STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 4.1.2017

JITIHADA za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika
kuziimarisha huduma za bandari haziwezi kufanikiwa iwapo waliopewa dhamana za
kuzisimamia na kufanya kazi bandarini hapo wataendelea kufanya kazi kwa mazoea.
Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein aliyasema hayo katika
hafla ya uzinduzi wa vifaa vipya vya kufanyia kazi bandarini, hafla
iliyofanyika katika Bandari ya Malindi mjini Unguja ikiwa ni miongoni mwa
shamrashamra za miaka 53 ya Mapinduzi ya matukufu ya Zanzibar.
Aliwataka wafanyakazi
Bandarini hapo kuwa waaminifu na waadilifu zaidi, kuepuka urasimu katika kutoa
huduma, kujiepusha na vitendo vya rushwa na zaidi kuhakikisha kuwa wateja
wanahudumiwa kwa muda mchache bila ya kukiuka taratibu ziliopo.
Sambamba na hayo, Dk.
Shein alikemea tabia ya baadhi ya wafanyakazi wa Bandari kufanya kazi kinyume
na maadili na taratibu za kazi zao na kueleza kuwa endapo wakijulikana wale
wote wanaofanya kazi hivyo watashughulikiwa ikiwa ni pamoja na kushtakiwa ama
kufukuzwa kabisa kazi.
Pia, Dk. Shein
alieleza jinsi ya mapato yanavyopotea katika Bandari hiyo ya Zanzibar kutokana
na wafanyakazi wachache wasiotimiza wajibu wao ipasavyo ambao hufanya hila na
udanganyifu ikiwa ni pamoja na kupitisha vitu vilivyopitwa na muda wa matumizi vikiwemo
vyakula.
Kutokana na hilo, Dk.
Shein ametoa wiki moja mambo hayo yasitokee tena, ikiwa ni pamoja na kukomesha hila
zinazofanywa bandarini hapo na baadhi ya wahusika za kutoa makontena bure na kupelekea
kuikosesha Serikali mapato.
Aidha, Dk. Shein
alisema kuwa hatua ya ununuzi wa vifaa hivyo ni mafanikio ya utekelezaji wa
Ilani ya Uchaguzi wa CCM ya mwaka 2015 hadi 2020 ambayo imeanza kutekelezwa kwa
kasi ikiwa ni pamoja na kuiendeleza Bandari ya Malindi kwa kuipatia vifaa na
kukamilisha ujenzi wa bandari mpya ya kuhudumia mizigo katika eneo la
Mpigaduri.
Pamoja na hayo, Dk.
Shein alisema kuwa Serikali itaiimarisha na kuiendeleza Bandari ya Mkoani kwa
kuipatia vifaa vya kisasa vya kuhudumia abiria na mizigo ambapo pia, Serikali
inaendeleza mazungumzo na wawekezaji kwa lengo la kuiimarisha Bandari ya Wete kutokana
na umuhimu wake kwa Serikali, wananchi wa Mkoa wa Kaskazini Pemba na watumiaji
wote.
Kwa upande wa Mkoa wa
Kaskazini Unguja, Dk. Shein alisema kuwa Serikali itaendelea kuiimarisha gati
ya Mkokotoni kwa kukamilisha ujenzi wa jeti kwa ajili ya huduma za usafiri wa
wananchi hasa wa Mkokotoni na Tumbatu.
Dk. Shein alisisitiza
haja kwa uongozi wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji pamoja na
Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika hilo kuwaangalia wafanyakazi wanaoendesha vifaa
hivyo kiafya na kimaslahi na kutoa pongezi zake kwa ununuzi wa vifaa hivyo.
Nae Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na
Usafiorishajim Ali Abeid Karume alisema kuwa mafanikio hayo yametokana na
uongozi bora wa Dk. Shein ambapo licha ya azma ya Serikali kujenga Bandari mpya
huko Mpigaduri lakini alisisitiza haja ya kununuliwa vifaa hivyo muhimu
bandarini hapo.
Mapema Katibu Mkuu wa
Wizara hiyo Mustafa Aboud Jumbe alisema kuwa jumla ya TZS Bilioni 11.8
zimetumika katika kununua vifaa hivyo vikiwemo Kreni 2, Terminal Tractor 2,
Terminal Trailer 2, Reach Stacker 3, Empty Container Hanler 1, Forklift 3 na
maboya ya solar 7.
Alisema kuwa vifaa
hivyo vinatoka nchini Sweden, Belgium, Italy na Ujerumani ambapo vimeingia
nchini kati ya Mei hadi Disemba, 2016 na tayari vimeanza kutumika kwa majaribio
ambapo alisisitiza kuwa kuwasili kwa vifaa hivyo kutasaidia sana kuongeza uwezo
wa Bandari kuhudumia mizigo pamoja na kuongeza kasi ya ushushaji na upakiaji wa
mizigo.
Viongozi mbali mbali
walihudhuria katika hafla hiyo akiwemo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif Ali Idd, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid na
viongozi wengine wa Serikali vyama vya siasa na dini.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment