STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 27.2.2017

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein ameelezea umuhimu wa
michezo na kusisitiza kuwa michezo hujenga udugu, umoja, mapenzi na mshikamano
katika jamii na wala sio ugomvi na uhasama.
Dk. Shein ambaye pia,
ni Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, aliyasema hayo huko katika ukumbi wa CCM,
Mkoa wa Mjini uliopo Amani mjini Zanzibar mara baada ya kukabidhi vifaa vya
michezo kwa vijana kwa ajili ya maandalizi ya Ligi ya Mpira wa Miguu kwa Timu
18 za Unguja ikiwa ni kusherehekea miaka 40 ya kuzaliwa kwa CCM.
Katika hotuba yake Dk.
Shein aliwataka vijana washindane katika mchezo huo na wala wasigombane kwani lengo
la michezo pamoja na kuanzishwa kwa mashindano
hayo ni kujenga umoja baina yao.
Dk. Shein aliwataka
vijana hao wacheze vizuri ligi hiyo ili kuendelea kukipa heshima na mapenzi
chama chao cha CCM na kueleza kuwa Ilani ya chama hicho ina vifungu
vinavyoeleza kutekelezwa kwa sekta hiyo ya michezo.
Aliongeza kuwa
mashindano hayo yana lengo la kuimarisha chama, kutoa vipaji kwa vijana na
kuwataka viongozi wa Majimbo kuwaunga mkono na kuwasaidia vijana wao
watakaoshiriki katika ligi hiyo kwani na wao wanawajibu wa kufanya hivyo.
Pia, Dk. Shein alikubali rai iliotolewa na Mwakilishi wa
Jimbo la Uzini ambaye pia, ndio mdhamini wa mashindano hayo Mohammed Raza ya kuanzisha mashindano kama hayo
kisiwani Pemba pamoja na mashindano ya vijana katika skuli za Mikoa yote ya
Zanzibar na kuahidi kuyadhamini kwa kushirikiana na wahisani wengine wa michezo
hapa nchini.
Dk. Shein ambaye
aliongeza kuwa uzinduzi wa mashindano
hayo utafanyika tarehe 24 mwezi ujao kati ya Timu ya Mfenesini na Mpendae
mchezo utakaopigwa katika uwanja wa Amaan mjini Zanzibar.
Nae Makamo wa Pili wa
Rais wa Zanzibar ambaye pia, ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Balozi Seif Idd,
alitumia fursa hiyo kueleza umuhimu wa mashindano hayo kwa vijana na kusisitiza
kuwa ligi hiyo itazidi kukuza mashirikiano na umoja kwa vijana wa chama hicho.
Mapema Mdhamini wa
mashindano hayo, Mohammed Raza alisema kuwa mchakato wa kuanzishwa kwa
mashindano ya ligi hiyo ni miongoni mwa utekelezaji wa Ilani ya CCM sambamba na
kutekeleza malengo ya kuwatumikia wananchi na utekelezaji wa ahadi kwa
wananchi.
Raza alisema kuwa kazi
kubwa iliyopo hivi sasa ni kuwatumikia wananchi bila ya ubaguzi na kusisitiza umuhimu
wa mashirikiano ya pamoja kwa wanaCCM ili kufikia malengo waliyojiwekea huku
akieleza azma yake ya mashindano hayo kuyapeleka kisiwani Pemba.
Katika taarifa ya Ligi
hiyo iliyosomwa na Omar Suleimn, Mjumbe wa wa Kamati ya Michuano hiyo, ilieleza
kuwa Umoja wa Vijana wa CCM kwa kushirikiana na CCM Mkoa wa Mjini, wameamua
kuanzisha ligi ya Majimbo ya Mpira wa miguu ambayo itashirikisha timu 18, Timu
9 kutoka Majimbo ya Mkoa wa Mjini kichama, Timu ya Tawi la Afisi Kuu ya CCM,
Timu ya CCM Family na Timu zilizo salia zitatoka Mkoa wa Magharibi, Kusini na
Kaskazini Unguja.
Taarifa hiyo ilieleza
kuwa mara baada ya kupata wazo la kuanzisha ligi hiyo, iliundwa Kamati ya
maandalizi ya mashindano hayo yenye Wajumbe 12 chini ya uongozi wa CCM Mkoa wa
Mjini ambapo mshauri wa Kamati hiyo Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub
Mohammed Mahmoud.
Kwa maelezo ya taarifa
hiyo lengo la mashindano hayo ni kusherehekea miaka 40 ya kuzaliwa kwa CCM,
kuinua vipaji vya vijana katika mchezo wa mpira wa miguu sambamba na kuunga
mkono kauli ya Dk. Shein ya kutaka Zanzibar iwe na vuguvugu la michezo kwani
wanaamini kuwa hoja hiyo imelenga utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
Vijana hao pia,
walitoa salamu zao za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tazania John
Pombe Magufuli kwa jitihada zake za kupambana na biashara haramu ya madawa ya
kulevya.
Mshindi wa kwanza wa
mashindano hayo atapata kikombe, gari na nishani ambapo mshindi wa pili atapata
milioni tatu na mshindi wa tatu atapata milioni mbili pamoja na zawadi nyengine
zitakazotolewa katika mashindano hayo.
Mbunge wa Jimbo la
Mpendae Salim Turky kwa upande wake
akiwa pia, ni mkereketwa wa michezo hapa nchini aliahidi kununua gari hiyo kwa
ajili ya mshindi wa kwanza wa mashindano hayo ambapo wafanyabiashara wengine na
wakereketwa wa chama hicho waliahidi kuchangia mashindano hayo zikiwemo fedha
taslim.
Miongoni mwa Timu
zitakazoshiriki mashindano hayo ni Jimbo la Mpendae, Jangombe, Kikwajuni,
Kwahani, Amani, Shaurimoyo, Chumbuni, Malindi, Magomeni, Kiembesamaki,
Mfenesini, Dimani, Mahonda, Uzini, Kaskazini A, Kusini, Afisi Kuu ya CCM pamoja
na timu ya CCM Family.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address:
2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment