Habari za Punde

Rais Dk Shein ahimiza wananchi kujipangia muda wa mazoezi
STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar                                                                1.1.2017

---
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewataka wananchi wasikae kusubiri hadi kuambiwa na madaktari kufanya mazoezi  ndipo wakaanza kukurupuka kwani mara nyingi mtu anapopewa ushauri wa kufanya mazoezi na daktari huwa athari fulani zimeshaanza kujitokeza mwilini mwake.

Hivyo, Dk. Shein aliwasisitiza wananchi  kuzingatia hekima ya wazee kwamba kinga ni bora kuliko tiba na badala yake ni vyema kila mmoja akajiwekea muda maalum wa kufanya mazoezi yanayolingana na afya na umri wake.

Dk. Shein aliyasema hayo leo mara baada ya kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Siku ya Mazoezi Kitaifa huko katika uwanja wa Amaan, Mjini Zanzibar yalioanza uwanja wa Tumbaku hadi uwanja wa Amaan mapema saa 12 za asubuhi,

Viongozi mbali mbali walishiriki mazoezi hayo akiwemo Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ali Hassan Mwinyi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd,  viongozi wengine wa dini na serikali pamoja na vikundi vya mzoezi kutoka Unguja, Pemba na Tanzania Bara.

Katika hotuba yake Dk. Shein alisema kuwa mazoezi ni lazima hasa katika dahari hizi ambapo mfumo wa maisha umekuwa na changamoto nyingi zitokanazo na kuongezeka kwa mahitaji na hamkani za maisha ya kisasa hapa nchini na duniani kote.

Alisema kuwa hivi sasa jamii imeacha utamaduni wa kutembea kwa miguu na kwa baskeli badala yake hupanda vyombo vya moto hata kwa masafa mafupi huku akieleza athari za vyakula vya kisasa vikiwemo mahanjumati, michuzi ya mafuta, mapochopocho yalionona ambayo hupikwa kwa samli za kisasa na kuacha vyakula vya asili.

Dk. Shein aliwahakikishia wananchi kwamba Serikali itaendelea na juhudi za kuimarisha michezo na kuviunga mkono vikundi mbali mbali vya mazoezi ya viungo ikiwa ni pamoja na kuweka miundombinu bora ya michezo.

Alisema kuwa Serikali imedhamiria kujenga viwanja vya michezo katika kila wilaya Unguja na Pemba ambapo tayari imeanza mchakato kwa viwanja vitatu kikiwemo kiwanja cha Kitogani Mkoa wa Kusini Unguja, Mkoa wa Kaskazini Unguja na Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Dk. Shein aliwaahidi wana mazoezi na wana michezo wote kwamba Serikali italifanyia kazi ombi lao la kuwapatia mafunzo walimu wa vilabu vya mazoezi ili waendeshe michezo na mazoezi kwa njia na mbinu za kitaalamu zaidi.

Aidha Dk. Shein alilitaja jambo linalodhorotesha juhudi za kuimarisha michezo kuwa ni uchache wa wadhamini katika ngazi zote za michezo ambapo kampuni nyingi zilizopo Zanzibar na Wafanyabiashara bado hawana mwamko wa kutosha wa kutumia michezo kwa kujitangaza.

Hivyo Dk. Shein aliutaka uongozi wa Wizara ya Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo kwa kushirikiana na Baraza la Michezo la Zanzibar pamoja na vyama vya michezo kubuni mikakati mipya kwa kuzishawishi Kampuni na Wafanyabiashara kutumia michezo kujitangaza.

Dk. Shein alisisitiza michezo kuzingatia nidhamu na kuwataka wanamichezo wasisahau kuwa dhamira ya michezo ni kuburudisha na kuunganisha na sio kugombanisha.

Kwa upande wa kombe la Mapinduzi , ambapo mara hii michuano maalum ya vijana katika Wilaya zote za Unguja na Pemba imeanzishwa na  kusisitiza kuwa timu za Zanzibar lazima zifanye vizuri ili kombe la Mapinduzi mara hii libaki hapa hapa Zanzibar.

Dk. Shein alitoa shukurani kwa uongozi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo na uongozi wa Chama cha Mchezo wa Mazoezi ya Viungo (ZABESA)  kwa maandalizi mazuri ya Bonanza hilo na hatimae kutoa vyeti maalum kwa wale wote waliofanikisha Bonanza hilo.

Nae Waziri wa Habarim Utalii, Utamaduni na Michezo, Rashid ... aliahidi kuwa Wizara yake itaendelea kushirikiana na vikundi vya michezo na mazoezi huku akitumia fursa hiyo kumpngeza Dk. Shein kwa kuanzisha siku maalum ya mazoezi Kitaifa.

Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar, Sharifa Khamis alimpongeza Dk. Shein kwa kuwathamini na kuwajali wanamichezo wa Zanzibar na kueleza jinsi wanavyofarajika na juhudi zake katika kuinua sekta ya michezo hapa nchini.

Mapema katika risala yao wafanyamazoezi ya viungo walieleza kwamba kutofanya mazoezi kunaongeza hatari ya kupatwa kwa ugonjwa wa moyo na kuzisha hatari ya shinikizo kubwa la damu na pia huongeza maradufu uwezekano wa kufa kwa shinikizo la damu na kiharusi.

Walieleza kuwa mwamko wa kufanya mazoezi nchini umeongezeka huku wakieleza umuhimu wa mazoezi kwa watoto na hatimae kueleza changamoto yao ya kuhitaji kupatiwa walimu wa vilabu mafunzo ya kufanya mazoezi kitaalamu zaidi kwa maslahi ya Taifa.

Bi Rukia Ramadhani nae hakua nyuma katika kutoa burudani ambayo ilitumbuiza hadhara iliyokuwepo kwa nyimbo yake maalum ya kumpongeza Dk. Shein  ambaye ni muasisi wa Bonanza hilo ambapo pia wanamazoezi hao nao walipata fursa ya kuonesha mazoezi mepesi pamoja na vikundi vya sarakasi navyo vilionesha umahiri wao.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.