, Nyegezi
na Igunga.
Alisema mikakati iliyopo kwa sasa ni pamoja na kuwawezesha
wavuvi kukopa kutoka Benki ya Kilimo ili
kuwawezesha kuzalisha samaki na pia kuanzisha ufugaji wa Samaki katika
maeneo mbalimbali kwa kutumia mfumo wa vizimba.
Dkt. Budeba alisema katika kuvutia wawekezaji katika sekta
hiyo tayari Serikali imetoa amesema leseni 76,000, hatua inayolenga kuongezeka
kiwango cha uzalishaji wa samaki nchini.
Alibainisha kuwa miongoni mwa
changamoto zinazoikabili Wizara hiyo kwa sasa ni pamoja na uhaba wa Maafisa
ugani, ambapo kwa sasa ina maafisa ugani 800 ingawa mahitaji halisi ni maafisa
ugani 16,000.
No comments:
Post a Comment